loader
Dstv Habarileo  Mobile
SHUKURU JOSEPH ‘Jack Umeme’ :  Mwanamke shupavu aliyebobea utengenezaji wa magari

SHUKURU JOSEPH ‘Jack Umeme’ : Mwanamke shupavu aliyebobea utengenezaji wa magari

“NASHUKURU. Sasa najiona mwanamke niliyefanikiwa licha ya hapo zamani baadhi ya watu wakiwemo wanawake wenzangu, walikuwa wakinibeza, hasa waliponiona nimechafuka kutokana na mazingira ya kazi yangu yaliyonifanya nionekane hivyo.”

Hiyo ni kauli ya Shukuru Joseph (31) maarufu kwa jina la ‘Jack Umeme’ alipokuwa akizungumza na mwandishi wa safu hii, kuhusu harakati za maisha yake, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8.

Jack Umeme ni mwanamke aliyefanikiwa kupitia fani ya utengenezaji wa magari au ‘makanika’. Jack ambaye ni mama wa watoto wawili, anasema kuwa aliamua kujiita jina hilo la Jack, ili kulikwepa jina la Shukuru, alilopewa na wazazi wake, kutokana na kutopendezwa nalo. Anasema kadri siku zilipopita, kutokana na kujikita kwenye taaluma yake ya ufundi wa umeme wa magari, watu waliamua kumbatiza jina hilo la ‘Jack Umeme’. Anasema kwa sasa jina lake hilo ni maarufu, kiasi kwamba linatajwa pia na nyimbo za wasanii mbalimbali.

BIASHARA ZAKE

Kwa sasa Jack anamiliki duka kubwa la vifaa vya magari katika eneo la Ilala Dar es Salaam na ameajiri mafundi wanne, wanaofanya shughuli ndogo za ufundi wa magari katika duka hilo. Anasema haikuwa rahisi, kufikia mafanikio hayo, kwani amepitia mateso na machungu mengi. Hata hivyo, anasema silaha yake kubwa maishani ni kujituma, na kila mara hukumbuka maneno aliyowahi kuambiwa na baba yake.

Kwa mujibu wa Jack baba yake aliwahi kumwambia kuwa “hakuna nafasi yako kwenda sekondari, isipokuwa ufundi wa magari, kama hutaki utarudi kijijini.” Anasema kauli hiyo aliyoambiwa na baba yake ambaye kwa sasa ni marehemu, ilimfanya avurugikiwe kiakili, lakini ilimpa moyo wa kupenda kujituma. Jack anasema mwanzoni alihisi baba yake huyo hakuwa na mapenzi naye. Lakini, aliamua kukaa kimya ili kuepusha mzozo na baba yake. Hivyo anasema baadaye aliamua kuitikia mwito wa baba yake na kujiunga na ufundi.

ALIKOSOMA

Akizungumzia historia ya maisha yake, anasema alihitimu darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Mabibo wilayani Kinondoni Dar es Salaam mwaka 2002. Baada ya hapo alipelekwa Mbeya, ambapo ndipo asili ya wazazi wake na alikaa kwa kipindi cha miezi sita. Kisha alikwenda Malawi kwa dada yake na kuishi huko kwa mwaka mmoja, kisha alirejea tena jijini Dar es Salaam kuanza mafunzo ya ufundi.

MAFUNZO YA KAZI

“Niliporejea Dar es Salaam nilijiunga na mafunzo ya lugha ya Kiingereza katika Chuo cha Upendo kilichokuwepo Mwananyamala. Nilisoma mwaka mmoja kuanzia mwaka 2005 hadi 2006 nilipoanza rasmi mafunzo ya ufundi umeme wa magari katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),” anasema.

Anasema baada ya kuhitimu mafunzo hayo ya miaka miwili NIT, alienda katika Kampuni ya Scania na kufanya mafunzo ya ufundi wa magari kwa vitendo kwa miezi mitatu. Baadaye alihamia katika gereji ya mtu binafsi iliyopo eneo la Kinondoni, alikofanya mafunzo ya vitendo kwa miezi saba. Jack anasema baada ya hapo, alihamia katika gereji nyingine iliyopo eneo la Ilala na kufanya kazi chini ya Victor Koelo, maarufu Kidedea. Anasema Koelo ni mtu muhimu kwake na alikuwa bosi mzuri kwa kazi, kwani alimfundisha mambo mengi, yaliyomfanya awe bora katika fani ya ufundi hadi sasa.

MAANDALIZI YA KUJITEGEMEA

Anasema baada ya kufanya kazi kwa muda na bosi wake huyo, baadaye bosi huyo aliamua kuhamishia shughuli zake eneo la Kinondoni na kumtaka wahame wote. Lakini, aligoma kuhamia eneo la Kinondoni, kwa kuwa alipendezwa na eneo hilo la Ilala. Hivyo, alibakia Ilala na kujiunga na vijana wawili, aliowataja kwa majina ya Dick na Bahati maarufu Kachara.

Anasema akiwa na vijana hao wawili, walianzisha duka lao la kuuza vipuri vya magari katika ofisi ndogo waliyopanga. Hata hivyo, duka hilo halikuwa na vitu vingi, kwa kuwa hawakuwa na mtaji mkubwa.

Walipambana hivyo hivyo kuendesha maisha yao ya kila siku, huku yeye akijiwekea akiba ya fedha kidogo. Baada ya kufanya kazi kwa muda na vijana hao, walikubaliana kuachana na ofisi hiyo; na kuanza kupanga duka kubwa, ili liweze kuchukua vitu vingi. Waliamini kuwa kufanya hivyo, kungewapa hamasa ya kununua vipuri vingi zaidi na kuviingiza dukani mwao, hivyo kujiongezea wateja.

AANZA KUJITEGEMEA

“Lakini wakati tunakubaliana hilo, kichwani kwangu nilikuwa na wazo la kutaka kufanya kazi peke yangu. Mara nyingi roho ilikuwa inaniuma kuona tunagawana fedha tulizokuwa tunazipata. Jambo lingine nilibaini kuwa wenzangu wapo pamoja muda mwingi na mambo yao mengi yalikuwa ni siri yao. Hivyo niliona vyema nifanye mambo yangu mwenyewe,” anasema Jack.

Wakati fulani wenzake hao, walimuarifu kuwa wamepata chumba kikubwa, ambacho wangekitumia kama ofisi, iliyotakiwa kulipiwa Sh 300,000 kwa mwezi. Alikubaliana nao kuwa angechangia kodi baada ya kurejea kutoka Mbeya, alipokuwa likizo.

“Niliamua kuondoka Mbeya kesho yake kurejea Dar es Salaam na moja kwa moja nilienda kulipia ofisi hiyo bila kuwajulisha. Nilifanya hivyo kwa kuwa nilishajipanga kufanya kazi peke yangu. Nilimlipa mwenye nyumba Sh milioni 2.5; na kumuomba nitampelekea baadaye kiasi cha shilingi milioni moja na yeye alikubali,” anasema Jack.

Anasema kesho yake alikutana na vijana hao, ambapo walimtaka aende kulipia ofisi hiyo ili waanze kazi. Lakini, aliwafahamisha kuwa tayari ameshailipia. Aliwaeleza kuwa amefanya hivyo ili kujiandaa na maisha ya kufanya kazi peke yake, jambo alilodai kuwa liliwafanya wenzake hao kumchukia. Baada ya hatua hiyo, walikubaliana kugawana vitu vyote, vilivyokuwa dukani kwao kwa usawa kila mmoja.

Kuanzia hapo safari yake ya maisha ya kujitegemea kikazi ilipoanza rasmi. Anasema kuwa wakati anaanza, duka lake peke yake, lilikuwa lina vifaa vichache. Hata hivyo, kadri siku ziilivyokwenda, mtaji wake ulizidi kuongezeka na jina lake likazidi kupata umaarufu. Hali hiyo ilimwezesha kuanza kusafiri kwenda Dubai, kununua vipuri na kuachana na ununuaji wa vifaa hivyo kutoka Kariakoo, alikokuwa akinunua muda mrefu, kutokana na kuwa na mtaji mdogo.

“Hivi sasa nashukuru mambo yanaenda vizuri na mikakati yangu ni kufungua ghala la kuuzia vipuri vya magari aina zote, pengine kushinda maduka yote yaliyopo Dar es Salaam. Nina uhakika nitafanikiwa hilo kutokana na dhamira niliyo nayo na mipango mizuri niliyojiwekea,” anasema Jack.

MAFANIKIO YAKE

Akizungumzia mafanikio aliyoyapata kutokana na shughuli hiyo, Jack anasema imemwezesha kumiliki gari mbili za kutembelea na daladala moja. Pia anasema amefanikiwa kujenga nyumba mbili, moja ikiwa eneo la Mbezi. Pia, anamiliki viwanja kadhaa anavyotarajia kuvijengea nyumba siku zijazo.

CHANGAMOTO ZAKE

Anasema changamoto alikuzokutana nazo hadi kufikia mafanikio aliyonayo leo ni pamoja na kudharauliwa, hasa kipindi alichokuwa anajifunza kazi yake. Anasema muda mwingi alionekana mchafu, kutokana na mazingira ya kazi yake hiyo ya ufundi.

“Kazi hii ilinifanya wakati mwingine watu washindwe kunitambua kuwa nina jinsia ya kike au ya kiume, lakini hayo yote hayakunifanya nikate tamaa, badala yake nilizidi kukomaa, kwani wakati mwingine hao waliokuwa wakinidhihaki walikuwa hawana hata shilingi 1,000 mfukoni,” anasema Jack.

VITU ANAVYOPENDA

Anasema vitu anavyovipenda katika maisha yake ni pamoja na kuona watu wakijishughulisha, hasa wanawake wenzake. Pia, anasema anapenda kuwa karibu na marafiki na kubadilishana nao mawazo, kwani kufanya hivyo, kunamjengea mipango mipya ya maisha kila siku.

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi