loader
Picha

Tuwe makini na watoto wetu kipindi hiki

JUZI serikali ilitoa tamko la kufunga shule zote nchini na vyuo, ikiwa ni utekelezaji wa tahadhari dhidi ya maambukizi ya homa ya virusi vya corona, ambayo hadi sasa wagonjwa watatu wamethibitika kuugua ugonjwa huo hapa nchini.

Hatua hiyo ni njema na ya kuungwa mkono, kwa sababu inatoa mwanya kwa wanafunzi kutulia nyumbani na kupunguza kasi ya maambukizi, kwani ugonjwa huo unasambaa kwa kasi kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu mwenye virusi, hivyo akikohoa au kupiga chafya, virusi husambaa.

Pamoja na hatua hiyo, pia serikali imepiga marufuku mikusanyiko, matamasha, shughuli za michezo na mikutano inayokutanisha watu wengi, ikiwa ni njia ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo, ambao hadi sasa umeshaua zaidi ya watu 7,000 duniani kote.

Mlipuko wa ugonjwa wa corona ulianzia China mwishoni mwaka Desemba 2019 katika Jimbo la Hubei katika Mji wa Wuhan.

Hadi sasa umeshasambaa kwenye mataifa zaidi ya 160 duniani na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 7,000 duniani kote na wengine zaidi ya 180,000 wameambukizwa.

Hata hivyo, wengi walioathirika na ugonjwa huo waliopata matibabu, wamepona na baadhi wameruhusiwa kurejea kwao katika nchi tofauti.

Wakati ugonjwa huo ukisambaa kwa kasi sasa kwenye nchi za Afrika baada ya kupunguza kasi barani Asia, hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa na jamii ili kuhakikisha janga hilo halienei na kuleta madhara zaidi.

Hivyo basi, nafasi ya wazazi wakati huu shule na vyuo vimefungwa ni kuhakikisha watoto wanatulia nyumbani na kuacha kuzurura ovyo kwa ndugu na jamaa au kwenda kusoma masomo ya ziada.

Ikumbukwe kwamba serikali imefunga shule na vyuo vyote nchini ili kutoa mwanya wanafamilia kutulia nyumbani, ili kupunguza kasi ya maambukizi, kwa kuhakikisha watu hawasafiri au kutembea ovyo, kama hawana sababu ya kufanya hivyo.

Ugonjwa wa corona ni janga la dunia, hivyo wazazi, walezi na jamii tuone uzito wa jambo hili na kuwahimiza watoto wetu kutulia nyumbani na kujisomea, badala ya kuona wamepata nafasi ya kuzurura ovyo.

Kufanya hivyo ni kuongeza uwezekano wa kupata maambukizi na kuondoa ile maana ya kufunga shule.

Kwa wanafunzi wanaopenda kutembea, huu sio muda wa likizo, ni muda wa kukaa ndani kusoma na kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huu, kwani mtu mmoja akiambukizwa kwenye familia, ni rahisi kuusambaza kwenye familia nzima na hivyo kufanya wote kuwa hatarini.

Tuone umuhimu wa tamko la serikali na kuchukua hatua ya kubaki nyumbani na kuacha tabia ya kuzurura ovyo, kwani wapo watu ambao hawawezi kutulia, bali wanapenda kuzurura kwa ndugu mmoja hadi wa mwisho. Na kwa ndugu, huu sio muda wa kupokea wageni.

Kila mtu abaki kwake ili kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu.

Nasema hili kwa sababu wapo watakaodhani kumwambia ndugu kwamba usije kwangu ni kumtenga au kubagua. La hasha!. Huu ni wakati sahihi wa kufanya hivyo kwa maslahi mapana ya afya zetu .

Tukumbuke kwamba ‘Kinga ni bora kuliko tiba’ na pia tuzingatie ushauri wa wataalamu wa afya wa maelekezo ya jinsi ya kujilinda, kwa kunawa mikono na kuhakikisha hatushiki maeneo yoyote ya uso kabla ya kunawa mikono yako.

JUZI Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza kamati za maafa katika ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi