loader
Picha

Yanga wapewa faili la mrithi wa Tshishimbi

WAKATI Yanga ikiendelea na mazungumzo ya kumbakisha nahodha wao, Papy Tshishimbi, fasta tu Yanga wamepewa mchongo kwamba hakuna litakaloharibika kama mambo hayataenda sawa kwani wapo viungo wenye uwezo wa kuziba nafasi yake.

Tshishimbi amebakisha mkataba wa miezi minne Yanga na tayari Simba wameripotiwa kumfuata na kumuwekea dau nono, ili msimu ujao avae uzi mwekundu.

Hata hivyo baadhi ya wadau wa soka wanaamini kama Tshishimbi ataondoka, wapo viungo ambao wanaweza kucheza kama yeye akiwemo kiungo wa Mtibwa Sugar , Abdulharim Humud ni suala la Yanga Humud anayekipiga Mtibwa Sugar amekuwa akihusishwa kutua Yanga kutokana na kiwango kikubwa alichokionesha tangu kuanza kwa msimu huu, ikielezwa kuwa hata kocha Luc Eymael wa Yanga anaielewa kazi yake na hata yeye Humud pia yupo tayari kufanya kazi chini yake.

Kocha Kenny Mwaisabula aliyewahi kuinoa Yanga miaka ya nyuma, ameliambia gazeti hili kuwa kwake anaona siyo tatizo kama Tshishimbi ataondoka na Humud kutua kuchukua mikoba yake kulingana na aina ya uchezaji wao na hata walivyo ni kama wachezaji ambao wanashabihiana.

“Ukimuangalia Tshishimbi ni mtu ambaye hapishani sana na Humud. Wote wanacheza nafasi zinazofanana na jinsi wanavyotimiza majukumu yao wanashabihiana, isipokuwa Humud anakaba kwa kutumia nguvu kubwa tofauti kidogo na Tshishimbi, kwa hiyo kwangu naamini kama Humud akija na Tshishimbi akaondoka hakitaharibika kitu.

“Japokuwa naamini kwa timu kama Yanga, kwa ukubwa ilionao inahitaji upinzani mkubwa katika kila nafasi uwanjani kwa hiyo kama Tshishimbi atabaki na Humud pia akaja, itakuwa ni kitu kizuri mno maana yake inatoa uwanja mpana kwa kikosi kulingana na umuhimu na uwezo wa hawa wachezaji na unaweza ukawatumia wote pia ikawa na faida,” alisema Mwaisabula.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Mwanamtwa Kihwelu naye hakutofautiana sana na Mwaisabula isipokuwa alisisitiza namna Yanga inavyoweza kujijenga bila ya kumzunguka mchezaji mmoja.

“Siku zote Yanga imekuwa ikicheza bila ya kumzunguka mtu mmoja ndiyo maana sioni tatizo kama itatokea Tshishimbi akaondoka na mwingine kama Humud kuja kuziba nafasi yake. Yanga kulingana na jinsi ilivyo mtu kama Humud anaweza kufiti bila tatizo, kama ilivyokuwa walipoondoka wachezaji wengi mahiri na bado wengine wanaweza kuja na kumsahaulisha yule aliyekwenda,” alisema Kihwelu.

Pamoja na hayo, Eymael tayari amesisitiza na kufafanua jinsi gani bado anamuhitaji Tshishimbi na ameshazungumza binafsi na mchezaji pamoja na uongozi juu ya umuhimu wa kuendelea kumshuhudia kiungo huyo rasta akifanya kazi zake akiwa na Yanga msimu ujao.

Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. David Ruhago amesema wamekutana na Tshishimbi na kwamba mazungumzo yao kuhusu kuongeza mkataba yamefikia pazuri.

“Najua wenzetu Simba, wamekuwa wakimsumbua wakitaka asaini kwao, lakini wanajisumbua, tunatambua mchango wake ndani ya timu, ndio maana tumedhamiria kupambana, ili kuhakikisha yeye na wachezaji wengine waliopendekezwa na kocha hawaondoki,” alisema.

Tshishimbi ni kati ya viungo walioonesha uwezo mkubwa katika Ligi Kuu Bara tangu alipotua katika dirisha dogo Januari, 2018 na amekuwa kikwazo kwa safu ya kiungo ya Simba kila wakati zinapokutana timu hizo.

KLABU ya Tottenham imepata mkopo wa Pauni milioni 175 sawa ...

foto
Mwandishi: Hans Mloli

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi