loader
Picha

Samia atoa maagizo matano

MAKAMU wa Rais, Samia Hassan Suluhu ametoa maagizo matano kwa Watanzania katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, ikiwemo kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto, lakini pia kuimarishwa kwa usalama katika maeneo ya umma.

Aidha, ameelezea namna Serikali ya Awamu ya Tano ndani ya miaka mitano tangu ishike madaraka, ilivyofanikiwa kuinua nafasi za wanawake katika ngazi za uamuzi ikiwemo bungeni, mahakamani na Baraza la Mawaziri na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya tatu katika Jumuiya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Katika hatua nyingine, Rais John Magufuli alitoa salamu za kuwapongeza wanawake wote nchini, kwa kuadhimisha siku hiyo muhimu.

“Mchango wenu kwa familia, jamii na taifa hauna mfano. Serikali ninayoiongoza itaendelea kuwathamini, kuwaheshimu na kujenga mazingira bora yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yenu ipasavyo,” alisema Rais Magufuli kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Akihutubia kwenye maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika Viwanja wa Halmashauri wilayani Bariadi mkoani Simiyu jana, Samia alitaja maagizo hayo kuwa ni kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, wanawake wajitokeze kwa wingi na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo kuwaunga mkono wanawake watakaojitokeza na kuwapigia kura kwa wingi.

Aidha, aliwahimiza wanawake na wanaume, kuhakikisha wajawazito wanahudhuria kliniki na kujifungulia kwenye vituo vya afya na viongozi wa serikali za mitaa na wahusika katika sheria na vyombo vya dola, kusimamia na kuhakikisha watu wote wanaofanya ukatili wa watoto wanachukuliwa hatua.

Maagizo mengine ni kuwataka watanzania wote kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na mila na desturi, zinazochochea vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kuimarisha kamati za ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto, kuimarisha usalama wa maeneo ya umma na kutunga sheria ndogo katika ngazi za halmashauri kulinda haki za wanawake na watoto.

“Katika Salamu za Rais John Magufuli ametuahidi kuwa serikali itaendelea kuweka msukumo kwa sekta zote nchini ili kukuza usawa wa kijinsia na maendeleo ya wanawake,” alisema Makamu wa Rais.

Akizungumzia namna Serikali ya Tanzania ilivyofanikiwa kufikia maazimio ya Beijing kuhusu haki za wanawake, alisema imepiga hatua kubwa kutoka na ushiriki mkubwa wa wanawake katika ngazi za maamuzi, kiasi cha kuifanya Tanzania kushika nafasi ya pili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nafasi ya tatu SADC.

Alisema tangu serikali iingie madarakani, Bunge la Tanzania lina jumla ya wabunge wanawake 126 sawa na asilimia 36.7, ambayo ni juu ya uwiano wa SADC ambao ni asilimia 30.

“EAC Tanzana ni wa pili tukiongozwa na Rwanda na SADC ni wa tatu. Hili ni ongezeko la nafasi za wanawake kwa asilimia 30 la juu tangu tupate uhuru. Baraza la Wawakilishi kuna asilimia 38 ya wanawake, tumeshawahi kuwa na Spika wa Bunge Anne Makinda, mwanamke, tuna manaibu spika wawili Mgeni Juma wa Baraza la Wawakilishi na wa Bunge, Tulia Ackson,” alisema Makamu wa Rais.

Kwa upande wa Mahakama, Samia alisema idadi ya majaji Mahakama Kuu ni asilimia 30, Mahakama ya Rufaa asilimia 38, Baraza la Mawaziri wanawake asilimia 18 na manaibu mawaziri asilimia 33.

“Lakini CCM imeamua kutoa nafasi ya Makamu wa Rais kwa wanawake kwa roho safi kabisa. Hii ni ishara na dalili kwamba usawa wa kijinsia nchini umefikia pazuri,” alisisitiza.

Alisema wanawake ni sehemu muhimu ya ujenzi wa taifa na kutoa mfano kuwa kwenye kilimo, uwiano ni wanawake watatu kwa mwanamme mmoja, viwanda wafanyakazi mahiri na makini ni wanawake.

Hata hivyo, alionya juu ya ongezeko la vitendo vya ubakaji wa watoto wakiwemo wa kiume. Aliwataka Watanzania hususani wazazi wote kuwa walinzi wa watoto, vinginevyo taifa linaenda pabaya.

“Ubakaji kwa watoto wetu wa kike na wa kiume unaathiri pakubwa sana, haya yanarudisha sana maendeleo kwa nchi yetu. Ukatili huu hauna sura kwa upande mmoja, wanafanyiwa wa kike na wakiume, hili si jambo zuri sote tuwe walinzi wa watoto wetu” alisema.

Alisema kwa mujibu wa takwimu, kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili yanayoripotiwa, ambapo mwaka 2016 yalikuwa ni 31,136, mwaka 2017 yalifikia 41,414, kati yake 27,945 wanawake na wanaume 13,771.

“Tunavigeuza vitoto vyetu vya kiume tunajenga sura gani? Taifa letu linaelekea siko, wote tusimame turekebishe hali hii,” alisema.

Alisisitiza kuwa serikali ina dhamira ya kuhakikisha inatokomeza tatizo la ukatili dhidi ya wanawake kwa mujibu wa Katiba. Wanawake ndio walezi wa familia na watoto ndio nguvu kazi.

Serikali inatekeleza mpango wa kutokomeza ukatili ifikapo 2020/22. Alionya juu ya mtindo ulioibuka na kuzusha juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa corona nchini.

Badala yake, aliwataka watanzania wawe mstari wa mbele kujikinga kwa kufuata maelekezo ikiwemo kuacha kukumbatiana, kupigana mabusu na kushikana mikono.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema Siku hiyo ya Wanawake, inalenga kujenga hamasa na uwezo wa wanawake katika kushirikishi na kunufaika na maendeleo. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya sasa na baadaye”.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi