loader
Picha

Wananchi Dodoma wajikinga wasipate corona

JIJI la Dodoma ambalo limekuwa na pilikapilika nyingi tangu serikali ilipohamishia makao yake makuu, wakazi wake wengi wameitikia mwito wa serikali wa kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga kupata virusi vya corona.

Ukiacha serikali kuhamishia makao yake makuu na karibu wizara zote kuhamia, pia taasisi mbalimbali za umma na binafsi, wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali wamehamia jijini hapa, hivyo kuongezeka kwa pilipika nyingi za watu kutokana na kuwapo shughuli mbalimbali.

Aidha, jiji hili kwa kawaida limekuwa likipata wageni wengi kipindi cha Kamati za Bunge na Bunge lenyewe linapofanya vikao vyake, lakini sasa hali ni tofauti.

Japokuwa hakuna mtu yeyote aliyepatikana kuwa na virusi vya corona jijini hapa, lakini wananchi wengi wameonesha mwamko mkubwa wa kujilinda wasipate maambukizi hayo.

Tangu mgonjwa wa kwanza wa corona apatikane nchini na serikali kutangaza hatua kadhaa za kudhibiti visisambae, ikiwamo kuwataka wananchi kuchukua tahadhari, staili ya maisha katika jiji hili imebadilika.

Pilikapika zimepungua kutokana na watu wengi kujizuia kutembea au kwenda kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi, kama ilivyokuwa hapo awali.

Katika kujikinga na virusi vya corona, karibu maeneo yote yenye kutoa huduma mbalimbali yawe ya umma au binafsi, yamewekwa vitakasa mikono na sabuni, kama vile kwenye mahoteli, mabenki, mihagawa, maofisi, hospitali na mengineyo.

Wananchi wengi wanaokwenda katika maeneo hayo kuanzia watoto hadi watu wazima, wamekuwa wakifuata maelekezo ya kutumia vifaa hivyo wanapoingia na kutoka.

Aidha, idadi ya watu wanaotembelea maeneo yaliyozoeleka kuwa na mikusanyiko ya watu, kama vile kwenye masoko, baa, eneo maarufu la Nyerere Square na Mnadani, ambako watu hufuata nyama choma siku za mwisho wa wiki, imepungua kutokana na wengi kujizuia kufanya matembezi yasiyo na umuhimu.

HabariLEO limetembelea maeneo ya jiji la Dodoma na kuzungumza na baadhi ya wananchi, ambao wengi wameeleza jinsi walivyochukua tahadhari ya kujikinga, wasipate virusi vya corona, hali ambayo imebadili mazoea ya maisha yao ya kila siku.

Mkazi wa eneo la Kigamboni, Dodoma anayejishughulisha na kuuza vitabu vikiwemo vya dini katika barabara ya Nyerere, Magreth Makinda, amesema idadi ya wateja aliokuwa akiwapata hapo awali kabla ya corona, imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na watu wengi kupunguza safari za mitaani kujinusuru na virusi hivyo.

“Nilikuwa nikipata wateja mbalimbali wakiwamo wafanyakazi wa serikali, wanafunzi wa vyuo na waumini wa dini, lakini tangu corona kutangazwa kuingia nchini, wateja hakuna, naweza kukaa siku nzima bila kuuza kitu na hivi vyuo vimefungwa ndiyo hali imezidi kuwa ngumu,” alisema.

Mwananchi mwingine, Robert Jarome, anayeendesha bodaboda mkazi wa Mailimbili, amesema hali imekuwa ngumu kutokana na watu kupunguza safari zisizo za lazima, kama vile kwenda sehemu za starehe baada ya kazi, hivyo wanakosa abiria.

“Tangu corona ilipotangazwa kuingia nchini, maisha yamebadilika ghafla tofauti na tulivyozoea. Kila sehemu unayoenda unatakiwa kunawa mikono, lakini kwetu (waendesha bodaboda) tupo kwenye hatari kwani hatuna maeneo ya kuoshea mikono wala vifaa vya kujikinga na virusi vya corona.”

Meneja wa hoteli ya Mwambao ambayo wageni wengi hupendelea kula wakiwamo wafanyakazi wa serikali, Peter Hotay, alisema wamechukua tahadhari, kwa kuweka vitakasa mikoni kwa ajili ya wateja wanaoingia hotelini hapo na kwamba wengi wamekuwa wakivitumia wakati wa kuingia na kutoka.

Mwananchi mwingine mkazi wa Kisasa, Juma Khalfani, amesema virusi vya corona vimebadili mienendo na tabia za watu wengi hasa katika suala la kuzingatia usafi, kusalimiana na matembezi.

Msimamizi wa usalama katika eneo maarufu la viwanja vya Nyerere, ambalo hutembelewa na watu wengi, Joseph Kigomba, amesema idadi ya watu wanaotembelea eneo hilo imepungua kidogo, ikilinganishwa na hapo awali kabla ya virusi vya corona kutangazwa kuingia nchini.

KIWANGO cha mimba za utotoni kimeripotiwa kupungua kwa kasi katika ...

foto
Mwandishi: Abdallah Bawazir, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi