loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kilimo watakiwa kufanya kazi kwa bidii

MENEJIMENTI ya Wizara ya Kilimo imetakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi katika kutekeleza maagizo ya Rais Dk John Magufuli ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uhakika wa chakula.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya jana wakati wa hafla ya makabidhiano rasmi ya ofisi na aliyekuwa Katibu Mkuu, Mathew Mtigumwe yaliyofanyika makao makuu ya wizara Mtumba mkoani Dodoma.

Kusaya alisema Wizara ya Kilimo ina changamoto ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na uhakika wa chakula kwa kuzalisha mazao kwa wingi na kwa ubora.

“Kila mtumishi wa Wizara ya Kilimo ahakikishe anafanya kazi kwa bidii na weledi kutekeleza malengo yote tuliyowekewa na Rais John Magufuli kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika na usalama wa chakula,” alisema Kusaya.

Kwa upande wake, Mtigumwe alisema anawashukuru watumishi wote wa wizara ya kilimo kwa ushirikiano waliompa alipokuwa Katibu Mkuu na kwamba anajisikia vema kuona wizara na taasisi zake wanachapa kazi. Alitaja changamoto za sekta ya ushirika na umwagiliaji kuwa zinahitaji msukumo mkubwa ili taswira ya wizara ya kilimo iendelee kuwa nzuri.

“Ushirika bado ni changamoto, nawaachia japo tulianza mchakato wa maboresho ya sheria, endeleeni ili wakulima wa Tanzania wanufaike na jasho lao,” alisema Mtigumwe ambaye kwa sasa amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, Mkurugenzi wa Mipango Bora ya Ardhi ya Kilimo, Paulo Tarimo ameahidi kwa niaba ya Menejimenti na watumishi wa wizara ya kilimo kutoa ushirikiano zaidi kwa Katibu Mkuu Kusaya ili malengo ya taifa yafikiwe.

foto
Mwandishi: Mwandishi maalumu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi