loader
Dstv Habarileo  Mobile
FURAHA: Mwanamke wa kwanza kuendesha bajaji ya abiria Morogoro

FURAHA: Mwanamke wa kwanza kuendesha bajaji ya abiria Morogoro

“UAMUZI wangu wa kufanya kazi ya kuendesha bajaji ya kubeba abiria uliwapa hofu wazazi wangu hasa baba aliyeonesha wasiwasi kuwa sitaweza kufanya kazi hii kwa vile aliona madereva wote wa bajaji ni wanaume na si wanawake,” hii ni kauli ya Furaha Stephano (23), dereva wa bajaji katika Manispaa ya Morogoro alipokuwa akizungumza na gazeti hili kuhusu harakati za maisha yake.

Furaha anasema baba yake aliwahi kumwambia kuwa hataweza kupambana barabarani na madereva wanaume lakini yeye alimhakikishia kuwa amesoma vizuri kozi ya udereva katika Chuo cha Veta Morogoro na kupata leseni hivyo haoni changamoto ya kumfanya ashindwe kuendesha magari au bajaji. “Hivi sasa baada ya kuniona nikiwa barabarani muda wa miezi minane hadi kufikia Machi mwaka huu tangu nianze kazi hii, baba yangu amekuwa mtu wa kuniombea dua nifike mbali,” anasema Furaha.

Wakati baba yake akionesha wasiwasi, anasema mama yake, Esther Matangoo alimtia moyo wa ujasiri akimwambia asiwe na wasiwasi kwani kazi hiyo ataiweza sawa na ilivyo kwa wanaume. Mbali ya wazazi wake kumpa moyo wa ujasiri, baadhi ya majirani zao wana mtazamo tofauti baadhi wakimshangaa kwa kitendo chake cha kuendesha bajaji ya kubeba abiria sawa na madereva wanaume.

“Majirani zangu hasa wanawake ninaporudi nyumbani wananiona mwanamke jasiri. Bado wanaamini mwamanke hawezi kitu,” anasema Furaha na kuongeza kuwa anaamini ule msemo wa asilimia 50 kwa 50 kati ya wanaume na wanawake kuwa kila jambo linawezekana kama kuna nia, malengo yanatimia. Kwa mujibu wa Furaha, maisha ni mchakato na mafanikio ya binadamu yanatokana na kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha.

Anasema tangu alipokuwa akisoma shule ya msingi ndoto yake ilikuwa ni kusomea udereva ili aweze kupata kazi ya kuendesha magari ya watalii nchini. Furaha na wazazi wake ni wakazi wa Bigwa katika Manispaa ya Morogoro.

Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Mgolole hadi mwaka 2012 na baadaye elimu ya sekondari kutoka kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule ya Sekondari Lupanga kutoka mwaka 2012 hadi mwaka 2016.

Anasema baada ya kumaliza elimu ya sekondari alichagua kusoma masomo ya Utalii Chuo cha Utalii cha Arusha lakini kabla ya kujiunga, alihamishiwa Chuo cha Utalii cha Serikali kilichopo Dodoma.

“Chuo cha Utalii cha Arusha ni cha binafsi lakini nilipelekwa Dodoma shule ya serikali, lakini sikuweza kusoma masomo ya utalii kutokana na changamoto za maisha zilizoikabili familia yangu,” alisema.

MAFUNZO YA AWALI YA UDEREVA

Baada ya kukosa fursa hiyo ya masomo, Furaha anasema aliamua kuchukua kozi ya awali ya udereva Chuo cha Veta kilichopo Kihonda Morogoro kwa muda wa mwezi moja, yaani Januari mwaka 2019.

Anasema Veta Kihonda alifundishwa kuendesha magari madogo, pikipiki na bajaji na kupatiwa leseni ndogo ya udereva. Baada ya kumaliza kozi hiyo alibaki nyumbani kwa miezi miwili na kufanya kazi ya ujasiriamali ya usambazaji chakula katika ofisi mbalimbali za mjini Morogoro ili kujipatia kipato. Anasema alifanya kazi hiyo kwa miezi minne kabla ya kuacha alipoona haimpi faida na inamchosha.

“Fedha niliyokuwa nikiipata haikuweza kunisaidia na haikuwa kazi chaguo langu,” anasema Furaha.

Furaha anasema, kwa kuwa tayari alikuwa na leseni ya udereva ya kuendesha magari madogo, pikipiki na bajaji, alimtafuta dereva mzoefu wa bajaji ya kusafirisha abiria ampe mbinu za kufanya kazi hiyo.

Furaha anasema alimpata Elias Myungile aliyempa mbinu na uelewa wa kuendesha abiria na kuzoea barabara na changamoto zake kitendo kilichompa uzoefu zaidi na kufanya aweze kufanya kazi hadi leo. Mwanamke huyo jasiri anasema, baada ya kupatiwa maelekezo na dereva mzoefu, alifanikiwa kupata bajaji yake ya kwanza baada ya kuingia makubaliano na mmiliki wa bajaji ili awaze kuanza kazi.

“ Njia niliyoichagua ni kutoka Mjini – Bigwa - Nane Nane na nilifahamika mara moja kwa kuwa dereva wa bajaji mwanamke nimekuwa pekee yangu hapa manispaa ya Morogoro,” anasema Furaha.

Hata hivyo, Furaha anasema hakudumu sana na bajaji kwani aliugua kwa muda na hivyo kushindwa kabisa kuendelea na kazi hiyo na aliporejea alikuta tayari mmiliki wake amempatia dereva mwingine.

Anasema kutokana na kufahamika kwake alipata mmiliki mwingine aliyempatia bajaji afanye biashara ya usafirishaji wa abiria na hadi sasa anaendelea na kazi hiyo na ametimiza miezi nane tangu arejee. Furaha anabainisha lengo lake ni kutimiza ndoto yake ya kusoma zaidi kozi ya udereva aweze kupata leseni kubwa itakayomwezesha kupata kazi ya kuendesha magari ya viongozi au mabasi ya mikoani.

MAISHA YAKE BINAFSI

Furaha anasema kwa kuwa yeye ni dereva pekee mwanamke wa bajaji ya kubeba abiria, alipoanza kazi alikabiliwa na changamoto nyingi kutoka kwa baadhi ya madereva wanaume na abiria hasa wanaume.

“Nilipoanza kazi hii nilikuwa nikisumbuliwa na baadhi ya madereva wanaume lakini abiria wanaume ndio walikuwa wasumbufu zaidi. Walihitaji namba yangu ya simu wakiwa kama wateja,” anasema.

Furaha anasema wanapochukua namba ya simu kwa ajili ya shughuli za kazi yake ya bajaji, baadhi ya wateja walikuwa wanageuka na kumpigia simu si kwa ajili ya kutaka usafiri na kuingiza masuala ya mapenzi, changamoto ambayo anaendelea kupambana nayo na kuwapotezea wateja wanaombugudhi.

 “Mimi ninajiheshimu na nina heshimu kazi yangu. Wapo wanaume walinifuata hadi kwenda kwa wazazi wangu kutaka wanioe, nimekataa. Kwanza, nahitaji kujenga maisha yangu yasiyo na utegemezi kwa mtu yeyote.

Nategemewa na familia yetu. Kwa sasa sina mume wala mpango wa kuwa na mtoto,” anasema. Anasema wazazi wake wana umri mkubwa na hawawezi kufanya kazi hivyo wanamtengemea na ana wadogo zake watatu , wawili wanasoma shule ya msingi na mmoja amemaliza elimu ya kidato cha nne.

KISA CHA BARABARANI

Furaha anaeleza kisa kimojawapo ambacho bado anakikumbuka alipokuwa akitekeleza shughuli yake ya kusafirisha abiria kwa bajaji siku za mwanzo ni kutokuwa na uelewa wa aina ya mavazi akiwa kazini.

“Sikuwa na uelewa siku za mwanzo nilipoanza kuendesha bajaji. Sikujua ni mavazi ya namna gani ya kuvaliwa nikiendesha bajaji barabarani kwa mimi mwanamke … nakumbua kisa kilichonipata siku moja nikiwa nimempakia mteja wangu kutoka Bigwa kwenda Rock Garden nilisimamishwa njiani na Askari wa Usalama Barabarani alikagua leseni na bima vyote vilikuwa hai,” anakumbuka Furaha.

Anasema askari huyo alimuuliza kwa nini anaendesha bajaji ya kusafirisha abiria akiwa amevaa sketi wakati sheria inakataza kwa mwanamke ikimtaka kuvaa suruali anapoendesha usafiri huo au pikipiki. Anasema askari huyo alimfahamisha anapoendesha bajaji au pikipiki avae suruali siyo gauni au sketi.

“Askari aliniamuru nirudi nyumbani nikavae suruali. Nilishuka na kuiacha bajaji na mteja wangu na nikachukua usafiri wa bodaboda hadi nyumbani kubadilisha nguo na kuvaa suruali kama nilivyoelekezwa na kurudi kuendelea na safari ya kufikisha mteja wangu sehemu alikohitaji kufikishwa,” anasema Furaha.

Anasema jambo hilo lilikuwa elimu tosha kwake na tangu siku hiyo amekuwa akivaa suruali isipokuwa kama yuko nyumbani baada ya kazi anakuwa dada na mwanamke anayezingatia uvaaji sketi na gauni.

UZINGATIAJI SHERIA ZA USALAMA BARABARANI

Kuhusu kazi ya udereva, Furaha anasema ni nzuri na inahitaji ustadi na uzoefu mkubwa, lakini pia inahitaji mtu kuwa na mtazamo sahihi na ustadi unaofundishwa na mwalimu darasani na kwa vitendo.

Kwa kutambua umuhimu huo, anasema, akiwa barabarani anafuata sheria zote za usalama barabarani, anakwenda mwendo wa kawaida jambo lililomwongezea imani kwa wateja wanaomkodisha na utaratibu wa zamu kwenye kituo chao kilichopo pembezoni mwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro.

“Ninapata abiria kwa kukaa zamu ( foleni ). Siwakimbilii abiria na pia sina ubavu wa kufukuzana barabarani kama ilivyo kwa baadhi ya madereva hasa waliotokea kuendesha bodaboda,” anasema.

Furaha anasema amekuwa mwaminifu kwa bosi wake, mmiliki wa bajaji kwa kuwasilisha kila siku kiwango walichokubaliana na makusanyo yanapokuwa yamepungua mmiliki hukubaliana na hali halisi.

MALENGO YA BAADAYE

Anasema bado lengo lake ni kuendelea na masomo zaidi ya udereva Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) apate nafasi ya kazi kwani anatamani kuwaendesha viongozi au hata mabasi ya abiria ya mikoani.

“Nahitaji uwezeshaji, ufadhili wa kunifikisha mbali katika ndoto zangu za udereva niende NIT kwa mafunzo yatakayoniwezesha kupata kazi ya kuendesha magari ya viongozi au mabasi ya mikoani,” anasema Furaha. Anasema, ndoto yake ikitimia ataweza kuwasaidia wazazi wake na wadogo zake.

VITU ANAVYOPENDA

Anasema ni wajibu kwa wanawake kujitoa kushiriki shughuli za uzalishaji mali na ujasiriamali badala ya kukaa nyumbani na kulalamika kwa kuwategemea wanaume , hali inayowarudisha nyuma kimaisha. Anasema mbali ya udereva, anapenda michezo hasa netiboli tangu akiwa shule ya msingi hadi sekondari.

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi