loader
Wanaofika Tanzania wawekwa kwenye uangalizi

Wanaofika Tanzania wawekwa kwenye uangalizi

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeanza utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli, ambapo kuanzia jana abiria wote walioingia kutoka kwenye mataifa yaliyoathirika na Covid 19 wakiwemo Watanzania, waliwekwa kwenye uangalizi maalumu kwa siku 14.

Gazeti hili lilishuhudia kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, kukiwa kumewekwa tahadhari kubwa ya watu wanaofika kwenye uwanja huo, ikiwemo sharti la kila anayeingia kwenye Jengo la Tatu la Abiria kunawa mikono na kuvaa barakoa.

Aidha, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa mwongozo wa utekelezaji wa agizo hilo la Rais Magufuli, ikiwemo sharti la wageni wote wanaoingia nchini kutoka mataifa hayo yaliyoathirika, kujaza fomu maalumu juu ya afya zao na kuziwakilisha kwa mamlaka husika pindi wanapowasili.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara inayoshughulika na Magonjwa ya Milipuko katika JNIA, Dk George Ndaki alisema tayari timu uwanjani hapo, imeanza kutekeleza agizo hilo, kwa kuandaa hoteli zitakazohifadhi wageni hao katika kipindi cha uangalizi.

Dk Ndaki alisema pamoja na ndege nyingi, kupunguza safari zake za kuja nchini, bado baadhi ya wageni kutoka nchi hizo zenye maambukizi ya corona wanawasili, na hadi jana mchana waliwasili abiria 48 na kuwekwa karantini.

“Tumezitambua kwanza sisi kama timu nchi zilizoathirika zaidi na corona na watu wanaotokea huko tunawatenga na kuna baadhi ya hoteli tumezitenga kwa ajili ya kuwaweka chini uangalizi na kutakuwa na watalaamu wetu wakifuatilia maendeleo yao kwa siku zote hizo 14,” alisema Dk Ndaki.

Ummy alielezea mwongozo huo kwa abiria wote wanaowasili nchini, hasa wale wanaotoka kwenye mataifa yaliyoathirika na corona kuwa kuanzia jana watalazimika kuwekwa kwenye uangalizi kwa gharama zao.

“Pia abiria wote watatakiwa kujaza fomu ya mwenendo wa afya zao ndani ya ndege au usafiri wowote watakaoutumia na kuwasilisha kwa mamlaka za afya pindi tu wanapowasili nchini,” alisema Ummy katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa na wizara jana.

Pia alisema kwa mujibu wa mwongozo huo, baada ya siku 14 endapo kuna abiria waliokuwa chini uangalizi, kwa bila kuwa na dalili za Covid 19, watatakiwa kujisajili taarifa zao binafsi ili wapatikane kirahisi endapo watahitajika.

Aidha, alisema mwongozo huo pia umewataka Watanzania kuepuka safari katika nchi zilizoathirika na corona.

Aliihimiza watu kupiga simu ya dharura 199, endapo kutahitajika dharura ya kimatibabu. Hadi juzi, Tanzania ilikuwa na watu 12 waliothibitika kupata maambukizi ya Covid 19. Kati yao, wanne ni raia wa nje ya nchi na nane ni Watanzania.

Aidha, wote isipokuwa mmoja walitokea mataifa yaliyoathirika na corona. Utekelezaji wa hatua hizo, unatokana na agizo la Dk Magufuli alilolitoa juzi la kuwataka wasafiri wote watakaoingia nchini kutoka kwenye mataifa yaliyoathirika na corona wakiwemo Watanzania, kuwekwa karantini kwa siku 14, kwa gharama zao wenyewe.

Mbowe asitisha mikutano Naye Anastazia Anyimike kutoka Dodoma anaripoti kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametangaza kuwa amesitisha mikutano ya hadhara iliyokuwa ianze Aprili 4, mwaka huu kutokana na mlipuko wa corona. Pia amesema chama chake kipo tayari kushirikiana na serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Mbowe aliyasema hayo jana jijini Dodoma kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, wakati wa kuzungumzia ugonjwa wa corona na jinsi chama chake kilivyojipanga kukabiliana nao.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuepusha mikusanyiko mikubwa ndani ya chama. Alisisitiza kuwa hakutakuwa na mikutano ya hadhara hadi hapo hali ya nchi itakapotengamaa.

“Siku chache zilizopita baada ya kutoka gerezani na serikali kabla haijatoa taarifa ya kuingia ugonjwa huo hapa nchini, nilitoa maelekezo ya chama ya kuanza mikutano ya hadhara Aprili 4, mwaka huu, tukilenga kuzungumzia kuhusu kuwepo tume huru ya uchaguzi na chama kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu,” alisema Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro.

Aidha, Mbowe alisema chama chake kiko tayari kushirikiana na serikali katika kupambana na ugonjwa huo na kusisitiza kuwa hakuna siasa kwenye ugonjwa huo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/76291d9882ce6568840b675024530e62.JPG

UMOJA wa Vijana wa Chama ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi