loader
Picha

Magufuli: Uozo aliobaini CAG usafishwe

RAIS John Magufuli amepokea Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2018/19 na kumuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kusimamia viongozi wengine wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa na makatibu wakuu, kuifanyia uchambuzi wa kweli na kuipatia majibu yale yote yaliyobainishwa katika ripoti hiyo.

Pia, amepokea Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ya mwaka 2018/19 na kuwataka viongozi wa ngazi zote kuanzia juu hadi chini, kuwajibika kwa kuhakikisha wanatatua matatizo ikiwemo dhuluma zinazowakumba wananchi wanyonge, kabla dhuluma na matatizo hayo hayajamfikia yeye kama Rais. Aliyasema hayo jana Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, baada ya kupokea ripoti hizo mbili kwa mujibu wa sheria.

“Ripoti nimeipokea (ya CAG), nitaikabidhi kwa wasaidizi wangu wakazifanyie kazi kupitia maeneo yao. Pia ni wajibu wetu kuikabidhi bungeni, ndio maana hapa Spika wa Bunge, Job Ndugai hajazungumza anasubiri akatudunde bungeni,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataja wasaidizi wake, aliowapatia ripoti hiyo kwa ajili ya kuifanyia kazi kuwa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Majaliwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi. Rais Magufuli alisema katika ripoti hiyo, imetaja na kugusa maeneo mengi yenye walakini zikiwemo taasisi nyeti, wizara na miradi mikubwa ya maendeleo.

“Sisi ndani ya serikali tuanze kuyafanyia kazi haya yaliyoelezwa, tupeleke ripoti hii bungeni, lakini kila waziri, mkuu wa mkoa na katibu mkuu, hoja zitakazotolewa bungeni tusisubiri kuzifanyia kazi, ziwe tayari na majibu,” alisisitiza.

Alisema hatua hiyo ya kujibu hoja zote, zilizoainishwa kwenye ripoti hiyo ya CAG itasaidia, kwani Bunge hilo litalojadili ripoti hiyo, ni la mwisho kwa kipindi cha awamu ya kwanza ya serikali yake, hivyo majibu hayo yatasaidia Bunge lijalo lisiwe na viporo kwa watendaji.

“Ikiwezekana tukajifungie kabisa mahali, tutafutie hizi hoja majibu, tuzifanyie kazi na hili nakuchia kabisa Waziri Mkuu ulibebe na watendaji, mawaziri na makatibu wakuu wako,” alisema.

Aidha, alimpongeza CAG, Charles Kichere kwa kuanza utaratibu mpya wa kukagua mashirika ya umma. Alieleza kuwa ilikuwa ni kitu cha ajabu kuweka watu binafsi, kukagua mashirika hayo ya umma wakati wakaguzi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) wapo, na wakati mwingine wanaenda kukagua nje ya nchi, huku wakijua kuna upungufu wa wakaguzi. “Kwa mashirika 10 tu umeokoa shilingi bilioni 1.4, je ukikagua yote utaokoa shilingi ngapi?

Hiki ni kitendo cha kizalendo na ndio Utanzania. Ng’ombe ni wako kwa nini ulete mtu mwingine akuhesabie? Kwa hiyo mmefanya vizuri katika hili,” alisema Rais Magufuli. Kuhusu ripoti hiyo, alisema itawasilishwa kama ilivyo bila kubadilishwa, kwa Ofisi ya Bunge kwa mujibu wa Katiba na masuala yote yaliyoainishwa, yakiwemo ya Chama Cha Mapinduzi Magufuli: Uozo aliobaini CAG usafishwe Rais Dk John Magufuli akipokea Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ya mwaka 2018/19 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Brigedia Jenerali John Mbungo, jana. (Picha na Ikulu). (CCM), yatajadiliwa na kuchambuliwa bungeni.

Aliitaka ofisi hiyo ya NAOT ifanye kazi kwa kifua mbele, kwani tayari anafahamu changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa ofisi hiyo, wanapoingia kwenye taasisi za serikali katika utendaji kazi wao. Aidha, alisema ofisi hiyo ilieleza wizi wa mabilioni uliofanyika katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia. Rais alisema kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, tayari ameshamrudisha, si balozi tena. “Hili litakuwa fundisho, ukiharibu sehemu lazima ubebe msalaba.

Ndio maana nawaomba viongozi wenzangu, hii ripoti itusaidia kuyarekebisha yale ya kuyarekebisha yaliyotajwa. Ripoti inaonesha taasisi muhimu kama polisi, wapo watu wanalipwa mishahara wameshakufa…”

“…Serikali haiwezi kuwalipa watu waliokufa kwa taasisi muhimu kama polisi wakati lokapu, pingu mnazo nyinyi, kwa nini mnawazunguka wanaohusika?. Nimetoa mfano tu, zipo wizara zimetajwa kuwa na matumizi yasiyo na document,” alieleza. Akizungumzia ripoti ya Takukuru, alimpongeza aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Brigedia Jenerali John Mbungo kwa kazi nzuri aliyofanya ya kuokoa Sh bilioni 8.8 za wakulima.

Alitangaza kuwa kwa kazi hiyo nzuri na nyingine, kuanzia jana alimthibitisha Mbungo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa.

“PCCB nawashukuru sana, tena hupaswi kuwa kaimu mpaka leo. Wewe ni mkurugenzi. Kama umerudisha fedha hizi, utarudisha nyingine. Wapo wengine wabaya hasa huyu wa Kinondoni na watu wake wanne. Nafikiri unamfahamu huyu na hawa, waangalie sana,” alisema Rais.

Alisema inakuaje hadi inafikia hali wananchi wa kawaida wanalima mazao yao, lakini hawalipwi huku viongozi wote wapo maofisini. “Mtu wa Takukuru ameeleza ameokoa fedha za wananchi zilizoibiwa na kuzirejesha. Sasa swali dogo tu unaweza kujiuliza je katika mikoa hiyo hakuna wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala, makatibu tarafa, maofisa kata, wenyeviti wa vijiji, mabalozi au hakuna viongozi wa vyama mbalimbali?”alihoji.

Alisema “Siku moja nilimuambia Waziri Mkuu kwamba wewe unatoka Lindi, nimekusikia mahali pengine unakemea kwanini Lindi wadhulumiwe shilingi bilioni 1.2 na wewe upo tena ni miongoni mwao”.

Alitaka kuanzia sasa viongozi wasisubiri mpaka taasisi kama Takukuru, ishughulikie matatizo ya wananchi. Awali, CAG Kichere wakati akiwasilisha ripoti hiyo alibainisha kuwa walikagua taasisi za serikali, mamlaka ya serikali za mitaa, mashirika ya umma na miradi mikubwa ya maendeleo na kutoa jumla ya hati 182. Alisema katika hati hizo, zilizoridhisha ni hati 1,017 sawa na asilimia 94, zenye shaka 46 sawa na asilimia 4.25, hati zisizoridhisha ni saba sawa na asilimia 0.64 na hati mbaya 12 sawa na asilimia 1.11.

Alitaja taasisi zilizopatiwa hati zisizoridhisha kuwa ni Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Kampuni ya Stangold, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Mradi wa Programu ya Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.

Maeneo mengine yaliyokaguliwa na kukutwa na utata ni mamlaka za serikali za mitaa ambako kuna dalili za ubadhirifu wa mabilioni ya fedha, baadhi balozi za Tanzania nje ya nchi na vyama vya siasa kikiwemo Chama cha Wananchi (CUF) chenye ruzuku ya Sh milioni 369.38, lakini kilihamisha Sh milioni 300 kutoka kwenye akaunti ya chama kwenda akaunti binafsi na fedha hizo hazikukaguliwa na CAG.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi