loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wagonjwa wa corona wafikia watano

JUMLA ya wagonjwa waliothibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Covid 19 nchini sasa ni watano. Wamefikia idadi hiyo baada ya wagonjwa wawili wapya, kubainika ndani ya saa 24 kutoka jana.

Aidha, kutokana na kubainika kwa wagonjwa hao, serikali imewaweka karantini watu 66 jijini Dar es Salaam na 46 jijini Arusha, kwa ajili ya kuchukua sampuli zao na kuwapima.

Lengo la hatua hiyo ni kubaini kama nao wameathirika, kutokana na kushirikiana kwa namna moja au nyingine na wagonjwa waliobainika. Katika taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wagonjwa hao wapya wawili ni Watanzania wenye umri wa miaka 40 walioingia nchini kwa nyakati tofauti, ambapo walipopimwa walibainika kuwa na virusi hivyo vya corona.

Alisema Mtanzania wa kwanza, alisafiri Uswisi, Denmark na Ufaransa kati ya Machi 5 hadi 13, mwaka huu na kurejea Machi 14, mwaka huu. Mwingine alisafiri Afrika Kusini kati ya Machi 14 hadi 16, mwaka huu na kurejea nchini Machi 17, mwaka huu.

Juzi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza kuwa na ongezeko la wagonjwa wawili wa corona, akiwemo raia wa Ujerumani kutoka Zanzibar na raia wa Marekani jijini Dar es Salaam na hivyo kufanya jumla ya wagonjwa wote wenye maambukizi kufikia watano, akiongezwa na Mtanzania wa kwanza, Isabela Mwampamba.

Mipaka Alipotembelea mpaka wa Namanga jijini Arusha jana, Ummy aliwataka maofisa afya kwenye maeneo yote ya mipakani, kufanya uchunguzi wa kina kwa wananchi wanaopita kwenye mipaka, ikiwemo maeneo yasiyo rasmi Alisema umakini ni muhimu katika uchunguzi wa ugonjwa huo haswa maeneo ya mipakani.

BoT yanena kuhusu noti Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewatoa hofu wananchi kuhusu maambukizi ya virusi vya corona kupitia noti za fedha, ikisema zimetengenezwa kwa namna ambayo zinaweza kuzuia vimelea kubakia kwenye noti.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki ya BoT, ilisema kwa kuwa noti hizo zinapita katika mikono, wananchi wazingatie miongozo inayotolewa na mamlaka zenye dhamana ya jamii.

Benki hiyo ilishauri wananchi kufanya miamala kwa kutumia njia mbadala za malipo, kama vile simu za mkononi, intaneti na kadi, bila kulazimika kufika kaunta za benki au ATM kuchukua noti. Mwendokasi, Daladala Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeagiza Mabasi yaendayo Haraka (BRT) kubeba idadi ya abiria kulingana na idadi iliyoainishwa kwenye leseni zake.

Aidha, mabasi yote ya mijini yajulikanayo kama daladala, yametakiwa kubeba abiria kulingana na idadi ya viti katika basi. Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe, alisema hayo jana wakati akielezea mkakati wa kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwa treni, magari ya abiria na mizigo. Pia, aliagiza waendesha teksi, pikipiki za magurudumu mawili na matatu, wahakikishe abiria wao wanapaka dawa ya kuua virusi mikononi kabla ya kupanda chombo husika.

Alilitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), kuhakikisha treni zinapuliziwa dawa za kuua virusi kila mwisho wa safari. Viongozi wanena Katika mwendelezo wa kutoa elimu sahihi kwa umma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alivishukuru vyombo vya habari kwa kutoa elimu kwa umma.

Lakini, alitahadharisha juu ya habari za uzushi na taharuki kuhusu ugonjwa huo, zinazotolewa na mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari.

“Kumeanza changamoto mitandao ya uzushi mitandaoni, niko hapa kuwakumbusha wananchi wanaotumia mitandao ya kijamii kuwa sheria ipo, ni vyema sana kutangaza habari sahihi na ambazo mtu una uhakika nazo. Kama huna uhakika ni afadhali kusikiliza muziki tu kuliko kusambaza habari ya uongo,” alisisitiza Dk Abbasi.

Alisema pia kuna baadhi ya magazeti yanaandika habari za kuzusha kuhusu ugonjwa huo wa corona. “Gazeti linaandika kiama chaja, jamani mimi nafikiri ugonjwa wa corona unadhibitika,” alisema Dk Abbasi.

Alisema serikali na watalaamu wake iko kazini, ikipambana na kudhibiti kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa huo, hivyo hakuna haja kwa vyombo vya habari kutia hofu wananchi isiyo na msingi. Jafo, Ndalichako Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo aliewataka wakuu wa mikoa, kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa corona, kwa kutoa elimu kwa wananchi mikoani mwao.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alitoa rai kwa wanafunzi wote wa shule za serikali, vyuo vya kati na vya juu, kuchukua tahadhari zote katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya corona Alisema katika kipindi hiki cha ugonjwa wa corona, serikali imeamua kufunga shule za awali, msingi, sekondari, vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa huo, hivyo ni vema wanafunzi kuchukua jukumu la kujilinda na kuchukua tahadhari mbalimbali zinazotolewa Dereva teksi Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Milipuko, Dk Janeth Mghamba alisema dereva teksi aliyembeba mgonjwa wa corona na wenzake 26, wapo salama.

Alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya washukiwa hao 27. Alisisitiza kuwa vipimo vyao, vimechunguzwa zaidi ya mara tatu kwenye Maabara Maalum ya Taifa. Jukwaa la Wahariri Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alisema vyombo vya habari nchini vimefanya kazi kubwa hadi sasa.

Lakini, alisema wahariri hawana budi kuendelea kutoa habari za ugonjwa wa COVID- 19, hasa njia za kuzuia maambukizi na kukabiliana na ugonjwa huo, iwe ajenda ya kudumu. Imeandikwa na Lucy Ngowi, Evance Ng’ingo, Halima Mlacha (Dar), Veronica Mheta (Arusha) na Peti Siyame (Sumbawanga).

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi