loader
Picha

Shibuda- JPM mulika watendaji, baadhi wanakuchafua

MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda amemwomba Rais John Magufuli kumulika baadhi ya watendaji wake hususan wenye mamlaka na masuala ya siasa kwa madai wamekuwa kikwazo na kusababisha masuala ya kujadiliana ndani ya nchi kwenda kuzungumzwa nje ya nchi.

Shibuda alisema sehemu ya siha kwa wadau kuzungumzia masuala ya siasa nchini ni kupitia vikao vya ndani ya baraza hilo na kwenye mafunzo lakini hayo hayafanywi na hakuna sababu zinazotolewa.

Alisema mara ya mwisho walikutana mwaka jana kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baada ya hapo, vikao vya kamati ya uongozi vilifuatia lakini hadi jana hakuna kikao kingine cha baraza hilo.

Hata hivyo, akizungumzia hoja ya Shibuda, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji mstaafu Francis Mutungi alisema serikali imetoa fedha kwa ajili ya baraza hilo na mambo mengine na kwamba muda muafaka utakapofika kikao cha baraza hilo kitaitishwa.

“Mwenyekiti wa Baraza anazungumzia vikao na mimi nasema kikao kitaitishwa, na wanaoitisha vikao ni Kamati ya Uongozi ya baraza hilo na waliitisha kikao cha juzi kati ya wadau wa siasa na NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) na kuwapa taarifa za matokeo ya maboresho ya daftari la awali la wapiga kura, hicho kilikuwa muhimu zaidi na kingine kitaitishwa karibuni,” alisema Jaji Mutungi kufafanua hoja za Shibuda.

“Kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, baraza hilo linaweza kukaa vikao hadi vinne kulingana na ajenda, sasa wanaoandaa kikao ni kamati ya uongozi, na ninajua wataandaa hivi karibuni na wadau wa siasa watajulishwa tarehe, wasubiri,” alisema Jaji Mutungi.

Shibuda alisema, “Leo tunaelekea kwenye uchaguzi, vikao vingapi vya baraza vimekaa? Na baraza ndio sehemu ya kujadiliana masuala ya kushauriana na serikali, wadau wa siasa hawana kikao au jukwaa la kushauriana na serikali ilihali mambo ya msingi ya kujadiliana yapo mengi na kwa sababu hiyo wanaenda kusema nje…sasa unawalaumuje wakati vyombo vilivyopewa mamlaka vimeshindwa kutimiza wajibu wao, hawatendi yale Rais Magufuli anayataka.”

Alisema wanasiasa au wadau wa siasa wa ndani wasilaumiwe kwa kukosa utiifu, bali wanaopaswa kuwajibika ni taasisi na vyombo vyenye mamlaka ya kuhakikisha masuala ya siasa nchini yanaenda vizuri.

“Utawalaumuje kuwa sio watiifu, wakati wewe huitishi vikao kuwapa nafasi ya kusema, nani anayeitisha vikao, Rais Magufuli hili wala sio lake, taasisi na vyombo vilivyopewa jukumu hilo…Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ipo, Sekretarieti ya Baraza ipo na Ofisi ya Waziri Mkuu ambao nao ni wasimamizi wa masuala ya siasa wapo. Sasa wamulikwe ili wabainike nani anakwamisha, kwa sababu baadhi wanajifanya wazalendo lakini ni wanafiki wanaoleta taswira hasi ya siasa nchini,” alieleza Shibuda.

Alimwomba Rais Magufuli kumulika taasisi hizo kuona utendaji wao katika siasa ulivyo kwani wapo baadhi wanamchafua na kuchafua mwenendo wa siasa hali inayoleta sintofahamu ya siasa na demokrasia.

Alisema ni jambo la kushangaza dira ya Serikali ya Awamu ya Tano na maudhui yake hazijatambulishwa kwa wadau wa siasa kwa kukosa vikao muhimu vya baraza ambalo ni sehemu ya kukutanisha wanasiasa na serikali na kuzungumza kisha kama kuna masuala ya kushauriana yanajadiliwa na kufikia muafaka.

KIWANGO cha mimba za utotoni kimeripotiwa kupungua kwa kasi katika ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi