loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ashauri masomo kwa njia ya mtandao

MMOJA wa walimu wanaofundisha masomo mbalimbali kwa njia ya mtandao, ameshauri shule kuwa na mfumo wa kufundisha wanafunzi kwa njia ya mtandao hasa katika kipindi hiki ambapo wako nyumbani ili kuwawezesha kuendelea kujifunza.

Akasema katika kipindi hiki cha tishio la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona, kitafanya wanafunzi kusahau masomo, lakini kukiwa na mfumo huo, kuwasaidia kumudu masomo yao vyema.

Pia mwalimu huyo, Shaaban Omary akasema kuna haja kwa serikali kuangalia namna ambavyo inaweza kuutumia mfumo huo katika shule zake, hatua ambayo mbali na kuwawezesha wanafunzi kuipata elimu hiyo kwa urahisi, itasaidia kupunguza mzigo mzito wa ufundishaji kwa walimu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Shaaban alisema uongozi wa shule ukianzisha programu hiyo kwa wanafunzi, siyo tu itawasaidia kujifunza wakati huu wa likizo ya dharura, bali pia kuwafanya waondokane na uzururaji usio wa lazima na kujiunga na makundi yasiyofaa mitaani.

“Hili ni suala kukubaliwa na wadau wengine wa elimu, ukweli ni kwamba matumizi ya mfumo huo wa utoaji wa elimu kwa mtandao kunawafanya wanafunzi kujiona kuwa bado wapo shuleni na walimu wao, pia kuwaepusha na kujisahau, kikubwa ni kwa wazazi kuendelea kuwapa ushirikiano,” alisema.

Pia akizungumzia mfumo huo unavyofanya kazi, mwalimu huyo anayefundisha shule mbalimbali za jijini Dar es Salaam, alisema ili elimu hiyo itolewe inampasa mwanafunzi kuwa na simu janja ikayomuwezesha kuungwa katika kikundi kimoja kitakachokuwa chini ya usimamizi wa mwalimu wa somo husika.

Alisema kupitia mfumo huo, mwalimu huandaa somo lake na kuliwakilisha katika kundi hilo huku wanafunzi wakimfuatilia lakini pia kupata fursa ya kuuliza maswali na kujibiwa kwa namna ambavyo inastahili.

“Wakati mwingine mwalimu na mwanafunzi huweza kufanya mawasiliano ya moja kwa moja kupitia simu, hapa humwezesha kupata uelewa wa kutosha pale mwanafunzi anapohitaji msaada wa ziada hasa kwa somo ambalo hajaliewa,” alisisitiza Shaaban.

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi