loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM: Uchaguzi Mkuu, Bunge havitaahirishwa

RAIS John Magufuli amebainisha kuwa pamoja na kuwepo kwa ugonjwa wa corona nchini na duniani, Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, utafanyika kama ilivyopangwa.

Aidha, amesema vikao na mikutano ya ndani ya serikali, ikiwemo vikao vya madiwani na Bunge, vitaendelea kama kawaida, kwa kuzingatia zaidi tahadhari za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.

Rais Magufuli aliyasema hayo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma jana, wakati akipokea Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2018/19 iliyowasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Seriakali (CAG), Charles Kichere na Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2018/219, iliyowasilishwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Brigedia Jenerali John Mbungo.

“Hatujazuiwa kukutana, leo nilikuwa nasoma gazeti moja linasema madiwani wafanya kikao cha madiwani, sasa sijui alifikiri vikao vya madiwani vimezuiliwa kwa sababu ya corona?” alihoji Rais Magufuli.

Alisema serikali itaendelea na vikao vyake, kama kawaida, na ndio maana hata jana walikutana katika mkutano wa kawaida wa kupokea ripoti za taasisi hizo mbili.

Alisema pamoja na vikao vya serikali, lakini pia Bunge nalo litaendelea na vikao vyake. “Hata kwenye nchi zilizoathirika kabisa na corona mabunge yao bado hayajafungwa, bado mabaraza yao ya madiwani yanaendelea kufanyika. Kazi lazima iendelee kufanyika na uchaguzi tutafanya tu. Wako wengine wanafikiri nitaahirisha.

Nani anataka kukaa kwenye maofisi haya muda wote huo?,” alieleza. Virusi vya corona viliibuka katika Jimbo la Wuhan nchini China mwezi Desemba mwaka jana. Hadi sasa virusi hivyo vimesambaa katika nchi 180 duniani ikiwemo Tanzania, ambayo tayari yenyewe ina watu 13 walioambukizwa.

Baada ya corona kuingia nchini, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Magufuli walitangaza hatua mbalimbali, ambazo ni kufunga shule kuanzia awali, msingi, sekondari, vyuo vikuu na kati na kusitisha mikusanyiko ikiwemo mikutano, warsha, makongamano na michezo hasa ya ligi zote.

Pia, wasafiri wote wanaoingia nchini kutoka kwenye mataifa yaliyoathirika na corona wakiwemo Watanzania, sasa wanawekwa karantini kwa siku 14 kwa gharama zao wenyewe.

Aidha, serikali imeimarisha Maabara Kuu ya Taifa kwa kuipatia vifaa vya kisasa vya uchunguzi. Nayo maeneo yote ya vituo vya mipakani, yanayotumiwa na watu kuingia nchini, yamepelekewa vifaa vya kupima corona.

foto
Mwandishi: Baraka Messa, Ileje

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi