loader
Dstv Habarileo Mobile
Picha

Zijue faida, umuhimu wa mtama

MTAMA ni zao linalolimwa katika nyanda kame, hususani Kanda ya Kati inayohusisha mikoa kadhaa ikiwamo ya Dodoma na Singida. Hii ni kutokana na hali halisi ya kimazingira ya mikoa hiyo.

Zao hili lenye virutubisho vingi vinavyohitajika katika mwili wa mtumiaji kuimarisha afya, limekuwa likiwasaidia watu wa nyanda kame kuwa na usalama wa chakula, lakini pia kupata faida kwa kuuza zao hili.

Kwa mujibu wa mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti Makutupora, Sada Shosy, mtama ni zao lenye wingi wa vitamini, wanga, madini joto, zinki, potasiamu na magneziamu. Madini kama ‘copper’, ‘iron’ (madini joto), zinki, magneziamu, na kalsiamu yanapatikana kwenye mtama. Copper husaidia uingizwaji wa iron (madini joto) kwenye mwili.

Anasema kikubwa zaidi kilichopo katika mtama na kinaufanya kuwa tofauti na mazao mengine, ni nyuzinyuzi maarufu zilizopo kwa wingi na zinazozuia sukari anayokula mtumiaji kutoingia kwa wingi kwenye mfumo wa damu.

“Ganda la nje la punje za mtama lina viondosha sumu, anthrocyanins, ambavyo havipatikani kwenye vyakula vya aina nyingine. Viondosha sumu hivi vina uwezo wa kupunguza aina kadhaa za saratani, ikiwemo ya koo, ukilinganisha na watu wanaokula mahindi na ngano mara kwa mara,” anasema Shosy.

Mtafiti huyo anasema viondosha sumu ni kampaundi zenye faida zinazozima na kuondoa kabisa sumu huru (free radicals) katika mwili. Anasema: “Hizi ni sumu ambazo mara nyingi husababisha seli zenye afya kwenye mwili kubadilika na kuwa seli za saratani.”

Taarifa zinasema mtama una nyuzinyuzi ambazo ni muhimu kwa watumiaji wa hasa wagonjwa wa kisukari kwa kuwa nyuzi nyuzi hizo zinapunguza sukari katika mfumo wa damu na hivyo, kumsaidia mgonjwa wa kisukari kupunguza sukari kwenye damu.

“Pamoja na kupunguza kiwango cha sukari katika mfumo wa damu, pia unamsaidia mgonjwa katika umeng’enyaji wa chakula mwilini na kupunguza tatizo la kukosa choo au kupata choo kigumu na kidogo,” anasema.

Anawashauri watumiaji hasa wagonjwa wa kisukari kuepuka kukoboa mtama kwani kufanya hivyo ni kuondoa nyuzi nyuzi hizo muhimu zinazopatikana kwenye ganda la mtama.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vikiwamo vya kimtandao, mgonjwa wa kisukari anapotumia mtama, hupata faida kwa kuwa hupunguza kiwango cha sukari kwenye damu. “Mtama una Phenolic Compound (tannin) inayosaidia kufanya porotini iliyopo kwenye chakula isitumike kwa urahisi,” kinasema chanzo kimoja. Kinaongeza: “Kama tunavyojua, tunapokula chakula kinachoanza kusagwa huwa ni wanga kupelekwa kwenye glukosi na kama wanga utakuwa umeisha inaanza kusagwa protini na kupelekwa kwenye glukosi.”

Shosy anasema: “Nafaka huwa na kiwango kikubwa cha wanga. Kwa kawaida, wanga huvunjwavunjwa na kuwa sukari nyepesi hivyo kuongeza kiwango cha sukari kwenye mwili hali inayoweza kumfanya mtu apate kisukari au kusababisha mtafaruku kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari.”

“Lakini kwenye mtama kuna ganda la nje lenye utajiri wa ‘tannin’ ambayo ina uwezo wa kuzuia kusaidia kupunguza kuingiza kiwango cha sukari kwenye mfumo wa damu na hivyo basi, wenye ugonjwa wa kisukari hawatapata shida za hapa na pale katika kiwango cha sukari…”

Hata hivyo anasema Phenolic Compound (tannin) inaifanya protini isipelekwe kwenye glukosi na hivyo kumsaidia mgonjwa wa kisukari kwani sukari yake ya kwenye damu itakuwa imepungua kutokana kwa kuwa hakutakuwa na sukari inayopelekwa kwenye damu.

Inaelezwa kuwa, mtama ni moja ya nafaka zenye nyuzi nyuzi kwa wingi (dietary fiber) zinazosaidia mfumo wa umeng’enyaji wa chakula yaani chakula kupita bila shida, kuzuia kufungamana njiani, kutopata choo, maumivu ya tumbo na gesi kuzidi. Aidha, kiasi cha fiber kinachozidi kwenye mwili husaidia kukwangua na kuondoa lehemu (cholesterol) hatari (LDL) inayoboresha afya ya moyo na kuulinda mwili.

“Siyo kwamba mgonjwa wa kisukari pekee ndio anatakiwa kutumia mtama lakini pia hata ambae hana kisukari anapaswa kutumia mtama ili kuilinda afya yake kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba,” anasema na kuongeza: “Kazi ya mtama ni kuzuia sukari iwe katika kiwango cha kawaida kwa maana ya kutopandisha wala kushusha sukari kwenye mfumo wa damu.”

Imebainika kuwa, ingawa ganda la mtama ndilo husaidia kurekebisha kiwango cha sukari mwilini, bado watu wengi wana kasumba ya kutopenda kula mtama usiokobolewa. Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa iliyobahatika kupata mbegu bora na za uhakika za mtama kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari).

Mbegu ni za uhakika na zinahimili nyanda kame, magonjwa pamoja na wadudu. Anawashauri wakulima kutumia mbegu bora zinazotolewa na taasisi hiyo na kwamba mbegu hizo huzaa na hivyo, kuwasaidia kuongeza kupata pesa sambamba na faida za kiafya. Uchunguzi umebaini kuwa, mbegu hizo zinazopatikana katika Kituo cha Makutupora zikiwa zimeboreshwa ni pamoja na ‘tegemea’, ‘hakika’, ‘wahi’ na ‘masia’.

Kwa mujibu wa Shosy, ugonjwa wa ‘celiac’ ni mzio unaotokea wakati vyakula vyenye asili ya kuvutika kama ngano vinapoliwa. Kinga ya mwili hujaribu kupambana pindi ‘gluten’ inapoliwa na kusababisha kuharibika kwa utumbo mdogo. Gluten ambayo inapatikana kwenye maelfu ya vyakula vya kawaida, na kufanya hali kuwa ngumu mno kwa wale wenye ugonjwa wa celiac.

Nafaka mbadala kama mtama, zinaweza kuliwa kwa usalama na wale wanaosumbuliwa na tatizo hilo. Hii inamaanisha uwezekano wa kupunguza kasi ya ugonjwa wa anaemia, kukiwa na madini ya kutosha ya copper na iron kwenye mfumo, chembe hai nyekundu za damu huongezeka, hali hiyo huongeza mzunguko wa damu, kuongeza ukuaji wa seli na kurekebisha seli zilizoharibika.

Vyanzo mbalimbali vinabainisha kuwa mtama una kiwango kikubwa cha madini aina ya magnesiamu yanayoongeza uingizwaji wa madini ya kalsiamu katika mwili. Madini haya magnesiamu na kalsiamu ni muhimu kwa maendeleo ya tishu za mifupa na kuharakisha kupona kwa mfupa ulioharibika au mifupa iliyozeeka.

“Tuzingatie kuwa, bidhaa bora za mtama hutokana na mtama uliotunzwa vizuri shambani, kuvunwa kwa wakati, kukaushwa, kusafishwa vizuri na kuhifadhiwa vema,” anasema na kuongeza kuwa, maandalizi yanayotakiwa kufanywa kabla ya kupika ni pamoja na kupepeta na kupembua, kuosha na kusaga kama unataka kupata bidhaa ya unga.

Hata hivyo, mtafiti huyo anasema mtama kama nafaka nyingine, una matumizi mbalimbali ukiwa ni pamoja na kutengeneza uji, kupikia ugali, kande, wali, keki, mkate, bisi na pombe. Aidha uchunguzi umebaini kuwa, mtama ni chakula kizuri cha mifugo kama kuku, ng’ombe au nguruwe.

foto
Mwandishi: Agnes Haule

2 Comments

 • avatar
  Aveline
  18/09/2020

  Asante kwa elimu

 • avatar
  Aveline
  18/09/2020

  Asante kwa elimu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi