loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwalimu Nyerere alivyobeba mafanikio

HISTORIA ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ina vipindi vingi vya kihistoria vinavyoanzia katika harakati za ukombozi wa nchi za Afrika.

Katika miaka ya 1950 na 1960, Waafrika wachache waliochoshwa na unyonyaji uliokuwa unafanywa na wakoloni karne na karne barani humo, waliamua kujiunga kwa kauli moja kutafuta uhuru wa kweli.

Tanzania kupitia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, inatajwa kama nchi kiongozi na Mwalimu anatajwa kuwa mwanamapinduzi halisi wa ukombozi wa Afrika na jasiri wa kupigania Afrika huru.

Mapambano ya ukombozi wa Afrika yalifanywa na viongozi kadhaa akiwamo Mwalimu Nyerere, Dk Kenneth Kaunda wa Zambia na Seretse Khama wa Botswana, ambao ndio waanzilishi wa Nchi za Mstari wa Mbele (Frontline States-FLS).

Baadaye waliongezeka Antonio Agostino Neto wa Angola na Samora Machel wa Msumbiji baada ya nchi hizo kupata uhuru mwaka 1975.

FLS ni muungano wa nchi tano huru kusini mwa Afrika ulioanzishwa kuhakikisha ukoloni na ubaguzi wa rangi unakoma barani Afrika.

Mwalimu Nyerere alikuwa Mwenyekiti wa FLS hadi alipostaafu mwaka 1985 na kumwachia Rais Dk Kaunda wa Zambia.

Baada ya harakati za FLS mwaka 1980, lilianzishwa Jukwaa la Kuratibu Harakati za Maendeleo Kusini mwa Afrika (The Southern African Development Co-ordination Conference-SADCC) na hili ndilo chimbuko la kuanzishwa kwa SADC mwaka 1992 yenye makao yake makuu jijini Bagorone, nchini Botswana.

SADCC (jukwaa) kilikuwa chombo cha nchi za mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi Afrika huku viongozi wa nchi zilizokuwa huru wakipigana kufa na kupona kwa vita vya chini kwa chini, kuyakomboa mataifa mengine.  

Tanzania kupitia Mwalimu Nyerere, inatajwa kuwa kinara wa harakati hizo. Nyerere alijitoa mwili na roho kuhakikisha Tanzania haiwi huru peke yake. Tanzania ikiitwa Tanganyika ilipata uhuru Desemba 9 mwaka 1961 kabla ya kuungana na Zanzibar mwaka 1964 na kuwa Tanzania.

Imani ya Mwalimu Nyerere iliongozwa na falsafa kwamba, Tanzania haiwezi kuwa huru kama nchi nyingine za Afrika haziko huru. 

Katibu Mkuu mstaafu, Uledi Mussa katika moja ya mafunzo kwa waandishi wa habari wanaoandika masuala ya SADC ikiwamo walioandaliwa mkoani Morogoro mwaka jana (2019) kuripoti Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika jijini Dar es Salaam, alisisitiza kuhusu hilo.

Uledi anasema nchi nyingi zilizounda kundi la FLS, kijiografia, kiuchumi na kijeshi zisingeweza kuhimili vishindo vya serikali za kibaguzi na mabavu bila ushiriki wa dhati wa Tanzania ambayo pamoja na mambo mengine, ilitoa hifadhi kwa wapigania uhuru wa nchi mbalimbali. 

Maeneo walikopata hifadhi ni pamoja na Nachingwea (Lindi), Kongwa (Dodoma), Mgagao-Kihesa, (Iringa), Mazimbu na Dakawa (Morogoro), Kaole- Bagamoyo (Pwani) na Dar es Salaam.

Nchi zilizoweka kambi nchini wakati wa harakati za ukombozi ni pamoja na Msumbiji, Angola, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe.

Mchango wa Mwalimu Nyerere kuhakikisha Afrika inakuwa huru na kuondoka katika ubaguzi na utegemezi, ulikuwa wa dhati na hata alipostaafu uongozi katika taifa la Tanzania, aliendelea kuwa mshauri mkubwa wa kuipata Afrika iliyo huru kiuchumi na umoja.

Katika hotuba zake mbalimbali, Mwalimu Nyerere amenukuliwa bila kusita, akidhihirisha kukerwa na taifa linalotegemea wahisani na wafadhili ili liendelee.

Nyerere ndiye kiongozi wakati wa uhai wake aliyezuia madini yasichimbwe nchini Tanzania mpaka Watanzania watakapopata ujuzi wa kuyachimba wenyewe.

Matamanio haya ya Baba wa Taifa yalilenga kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi badala ya kunufaisha wageni pekee.

Hilo ndilo alilolizungumza Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa mwaka jana katika mhadhara wa umma uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kujadili mafanikio, changamoto na fursa za jumuiya hiyo.

Mkapa pamoja na kuipongeza SADC kufanya vizuri katika amani na utulivu wa kikanda, akazihadharisha nchi wanachama kuacha utegemezi wa washirika wa maendeleo na kuwataka kuhakikisha rasilimali za Afrika zinamilikiwa na kuwanufaisha Waafrika.

“Naweza kuzungumza kwa kujivuna katika eneo la amani na uimara kwamba, ukanda umefanya vizuri sana. Pale inapojitokeza migogoro ya kitaifa, viongozi wa SADC kwa pamoja wamekuwa wakishauri na kuhimiza kurejea kwenye katiba na makubaliano ya kisiasa.”

“Tunaweza kusema bila wasiwasi kwamba, ushirikiano wa kikanda katika Afrika, SADC ndiyo iliyo imara na yenye amani.”

Katika mhadhara huo ambao Mkapa alikuwa mnenaji mkuu, alitembea katika nyayo za Mwalimu Nyerere za Afrika huru kiuchumi, jamii, siasa na usalama na kusisitiza kuwa ukombozi wa fikra utaongeza ujuzi na ubunifu wa kufanyia kazi changamoto za ajira kwa vijana na kuipeleka SADC kwa watu wa kawaida kutoka mwonekano wa chombo cha viongozi.

Kiongozi huyo aliyekuwa Mwenyekiti wa SADC mwaka 2003 akiwa Rais wa Tanzania, miaka 17 iliyopita na mtu aliyekuwa karibu na uongozi wa Nyerere kwa muda mrefu, anaamini kuwa Afrika inawahitaji wadau wa maendeleo katika kukuza uchumi, lakini haipaswi kuwa na utegemezi uliokithiri.

Hofu yake katika rasilimali ni kuona kile kilichopigwa vita na Mwalimu Nyerere, Dk Kaunda, Khama, Machel na Neto, bado kinaendelea kwa namna mbadala, lakini ikiwa ni ukoloni ule ule.

“Ndio maana nashauri kwamba, tuna rasilimali nyingi, iwe ardhi, madini… tunajiona kama zipo kwenye mamlaka yetu kwa kuwa zipo kwetu, lakini kwa uhalisia zipo mikononi mwa watu wengine ambao wanazitumia kwa matakwa na faida zao zaidi,” anasema Mkapa na kutaka umiliki huo urudi kwa Waafrika.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC aliyemaliza muda wake, Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Naibu Waziri Mkuu wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, akihutubia mhadhara huo wa UDSM, aliitaka SADC kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere na kusema alikuwa mpigania uhuru wa kweli wa Afrika.

Anasema katika miaka ya 1980 alikuja Tanzania kukiwakilisha chama cha Swapo (The South West Africa People’s Organisation) cha Namibia katika Afrika Mashariki, makao makuu yalikuwa Dar es Salaam.

Ndaitwah anasema amekaa kwa miaka sita nchini Tanzania na wakati wote Nyerere alimwita Mama Swapo kila walipokutana. “Hakika Nyerere ni mwanamapinduzi wa kweli wa Afrika.”

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akizungumza katika mkutano wa baraza hilo mwaka jana, alisema Tanzania inayo heshima kubwa kuona kuwa nchi za SADC zinatambua mchango wa Tanzania hasa wa Mwalimu Nyerere katika ukombozi.

“Tuliwahifadhi wapigania uhuru wengi kupitia vyama vya ukombozi kama Angola MPLA (The People’s Movement for the Liberation of Angola), ANC (The African National Congress) na PAC (Pan African Congress) vya Afrika Kusini.

"Frelimo (The Mozambique Liberation Front) cha Msumbiji, Zanu (The Zimbabwean African National Union) na Zimbabwean African People's Union (Zapu) vya Zimbabwe, Swapo cha Namibia na vyama vingine vingi,” alieleza Profesa Kabudi.

Anasema pia Tanzania iliwapokea wapigania uhuru na kufanikisha kuanzishwa kamati ya OAU (Umoja wa Nchi Huru za Afrika) na kauli hiyo iliungwa mkono pia na Katibu Mtendaji mstaafu wa SADC, Dk Simba Makoni.

Mafanikio ya uhuru kwa nchi za Afrika ni ishara tosha kuwa, alichokitamani Mwalimu Nyerere na wanamapinduzi wenzake, yamezaa matunda yanayopaswa kulindwa kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi