loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanariadha waijia juu RT

WANARIADHA maarufu mkoani Arusha wamesema viongozi wanaongoza Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) ni batili na wamevunja Katiba ya shirikisho hilo.

Kufuatia hali hiyo wanariadha hao wameliomba Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuvunja uongozi huo na kuunda kamati ya muda ikiwashirikisha wanariadha, lengo ni kutaka ushirikishwaji wa pamoja kwa maslahi ya mchezo huo.

Akizungumza na gazeti hili jijini Arusha, mwanariadhaa mkongwe, Shenya Imori amesema kwa mujibu wa Katiba ya RT, kiongozi wa juu wa wa RT anapojiuzulu, wanapaswa kuitisha Mkutano Mkuu ndani ya siku 90, lakini hilo halikufanyika hadi sasa toka Wilhelm Gidabuday alipojiuzulu Novemba mosi mwaka jana.

“Hivi karibuni aliyekuwa Katibu Mkuu wa RT, Gidabuday alibwaga manyanga na kwa mujibu wa katiba ya shirikisho, ndani ya siku 90 walitakiwa achaguliwe katibu mwingine kushika nafasi hiyo,” alisema Imori.

Imori amesema katika kikao cha Novemba mosi mwaka jana kati ya uongozi wa juu wa RT ukiongozwa na Rais Anthony Mtaka, BMT na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, shirikisho liliahidi kufanya mkutano Desemba mwaka jana, lakini hadi leo hakuna kilichofanyika.

BMT hivi karibuni iliunda kamati ya muda kufanya marekebisho ya Katiba ya shirikisho hilo, kitu ambacho ni kama kiini macho, kwani kamati hiyo inapaswa kushirikisha wanariadha, ambao ndio wavuja jasho.

Mwanariadhaa huyo pia alisema kuwa RT hadi sasa haina Tin namba (Tax Identification Number) kwa mujibu wa sheria za nchini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwa kufanya hivyo ni kama wanaficha kitu fulani ndani ya shirikisho.

Mwanariadhaa mwingine aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini alisema RT inadaiwa mamilioni ya fedha na wanariadhaa, lakini wakitaka kudai fedha hizo hutishiwa kuchongewa kazini kwano ili wafukuzwe kazi.

Mwanariadhaa huyo alisema kuwa ni miaka minne imepita haijawahi kufanya mashindano ya taifa na kuibua wanariadhaa wapya na wanariadha wanashindwa kujua tatizo ni nini mashindano hayo kushindwa kufanyika na kumtaka msajili wa vyama vya michezo nchini na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenda RT kufanya mahesabu na wahusika kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

‘’RT ina misaada mingi ya fedha kutoka nje ya nchi, mawakala wa wachezaji hulipa fedha nyingi lakini fedha hizo hazinufaishi walengwa, ambao ndio wavuja jasho, “alisema mwanariadha huyo.

Mwanariadha mwingine naye aliomba kutotajwa jina alisema RT ina fedha nyingi lakini haifuatiliwi kama mashirikisho mengine yanavyofuatiliwa kama Shirikisho la Soka Tanzania (RT) pamoja na mengine.

Akizungumzia tuhuma hizo, Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Ombeni Zavalla alisema jana kwa njia ya simu kuwa madai ya wanariadhaa hao kwa uongozi wote wa shirikisho hilo kuwa hauko kikatiba ni ya uongo, kwani wao wako kwa mujibu wa katiba na sio vinginevyo. Zavalla alisema kuwa madai hayo yanapaswa kupuuzwa, kwani RT inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi Desemba mwaka huu na wanaotaka kugombea wajiandae kuchukuwa fomu pindi muda utakapofika.

Kuhusu marekebisho ya katiba, alisema kamati iliyoundwa wajumbe wake wamechaguliwa kwa kufuata vigezo na sio lazima kushirikisha Kamisheni ya Riadha pamoja na kuingia katika Kamati ya Utendaji ya RT.

Katibu huyo alizungumzia madai ya wanariadha wanaodai mamilioni ya fedha sio ya kweli, kwani ofisi yake haina kumbukumbu yoyote inayoonesha kuwepo kwa madai hayo na kama wana udhibitisho mlango uko wazi kuwasilisha.

Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha alipoulizwa juu ya madai ya uongozi wote wa RT ni batili alisema kuwa jukumu alilopewa na Waziri ni marekebisho ya Katiba na madai ya hao wanariadha hao, hayako mezani kwake kwa sasa.

Msitha alisema kama wanariadha wana malalamiko wanapaswa kufuata taratibu kwa mujibu wa katiba yao na kwenda kwenye vyombo vya habari kulalamika haoni kama huko ni mahali sahihi kwao.

‘’Nimepewa kazi ya kurekebisha Katiba ya RT na kuwa na wajumbe wenye mamlaka kisheria kufanya kazi hiyo na sio vinginevyo,’’alisema Msitha.

WACHEZAJI na viongozi wa Simba SC wamewasili jijini Dar es ...

foto
Mwandishi: John Mhala, Arusha

1 Comments

  • avatar
    witxcrafpr
    02/05/2020

    Muchas gracias. ?Como puedo iniciar sesion?

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi