loader
Picha

Wizara- Corona si ugonjwa wa wazungu

WANANCHI wanatakiwa kupewa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) ili kuepusha usisambae zaidi nchini sasa.

Hadi jana, Dar es Salaam ndiyo inaelezwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa Corona.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk John Jingu amesema katika mafunzo ya kukabili corona kwa maofisa wa ustawi wa jamii, Ofisa maendeleo na Msalaba Mwekundu Ukumbi wa Manispaa ya Temeke, Dar es salaam.

Dk Jingu amesema upashanaji elimu ya kujikinga na maambukizi ya Corona kwa wananchi ni jambo muhimu kwani jamii inapaswa kuwa na uelewa wa pamoja ugonjwa unavyoambukizwa na dalili zake ili kila rika lifahamu na kuepusha ugonjwa usiendelee kusambaa zaidi nchini.

“Dar es Salaam ndio yenye wagonjwa wengi zaidi wa Corona. Madaktari ni wachache hivyo ni muhimu watu wapewe elimu kujilinda ugonjwa usije kusambaa zaidi,” Dk Jingu alionya.

Alisema Dar es Salama ina wagonjwa wengi kutokana na kuwa lango kuu la biashara kwani ina bandari, uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hivyo mwingiliano mkubwa.

Alisema wanawapa mafunzo maofisa wa ustawi wa jamii, maofisa maendeleo na Msalaba Mwekundu ili wakatoe elimu zaidi kwa wananchi namna ya kuepuka ugonjwa huo kwani madaktari ni wachache hivyo watu wanapaswa kujikinga ili ugonjwa huo usiendelee kuenea.

“Dar es Salaam iko mstari wa mbele, kuna wapiganaji. Kesi ambazo tumezipata wengi wametoka nje ya nchi, maeneo ya mipaka. Dar es Salaam haipo mpakani lakini ina uwanja wa ndege mkubwa, wageni wengi wanaingia, bandari na kituo kikubwa cha basi,”alisema .

Alisema juhudi kubwa zimefanywa na serikali kuzuia ugonjwa wa Corona kuenea zaidi.

“Angalia Mataifa makubwa yanavyohangaika na Corona. Italia, Hispania, Uingereza na Marekani ni mataifa makubwa yameumizwa na yanaendelea kuumizwa na Corona, “ alisema.

Vitu vya kuepuka Dk Jingu alisema wananchi wanatakiwa kuacha tabia ya mazoea ya kupiga soga na kugonga mikono, mnakutana mnapeana mikono, kukumbatiana, dhana hiyo inapaswa kuachwa kutokana na janga hilo la Corona ambalo limeshaua maelfu ya watu duniani kote.

“Kuna dhana huu ugonjwa ni wa wazungu, dhana hii ni potofu, inabidi iachwe, ugonjwa huu sio wa wazungu ni ugonjwa wetu sote, cha msingi ni kujilinda,”alisema Dk Jingu akionya.

Dk Jingu alisema kuna watu wachache wanaochukua tahadhari, lakini wengi ni kama hawajui kinachoendelea na kuwataka maofisa hao wakawasaidie kwa kutoa elimu kwa wananchi ili wawe salama, kuwaelimisha kunawa mikono kwenye maji tiririka, kukaa bila kuangaliana, wapeane nafasi wakati wa kukaa, na pia kujiziba wakati wa kupiga chafya.

Alisema miongozo ya serikali lazima ifuatwe na itekelezwe, baadhi ya vitu vimekatazwa nchi nyingine lakini hapa havijakatazwa akitolea mfano watu kukaa ndani bila kutoka nje kufanya shuguliza kila siku, na iwapo serikali itachukua uamuzi wa kuzuia watu kutoka nje, basi watakuwa wamewakinga na janga la Corona lakini wengi watapoteza maisha kwa njaa.

Dk Tumaini Haonga, ofisa Programu kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto alisema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza juhudi katika vita vya ugonjwa huo wa Corona ili kupambana zaidi kuzuia mambukizi miongoni mwa jamii.

Alisema ili kufanikiwa, lazima wajenge utayari katika mifumo ya kijamii, kama viongozi wa serikali za mitaa ili kutumia mifumo iliyopo wakatoe mafunzo kuanzia ngazi ya halmashauri hadi mitaa wananchi wapate taarifa sahihi ugonjwa unavyoenea na kujikinga asiambukize.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Shamira Hassan, Ofisa Maendeleo Manispaa ya Temeke alisema Dar es Salaam siyo kisiwa, inapokea wageni wengi hivyo mafunzo hayo ni muhimu kwao, watayatumia kutoa elimu kwa mama lishe, kwenye madaladala, sokoni na maeneo mengine yote ikiwemo kanisani na misikitini ili kusaidia ugonjwa huo usisambae.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua imetoa mikopo ya Sh milioni ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi