loader
Picha

Gari la matangazo linavyosaidia elimu ya mpiga kura

MWAKA huu, nchi yetu itaingia kwenye jambo moja muhimu la kujipatia viongozi wake watakaoiongoza nchi yetu kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Ni wa mantiki hiyo, elimu ya mpigakura ni moja ya nguzo muhimu ya kukuza uelewa wa wananchi wakati tunavyoelekea kwenye uchaguzi huo na nyingine zitakazokuja.

Wananchi wana wajibu wa kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kushiriki katika chaguzi na elimu hii inawasaidia kuhusu namna ya kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia Kifungu cha 4 (C) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 292 imepewa jukumu la kutoa elimu ya mpigakura nchi nzima na kuratibu na kusimamia watu au taasisi zinazotoa elimu hiyo.

Katika kutimiza jukumu hilo, NEC imeanza kutumia gari la matangazo katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura wa awamu ya kwanza uliohitimishwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hivi karibuni.

Gari hilo limepita karibu mikoa yote ya Tanzania Bara, kuelimisha, kuhabarisha, kuburudisha na kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura au kuboresha taarifa zao.

Ili kuwafikia wananchi gari hilo limepita katika miji ya mikoa hiyo kutangaza na kutoa elimu katika magulio, masoko, minada, stendi za mabasi ya mikoani na ya miji husika.

Kama hiyo haitoshi, gari hilo limeshiriki katika maonesho ya Nanenane na matamasha katika mikoa mbalimbali na kuweka kambi katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na kutoa elimu na burudani.

Gari hilo la matangazo pia lilitembelea shule za sekondari 17 katika mikoa mbalimbali na kuwaelimisha walimu na kuwahamasisha wanafunzi waliotimiza miaka 18 kujitokeza kwenda kujiandikisha.

Baadhi ya wananchi waliopata elimu kupitia gari hilo wamezungumza mambo mbalimbali kuhusu elimu inayotolewa na kutoa ushauri ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.

Baraka Matiko, mwanafunzi wa kidato cha sita, Shule ya Sekondari Galanos iliyopo jijini Tanga anatoa shukrani zake kwa watendaji wote wa tume, akisema amefurahi sana kupata elimu muhimu kuhusu mpigakura na kwamba sasa ameelewa kwamba ana haki na sifa za kwenda kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura na hatimaye kupiga kura.

“Ninapojiandikisha ninapata kadi ya mpigakura ambayo inanipa hadhi ya kupiga kura ili kumchagua kiongozi kwa ajili ya maendeleo ya taifa langu,” anasema Matiko.

Anasema amefurahi kupata elimu hii na anaiomba sana Tume ya Taifa ya Uchaguzi iendelee kutoa elimu hiyo kwa watu wengine ambao hawajaipata.

“Kubwa ambalo ningependa kuwaasa wale ambao huenda elimu hii wameipata lakini hawajaielewa umuhimu wake, waendelee kuitilia mkazo na hasa pale itakapofika wakati wa kupiga kura wafanye uamuzi sahihi kwa kutumia haki yao ya kumchagua kiongozi wanayemtaka,” anasema Matiko.

Ally Shabani Khailala, mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na mfanyabiashara wa bodaboda  anasema miaka ya nyuma kulikuwa hakuna huduma hiyo badala yake walikuwa wanasikia tu kwa watu wenye mawasiliano kama redio na televisheni ambao walikuwa wanapata nafasi ya kupata taarifa hizo.

“Wengine sisi ambao hatuna hata redio tulikuwa tunashitukizwa tu jamani kesho, lakini leo hii wiki mbili au wiki moja kabla tunapata faida ya elimu hii,” anasema Khailala.

Anasema kinachofurahisha zaidi ni kuona gari hilo linasimama sehemu ambazo kuna watu wengi wakiwemo ambao hawana redio wala televisheni na kutoa matangazo na elimu ya mpiga kura.

“Bahati mbaya sisi Watanzania wengi hatuna utamaduni wa kusoma magazeti na hata televisheni tunaangalia tu tamthilia wakati vipindi vya habari tunawaachia wengine,” anasema Khailala na kuongeza:-

“Kwa hiyo tunaipongeza sana Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuboresha utoaji elimu na taarifa na tunaishukuru kwamba imetambua Watanzania wanahitaji nini, ni hili gari kwa kweli limetukomboa, limetuelimisha na kutuhamasisha na kutuburudisha.”

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Macechu ya huko huko Tanga, Mwanaidi Mhina anapongeza Tume ikiwa na gari hilo la matangazo kufika shuleni kwake kuwaelimisha wanafunzi juu ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.

“Mimi naahidi sisi walimu kwa nafasi zetu tutaendelea kuwahamasisha wanafunzi wetu na nyumbani wanakotoka ili wajitokeze kujiandikisha na hatimaye kupiga kura ili tupate viongozi bora kwa manufaa ya taifa letu,” anasema Mwalimu Mhina.

Likiwa katika Manispaa ya Bukoba, gari hilo lilikutana na watu wenye ulemavu wawili na kuwapa habari njema juu ya kipaumbele kinachotolewa kwao wakati wote wa mchakato wa Uchaguzi.

Mmoja wa walemavu hao ambaye hakutaka kutaja jina lake alitoa ushuhuda juu ya kipaumbele kinachotolewa kwao wakati wa uchaguzi na kutoa shukrani zake kwa NEC kwa kuwathamini watu wenye ulemavu katika vituo vya kupigia kura.

Mpigadebe katika stendi ya Babati mkoani Manyara ambaye naye ni mwenye ulemavu wa miguu, Pascal Zacharia Salao, anasema itakuwa vizuri endapo elimu ya mpigakura itafika maeneo ya vijijini kwa sababu watu wenye ulemavu waliopo vijijini ni wengi na elimu hii ni muhimu kwao.

Anasema kwa kuwa watu wenye mahitaji maalumu wanapenda kupiga kura wanahitaji elimu hii ili kuwahamasisha kushiriki kwenye uchaguzi na amewakumbusha wananchi wasiwafiche watu wenye ulemavu kwani nao ni sehemu ya jamii.

UWEZO wa virusi vya corona kumshambulia mwanadamu katika mfumo wake ...

foto
Mwandishi: Hussein Makame

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi