loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Madawati 4,545 kusambazwa shuleni

KAMATI ya kitaifa ya madawati Zanzibar kwa shule za msingi na sekondari itasambaza madawati 4,545 shule za Unguja na Pemba.

Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya madawati shule za Unguja na Pemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari hapa jana. Haroun alikagua pia madawati yaliyowasili yakiwa hatua za matayarisho ya kuunganishwa.

Alisema kamati hiyo imeundwa kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri. Alisema juhudi kubwa zimefanywa kulipatia ufumbuzi tatizo la uhaba wa madawati nchini na kukusanya michango kupitia njia za harambee kwa wahisani na wafanyabiashara kuchangia. ‘’Tatizo la uhaba wa madawati hivi karibuni tutalipatia ufumbuzi.

Tayari tuna madawati 4,545 viti na meza ambazo tutasambaza kwa shule za Unguja na Pemba,’’ alisema Haroun. Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khalid Masoud alisema makontena tisa tayari yamewasili nchini huku wakisubiri makontena mengine 13 zaidi.

Alisema wanafunzi 13,615 watafaidika na madawati hayo ambayo mahitaji yake makubwa yapo upande wa shule za chekechea na msingi.

‘’Matarajio yetu makubwa madawati haya yatasaidia katika kukabiliana na uhaba uliopo ambao zaidi ni upande wa shule za maandalizi pamoja na msingi Unguja na Pemba,’’ alisema.

Mapema Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohamed Said alisema tatizo la uhaba wa madawati ni kubwa na juhudi za makusudi zinahitajika kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema kuongezeka kwa shule za msingi na sekondari kumeibua tatizo la uhaba wa madawati ikiwemo viti na meza.

‘’Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imefurahishwa na juhudi za kamati kukabiliana na uhaba wa madawati. Tunaziona,’’ alisema

. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliunda kamati ya kitaifa kukabiliana na uhaba wa madawati shule za Unguja na Pemba baada ya kubainika wanafunzi wengi wa shule za maandalizi na msingi wanasoma sakafuni.

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi