loader
Picha

Maeneo 23 ya mafanikio ya JPM

MAFANIKIO ya kishindo, kujivunia na ya kihistoria yanayojumuisha maeneo 23 yamepatikana katika Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi kifupi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango (pichani) alielezea mafanikio hayo juzi wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/21.

“Mafanikio haya makubwa yamepatikana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuanzia mwaka 2016/17 hadi Januari 2020 chini ya utawala wa Rais Magufuli na Serikali yake ya CCM,” alisema Dk Mpango.

Dk Mpango alisema katika bajeti ya mwaka 2019/20, Sh trilioni 12.25 zilitengwa kugharamia miradi ya maendeleo, ambapo kati ya hizo Sh trilioni 9.74 zilikuwa fedha za ndani na Sh trilioni 2.51 fedha za nje. Miongoni mwa mafanikio makubwa ni Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge (SGR) ambao kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 300) umefikia asilimia 75 na Morogoro – Makutupora (kilometa 422) asilimia 25.

Hadi Septemba 2019 mradi huu umezalisha ajira 13,117. Aidha, zabuni zenye thamani ya Sh bilioni 664.7 zimetolewa kwa wazabuni na makandarasi wa ndani 640.

Sh trilioni 2.96 zimetumika kugharamia mradi huu, zikijumuisha Sh bilioni 237.5 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020. Pia ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere wa megawati 2,115, ambao kazi zilizokamilika ni ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi kama njia ya kusafirisha umeme, barabara kwa kiwango cha changarawe, mfumo wa maji, mawasiliano ya simu na nyumba za makandarasi na ujenzi wa daraja la muda namba 2.

Pia utafiti wa miamba na udongo na uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini wenye urefu wa mita 147.6, kuelekea kwenye mtaro wa chini kwa chini wa kuchepua maji na mtambo wa kuchakata kokoto namba moja, ambapo utekelezaji wa mradi wote umefikia asilimia 10.74.

Dk Mpango alisema Sh trilioni 1.28 zimetumika kugharamia mradi huu, ikijumuisha Sh bilioni 200.7 ambazo zimetolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020. Mradi huu umezalisha ajira zipatazo 3,074 na makandarasi wa kampuni 10 za Tanzania wamepata fursa.

“Serikali imeendelea kuboresha Shirika la Ndege Tanzania kwa kununua ndege mpya 11, kati yake ndege nane (8) mpya zenye thamani ya shilingi trilioni 1.27 zimepokelewa na malipo ya awali ya shilingi bilioni 85.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu (3) yamefanyika ambapo ndege mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni aina ya De Havilland Dash 8-400,” alisema Dk Mpango.

Miradi kadhaa ya umeme imekamilika, ukiwemo wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Makambako –Songea ambao Sh bilioni 160.1 zimetumika.

Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga unaendelea, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 63 na Sh bilioni 219.4 zimetumika katika kipindi cha Julai 2016 hadi Januari 2020. Pia inaendelea na utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kupitia REA, ambapo vijiji 8,641 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa umeme sawa na asilimia 70.4.

Alisema katika kipindi cha Julai 2015 hadi Januari 2020, Sh trilioni 1.53 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huu, ikijumuisha Sh bilioni 207.2 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020.

Alisema serikali inaendelea kuboresha huduma ya majisafi na salama vijijini na mijini, ambayo utekelezaji wa miradi 875 unaendelea ikijumuisha miradi 802 ya maji vijijini na miradi 73 ya maji mijini na 75 ya maji vijijini imekamilika.

Serikali imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kugharamia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vituo 540 vya kutolea huduma za afya, ikijumuisha vituo vya afya 361, hospitali za halmashauri za wilaya 71, hospitali za zamani tisa na zahanati 99. Watumishi 477 wameajiriwa na kupangiwa vituo.

Aibainisha kuwa serikali inaendelea na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III), ambao kaya 1,067,041 zenye wanakaya 5,130,001 zimetambuliwa na kuandikishwa katika vijiji na mitaa 9,627 kwenye halmashauri 159 Tanzania Bara na kaya 32,248 zenye wanakaya 169,999 katika Shehia 204 za Zanzibar na ruzuku ya fedha Sh bilioni 968.73 imehawilishwa katika kaya hizo. Kati ya hizo, Sh bilioni 935.94 ni kwa Tanzania Bara na Sh bilioni 32.79 ni kwa Zanzibar.

Katika sekta ya madini, serikali imepitia na kurekebisha sera, sheria na mikataba ya uwekezaji katika sekta ya madini, ambapo marekebisho hayo yamewezesha kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya serikali (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84), kuanzishwa kwa masoko 28 na vituo 25 vya ununuzi wa madini, na kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne vya umahiri katika maeneo ya Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni na kuendelea na ujenzi wa vituo vya Songea, Mpanda na Chunya.

Serikali imepata mafanikio mengi katika maeneo mengine yakiwemo ya viwanda, kilimo, uvuvi, ufugaji, ujenzi wa barabara na madaraja na usajili wa wajasiriamali na utoaji haki mahakamani.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi