loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mbinu zinazoipaisha Bagamoyo ufaulu shule za sekondari

ELIMU na viwanda ni sekta mbili tofauti lakini zinategemeana. Utegemezi wa sekta hizi upo katika eneo la rasilimali watu. Viwanda bila watu wenye elimu, ujuzi na maarifa hakuna uzalishaji.

Viwanda vinajengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hasa mkoa wa Pwani ambao kijiografia upo katika eneo la kimkakati. Bagamoyo, ni kati ya halmashauri tisa zilizopo ndani ya wilaya saba za Mkoa wa Pwani, inayotekeleza sera ya viwanda kwa kuvutia wawekezaji kuwekeza ndani ya halmashauri hiyo.

Swali linakuja, je, wenyeji katika maeneo ambayo viwanda vinajengwa kwa kasi namna hii wataweza kutumia fursa hii kupata ajira, kufanya biashara na kuendeleza shughuli za kijasiriamali kwa ujumla wake? Jibu la swali hili si tu linawagusa wananchi bali hata mwekezaji kwani atakuwa na uhakika wa nguvu kazi na huduma nyingine muhimu.

Kwa kulitambua hili, uongozi wa halmashauri hiyo kongwe umejiwekea mikakati madhubuti ya kuhakikisha hakuna mtoto hata mmoja wa Bagamoyo aliye na sifa za kujiunga na masomo ya sekondari anayeachwa nyuma au kukatizwa masomo yake ili ashiriki mila za jando na unyago. Katika kuhakikisha ndoto ya uchumi wa viwanda na ustawi wa taifa inakuwa kweli, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imeanzisha programu ya ‘Tusome Pamoja’ ambayo matokeo yake yamezidi kuonekana mwaka hadi mwaka.

Mkakati huu pamoja na ushirikishwaji wa shule binafsi na zile za umma, ufuatiliaji wa utendaji kazi wa walimu na mafunzo ya mara kwa mara kwa wakuu wa shule na taaluma na ufuatiliaji wa utoro kwa wanafunzi umeifanya wilaya hii kufanya vema kwa miaka ya hivi karibuni.

Takwimu rasmi za Halmashauri ya Bagamoyo zinaonesha kuna jumla ya shule za sekondari 22 zikiwemo za serikali 10 na za watu binafsi/ taasisi 12 ambazo zina jumla ya wanafunzi 10,716.

Kati ya idadi hiyo, waliopo katika shule za serikali ni 5,006, ambapo wavulana ni 2,483 na Wasichana 2,523. Wanafunzi hawa wanafundishwa na walimu 463 katika shule za serikali; walimu wa sayansi wakiwa 78 na wale wa masomo ya sanaa wakiwa 385.

Ufaulu Kwa miaka mitatu mfululizo, kuanzia 2017 – 2019, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imeshika nafasi ya kwanza kimkoa na kitaifa katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne na mtihani wa upimaji wa kidato cha pili. Kupitia umbo la pembenne linaloundwa na uongozi, walimu, wanafunzi na wazazi, halmashauri hii imefanikiwa kupata matokeo chanya kwani kiwango cha ufaulu wa wanafunzi ngazi ya sekondari umeendelea kupanda ambapo hadi kufikia mwaka jana ulifikia asilimia 84.

Uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia, ikiwemo ujenzi wa maabara, sera ya elimu bure na ongezeko la idadi ya shule za sekondari kwa pamoja zinatajwa kuwa ni miongoni mwa sababu zilizochangia ufanisi wa Halmashauri ya Bagamoyo katika sekta ya elimu. Takwimu rasmi zinaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ina jumla ya kata 11 na hadi sasa, imefanikiwa kujenga shule za sekondari za kata katika kata tisa. Kati ya idadi hiyo, shule tatu zimejengwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano.

“Kuanzishwa kwa shule hizo pia kumesaidia kuwapunguzia wazazi gharama, kwani awali walikuwa wakitumia fedha nyingi kwenda kusomesha watoto nje ya nchi,” anasema Violeth Mlowosa, Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Mkuu huyu anaeleza mbinu nyingine zinazotumika katika eneo lake la kazi kuwa ni upimaji ya kidato cha pili na mitihani ya taifa ya kidato cha nne na sita.

“Mwaka 2018 na 2019,halmashauri ilifanya makongamano makubwa la kujadili na kufanya tathmini ya mitihani ya upimaji kidato cha pili na mitihani ya Taifa ya kidato cha nne na sita. Washiriki katika makongamano haya walikuwa ni wadau wote wa elimu katika halmashauri, wamiliki wa shule binafsi za sekondari, walimu wote wakuu wa sekondari za serikali na binafsi, viongozi wa serikali katika wilaya, wazazi, viongozi wa dini na mashirika binafsi yanayojishughulisha na masuala ya elimu,” anaeleza.

Akieleza madhumuni ya tathmini, Mlowosa anasema yalilenga kuongeza ufaulu na kuendelea kushikilia nafasi ya kwanza mwaka 2019, malengo hayo yamekamilika mwaka 2019 kwani Bagamoyo ilibaki kileleni. Jedwali likionesha nafasi ya ufaulu wa Halmashauri Kimkoa na Kitaifa kwa miaka minne iliyopita.

Motisha kwa walimu, wanafunzi Nadharia ya mwanasaikolojia Abraham Maslow ya namna ya kumpa mfanyakazi motisha inatumika katika halmashauri hii kwa lengo la kuifanya Bagamoyo kuendelea kushikilia nafasi ya kwanza ndani ya mkoa na kufanya vema ngazi ya kitaifa pia.

Wakati Maslow akiamini kupitia nadharia yake ya ‘Maslow’s Hierachy of Needs’ kuwa motisha huchochea ufanisi kazini, halmashauri hutekeleza hili kwa vitendo kwani huwatambua na kuwapa mkono wa pongezi walimu na hata wanafunzi waliofanya vema kidato cha nne na sita katika kongamano la elimu la wilaya kwa lengo la kuibua ari ya kufundisha (walimu) na (wanafunzi) kujisomea.

Mbali na hatua hiyo, Mlowosa anasema Halmashauri hiyo imeanzisha mpango maalumu uitwao “TUSOME PAMOJA” wenye lengo la “kuwainua wanafunzi wenye uelewa mdogo darasani kupandisha ufaulu wao.”

Akieleza namna mpango huu unavyotekelezwa, anasema kinachofanyika ni walimu kuwatambua wanafunzi wao ambao wanapata shida ya “kuelewa kwa haraka” kisha kuwatenga kwa kuanzishia ‘masomo maalumu’ ya jioni. “Mwalimu hukaa na mwanafunzi mmoja mmoja na kusikiliza shida ya mwanafunzi inayofanya ashindwe kuelewa kwa haraka kisha kumsaidia mwanafunzi huyo,” anaeleza.

Udhibiti wa utoro Ikiwa shule zina walimu wa kutosha, madarasa na miundombinu ya kisasa ya kujifunzia wakati mahudhurio ya wanafunzi ni duni, ndoto kuondoa ujinga na kuupiga vita umasikini katika jamii kamwe haitatimia. Licha ya ukweli kwamba sera ya elimu bure imechangia kupunguza utoro shuleni, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imekwenda mbali zaidi na kuchukua hatua ili kudhibiti tabia hiyo inayochangiwa na mila na desturi.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Kawawa amelivalia njuga suala la utoro katika shule za sekondari kwa kuanzisha utaratibu unaomwajibisha hata mzazi ikiwa mtoto ana tabia ya utoro. Katika kila shule, mwalimu mmoja ameteuliwa kwa kazi moja tu; kuhakikisha wanafunzi wanaacha utoro kwa kuwafuatilia kila siku kuona nani yupo na nani hajafika shule na kufuatilia sababu za ambao hawafiki shule, kuzitafutia changamoto zao ufumbuzi na hili kwa hakika linaonesha mwitikio chanya kwa kiasi kikubwa.

“Ni jambo la faraja kubwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne na kwenye mitihani ya upimaji ya kidato cha pili kwa miaka mitatu mfululizo sasa, na hili ni baada ya juhudi kubwa tulizofanya kama wilaya,” Zainabu Kawawa anaeleza.

Anasema wilaya hiyo imejiwekea utaratibu wa kupambana kwa njia ya kuwekeana mikataba na wazazi wa wanafunzi ambao wazazi wamekataa kuwapeleka kidato cha kwanza ilhali wamefaulu kuendelea na elimu ya sekondari.

Mbali na hilo, mkuu huyo wa wilaya anaongeza kuwa, amejiwekea utaratibu wa kukutana na wazazi wa wanafunzi walioko katika kundi la ‘watoro waliokithiri’.

“Hawa pia huwa naingia nao mikataba maalumu ya wao kuhakikisha watoto wao hawatakosa kwenda shule bila sababu za msingi kama ugonjwa.”

Akieleza mafanikio ya mkakati huo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo anasema: “imetusaidia pia kupunguza wingi wa wanafunzi wanaopata daraja sifuri na kuongeza wanaopata daraja la I. Mfano; Mwaka 2017 kati ya wanafunzi 1,662 wa kidato cha nne waliofanya mtihani wa Taifa, Wanafunzi 1,371 waliofaulu kwa daraja la I – IV na waliopata daraja sifuri walikuwa 470 sawa na asilimia 18% ya wanafunzi wote.

“WATU wengine wakiona mwanamke mwenye ulemavu ana mimba, wanashangaa na ...

foto
Mwandishi: Mbinu zinazoipaisha Bagamoyo ufaulu shule za sekondari

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi