loader
Picha

Tuache utani, ubishi kudhibiti corona

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limeutangaza ugonjwa wa corona kuwa janga la dunia na kutaka kuunganishwa kwa nguvu kuudhibiti.

Kwa mujibu wa WHO, ugonjwa huo ulioripotiwa kwa mara ya kwanza Desemba 31 mwaka jana katika Mji wa Wuhan, Jimbo la Hubei nchini China, mpaka sasa umeenea katika nchi 169 kati ya 194 zilizopo duniani na umesababisha watu zaidi ya 209,839 kuugua na vifo zaidi ya 8,778. Tanzania ni moja kati ya nchi zenye waathirika wa corona.

Tangu kutangazwa rasmi mgonjwa wa kwanza nchini Machi 16 mwaka huu, idadi sasa imefikia sita, kati yao wamo raia wa kigeni na Watanzania.

Kufuatilia taarifa hii, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya imechukua hatua mbalimbali kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo ikiwamo kutenga maeneo ya karantini kwa washukiwa, elimu ya afya kuhusu dalili, namna ya kujikinga na kukinga wengine na namba za simu za kutoa taarifa.

Hata hivyo, pamoja na hatua hizo za Serikali, ikiwamo kuhamasisha watu kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka na kutumia vitakasa mikono (sanitizer) mara kwa mara, bado kuna upotoshaji mkubwa wa taarifa katika mitandao ya kijamii zinazokinzana na ukweli wa wataalamu wa afya.

Kwa mfano katika mabasi ya mwendo kasi hivi sasa ni lazima kupaka vitakasa mikono kabla ya kuingia garini.

Cha kushangaza ni kwamba bado kuna watuwanagoma wanapotakiwa kupaka kinga hii sijui kutokana na imani za dini au ujeuri na kiburi tu.

Binafsi natamani tangazo la Serikali litoke iwe lazima kutumia vitakasa mikono, kunawa na kinga nyingine.

Tusipochukua hatua ya makusudi katika vyombo hivi vya usafiri vya umma, maofisini, masokoni na hospitalini, tunaweza kuliingiza taifa katika matatizo makubwa ya kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa huu na tukashindwa namna ya kuudhibiti.

Nashauri wakati viongozi wetu wa nchi, dini na wataalamu wa afya wanapoendelea kutoa maelekezo kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa huu, ni vyema tukazingatia kwa lazima maelezo na taarifa sahihi badala ya kueneza upotoshaji na kugomea kutekeleza mambo wakati ni kwa faida yetu.

Ifikie mahali Watanzania tuwe makini kufuatilia taarifa katika vyanzo sahihi na kuzifanyia kazi kuliko kuleta mzaha katika jambo linalogusa uhai.

Watanzania tuache utani, tuheshimu na kufuata maelekezo ya viongozi na wataalamu wa afya ili tuwe salama sisi na nchi yetu.

MAPAMBANO ya ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) yanaendelea duniani ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi