loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwendesha bodaboda auawa, pikipiki yaporwa

MKAZI wa Mtaa wa Stoo katika Kata ya Igunga Mjini wilayani Igunga mkoani Tabora, Maiko Abel (20), ambaye ni dereva wa pikipiki ya biashara (bodaboda), ameuawa kikatili na watu wasiojulikana kisha pikipiki yake kuporwa.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Igunga Mjini, Robert Mwagala alisema mauaji hayo yalifanyika Machi 23, mwaka huu baada ya kijana huyo kukodiwa na mtu mmoja saa tano usiku ampeleke kitongoji cha Makomero.

Alisema kijana huyo alikuwa na pikipiki yenye namba ya usajili MC 757 CAM aina ya pikipiki TVS Star, lakini hata hivyo, hakurudi nyumbani hadi juzi Machi 24 saa nne asubuhi ambako mwili wake ulipookotwa na wachungaji wa ng’ombe ukiwa kwenye palio la ng’ombe nje kidogo na Mji wa Igunga.

Mwagala alisema wachungaji hao wa ng’ombe walitoa taarifa polisi ambao walifika na kuuchukua mwili huo hadi Hospitali ya Wilaya ya Igunga ambako ulihifadhiwa.

Hata hivyo, Mwagala alisema ilipofika muda wa saa sita mchana bodaboda wenzake waliutambua mwili huo, huku akitoa wito kwa madereva wa bodaboda kuwa makini na watu wanaowakodi.

Aidha, amewataka madereva wote wa bodaboda kuacha tabia ya kukubali kukodiwa nyakati za usiku na watu wasiowajua huku akitangaza msako mkali wa kuwasaka wageni wote wanaoingia Kata ya Igunga Mjini.

Baba mdogo wa marehemu, Enock Samweli alisema mwanawe alitoweka Machi 23 jioni, na hakurudi nyumbani hadi Machi 24 alipopigiwa simu na Jeshi la Polisi kuwa mwanawe ameuawa na mwili wake upo hospitali ya wilaya.

“Mimi nilipigiwa simu nikiambiwa mtoto wangu amefariki na nilipofika hospitali ya wilaya nilimtambua mwanangu, lakini alikuwa ametobolewa macho yote huku kisogo chake kikiwa kimebonyea… kwa kweli inauma sana mtoto wangu ameuawa kikatili,” alisema Samweli.

Sanjari na hayo, alisema pikipiki aliyokuwa nayo wameipora wauaji hao. Alisema pikipiki hiyo haikuwa mali yake, bali alikuwa ameikodi kutoka kwa Furaha Athumani.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Merchades Magongo alithibitisha kupokea mwili wa dereva bodaboda Maiko Abeli Samweli (20) ukiwa umetobolewa macho yote.

foto
Mwandishi: Lucas Raphael, Tabora

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi