loader
Magari kupuliza dawa Dar kudhibiti corona

Magari kupuliza dawa Dar kudhibiti corona

KATIKA kutekeleza agizo la Serikali la kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid -19), leo maeneo mbalimbali mkoani Dar es Salaam, yatapuliziwa dawa kwa kutumia magari.

Hiyo ni hatua ya kudhibiti ugonjwa huo usienee zaidi katika jiji hilo la biashara nchini.

Aidha, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), umeweka teknolojia ya kisasa ya kupima kiwango cha joto cha abiria kwa unyayo.

Pamoja na hatua hiyo, udhibiti wa ugonjwa wa corona katika mataifa mbalimbali, umepunguza zaidi ya asilimia 80 ya wageni waliokuwa akiingia nchini kwa shughuli mbalimbali ikiwemo biashara.

Taarifa za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaeleza kuwa mpaka sasa nchini watu 12 wamekutwa na virusi vya corona na wanane kati yao ni Watanzania.

Hayo yameelezwa jana kwa nyakati tofauti na watendaji wa JNIA na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati alipotembelea uwanja huo kuangalia namna maagizo ya Rais John Magufuli na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yanavyotekelezwa kudhibiti ugonjwa huo.

Kuhusu kupulizia dawa katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaaam, Makonda aliwataka wakazi wa mkoa huo, wasipate taharuki watakapoona magari yakipulizia dawa katika maeneo yao.

Alisema kazi hiyo inaanza leo katika maeneo kadhaa na lengo ni kufikia jiji zima ili kuondoa virusi, vimelea vya malaria na wadudu wengine. Akizungumza baada ya ziara yake, Makonda alisema,

“Nimeridhishwa na namna wenzetu wa JNIA mnavyotekeleza kwa vitendo maagizo ya serikali kupambana na corona. Wenyewe mmeona maeneo yaliotengwa kwa kila anayeingia kunawa mikono na kwenye kila milango kuna vitakasa mikono (sanitizers) na kuna chumba maalumu washukiwa hupelekwa kwa mahojiano kabla ya kupelekwa hospitalini.

“Lakini kubwa zaidi mmejionea jinsi walivyopiga hatua katika teknolojia ya upimaji wa joto kwa njia ya kuskani (scanner) unyayo kimya kimya bila hata mtu kujua, akiwa kwenye foleni akionekana ana joto lisilo sawa, anaondolewa na kupelekwa katika chumba maalumu kwa ajili ya kupelekwa hospitali au karantini,” amesema.

Akifafanua kuhusu teknolojia hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Afya wa JNIA, George Ndaki amesema teknolojia hiyo inampima mtu bila kujua baada ya abiria kukanyaga eneo lililochorwa nyayo, ambako mara moja mashine na kamera huakisi na kupima kiwango cha joto la mwili na mtu anayekuwa na kiwango kisicho cha kawaida (nyuzi joto kuanzia 38 kuendelea), hupelekwa chumba maalumu.

“Unajua hapa tunapima abiria wanaofika, pamoja na kwamba uwanja mzima kuna mashine za mkono za kupima joto za kawaida, lakini kuna hii teknolojia ya unyayo.

“Hii wengi hawaijui ndio maana wanasema hakuna vipimo JNIA lakini tukigundua una joto kali, sababu si kila joto ni corona, tunakuchukua na kukupeleka chumba maalum na kisha karantini siku 14,” alisema Ndaki.

Aliongeza, “Kwenye chumba hicho chenye uwezo wa kuchukua watu wanne mpaka watano, utafanyiwa mahojiano zaidi kabla ya kukupeka hospitali au karantini kwa mujibu wa hali ya mtu. Tunafanya haya kwa uangalifu mkubwa na kwa ushirikiano wa karibu sana na wataalamu wa afya wakiwamo wizara.”

Awali, Makonda alisema juhudi hizo zinazofanywa na JNIA zinastahili pongezi, ingawa kiwango cha wageni kuingia nchini kimepungua kwa asilimia zaidi ya 80 kutokana na nchi nyingi duniani kuweka zuio na mashirika ya ndege ya kimataifa kama Emirates, Qatar, KLM na Ethiopia Airline kupunguza safari huku nyingine zikisitisha kabisa.

“Abiria ni wachache sana wanaoingia, nadhani hata nyie mmejionea. Hakuna sababu ya kutangaza kufunga mipaka maana nchi zenyewe zimejiwekea zuio. Hivi karibu asilimia 95 ya ndege zote za kimataifa zitasitisha safari, ndio maana Rais Magufuli anasisitiza kama huna sababu maalumu ya kusafiri, usisafiri hata kama ni mkoa kwa mkoa,” amesema Makonda.

Makonda alisema kuna hoteli 10 zimetengwa jijini humo zenye hadhi ya nyota tano mpaka hosteli za gharama ya chini kwa ajili ya kupeleka abiria wote wanaotoka katika nchi zenye maambukizi. Hivyo, alisema malalamiko kwamba gharama za hoteli ni kubwa, hayana mantiki.

Alisema kama serikali ilivyosema wageni hao watalipia gharama wenyewe kwa siku 14.

Alisisitiza kuwa taarifa za abiria kupitia fomu wanazojaza wakiwa safarini kwa njia ya majini, mabasi na ndege, zimeendelea kuchukuliwa tangu mtu akiwa safarini mpaka anapofika nchini na kufuatiliwa akiwa nchini.

Katika kuonesha corona ni janga la dunia, Makonda alisema kuna ndege iliyokuwa na abiria 200 ilizuiwa kutua Comoro kutokea nchini, kutokana na Tanzania kuwa na waathirika wa corona.

Imebidi abiria hao wabaki Tanzania mpaka Comoro itakaporidhia waende. Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha alisema hali ya udhibiti inaendelea vizuri.

Kuhusu abiria hao 200, alisema wamerudi katika hoteli walizokuwa wamefikia awali mpaka Comoro itakapowaruhusu kwenda.

Alisema wengi ni wafanyabiashara. Makonda aliagiza wenyeviti wa serikali za mitaa, wamiliki na madereva wa vyombo vya usafiri vya abiria zikiwamo daladala, baa, klabu za usiku, kudhibiti msongamano na kutumia kinga zilizoelekezwa, ikiwamo kunawa mikono.

Alisema hatua hizo ni kwa faida yao na wasipotekeleza hawaikomoi serikali, bali wao wenyewe.

Kabla ya kwenda JNIA, Makonda alitembelea Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani na Nchi Jirani cha Ubungo, kujionea utekelezaji wa maagizo ya serikali na kukuta hali ni nzuri.

Alisema zaidi ya mabasi 10 hufanya safari nje ya nchi ikiwa Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/857a660913b2a495ae73777b1bc47059.jpeg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi