loader
Picha

Mpango wa ushauri unavyojenga, kuimarisha  vijana kifikra

USHAURI ni suala lenye umuhimu wa kipekee kwa vijana kwani limekuwa likiwapatia matokeo chanya, huku likiwafanya wengine kufanikiwa kuwa mfano wa kuigwa na wenzao baada ya kujengewa uwezo wa kufikiri kwa mapana zaidi na hatimaye kufikia ndoto zao; hasa zile za kuwa na maisha bora katika jamii zao.

Kama njia ya kuwajengea vijana uwezo na kuwawezesha kutumia fursa zilizopo zikiwemo za kiuchumi na ajira, hadi sasa tayari kuna vijana 18,000 wamepata ushauri na zaidi ya 600 wamepewa mafunzo kadhaa wa kadhaa ndani ya miaka mitatu.

Kupitia ushauri na mafunzo, vijana walihamasishwa na kuwezeshwa kuzitambua fursa zilizopo ili kufikia ndoto zao, kuchukua hatua, kuwa wabunifu na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii zao.

Mwaka 2017 Mfuko wa Kijamii wa Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Bridge for Change, waliendesha programu maalumu iliyolenga kutoa ushauri na kufundisha wanafunzi katika Shule za Sekondari za Kibasila na Kilangalala zilizopo wilayani Temeke katika Jiji la Dar es Salaam.

Programu hiyo ililenga kuwasaidia wanafunzi kutengeneza mipango thabiti ya maisha kwa siku zijazo kwa kuwajengea ufahamu mahususi wa ajira na kuwaunganisha na washauri.

Zakia Mrisho (20) na Albert Chinguile (21) ni miongoni mwa vijana walioshiriki katika programu hiyo ambao sasa wanakiri wakisema kuwa, sasa wanaona ndoto zao zinaelekea kutimia.

Zakia anasema baada ya kushiriki katika programu hiyo sasa anajisikia dhahiri kuwa amekuwa kiongozi mzuri kwa wenzake na sasa anawahimiza wanafunzi katika shule kadhaa za Wilaya ya Kisarawe juu ya umuhimu wa elimu na fursa zilizopo.

Zakia, ambaye ni mwasisi wa taasisi ya Smart Heroes Foundation inayojihusisha na  utoaji wa ushauri kwa vijana walioacha shule anasema: “Lengo langu ni kutoa ushauri kwa wengine kile nilichokipata kwa sababu hawakufanikiwa kupata fursa kama ya kwangu. Vijana wanatakiwa kujua kwa nini wako shuleni, faida ya kusoma kwa bidii, na kuwatia hamasa. Kuna kila sababu ya kutoa hamasa hizi kwa vijana.” Kijana huyu amefanikiwa kujitafutia wafadhili kwa ajili ya masomo ya Stashahada ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika Chuo cha NLAB Innovation College kilichopo jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Albert Chinguile (21) ambaye pia ni mwanafunzi aliyeshiriki katika programu hiyo katika Sekondari ya Kilangalala, anatoa ushuhuda wake wenye matokeo chanya unaodhihirisha umuhimu wa programu ya ushauri kwa vijana.

Kwa mujibu wa Chinguile, baada ya programu hiyo alijikuta akibadilisha mwelekeo wake baada ya kuachana na masomo ya sayansi na kujiunga na mchepuo wa sanaa.

Kwa sasa, Chinguile ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akisoma masomo ya Saikolojia ya Binadamu.

 “Kupitia programu hiyo maalumu, nilipata nafasi ya kufahamiana na watu maarufu na taasisi mbalimbali ikiwamo hii ya Bridge for Change ambapo nafanya kazi kwa sasa lakini, muda wangu wa ziada huwa nautumia kuwashauri vijana wenzangu na wengi wao wameweza kujitambua na kufahamu umuhimu wa elimu na fursa zilizopo mbele yao na hata kuwashawishi wale waliokuwa wameacha shule kurejea tena masomoni,” anasema Chinguile.

Najenjwa Mbagga, ni mshauri kutoka Vodacom Tanzania aliyeshiriki katika programu hiyo kama mshauri. Anasema ulikuwa wakati mzuri kwake kubadilishana mawazo na wanafunzi na hasa wale wanaosoma sekondari za kata.

 “Programu ilikuwa na manufaa kwani kuna mambo mengi nimejifunza, kwa mfano, namna wanavyofanya uamuzi. Wachache wanaonekana kuwa na dhamira kimaisha huku wengine wakionekana kutokuwa na uhakika wa kile wanachokihitaji katika maisha yao,”anasema Mbagga.

Mbagga anasema kuwa kuna umuhimu wa mpango wa ushauri kuanzia darasa la kwanza na anashauri.

Anasema: “Maisha yana changamoto ambazo unaweza kuzikabili. Kuna watu wenye uzoefu wa kutosha ambao unaweza kujifunza kutoka kwao kuliko kupigana pekee yako bila mafanikio. Washauri wanaweza kukusaidia kuona mambo yako katika mtazamo tofauti kimasomo, ustawi, maamuzi sahihi na mengine mengi.”

Naye Happiness Shuma ambaye ni Mshauri mwingine kutoka Vodacom Tanzania, anasema kuwa ushauri ni muhimu kwa ajili ya kujenga maarifa na stadi kutoka kwa mshauri kwenda kwa mshauriwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Bridge for Change, Ochek Msuva, anasema kuwa ushirikiano wao na Vodacom umechangia kwa kiasi kikubwa taasisi hiyo kuwafikia vijana 18,000 kwa kutoa mafunzo kwa vijana 600 ndani ya miaka mitatu iliyopita.

“Mpango huu ulitoa mchango mkubwa sana kwa sababu mara nyingi vijana wako hatarini kufanya uamuzi usiokuwa sahihi. Ndiyo maana kuwa na mshauri ni jambo la muhimu sana ili kuondoa hali ya vijana kufanya mambo bila kufikiri kwa undani, lakini pia kutengeneza fursa zenye mafanikio,” anasema Msuva.

 

Kwa mujibu wa Msuva, Vodacom Tanzania Foundation ilitoa rasilimali zote zilizohitajika kwa programu hiyo, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wake kushiriki katika kufundisha na kushauri wanafunzi. Bridge for Change walikuwa na jukumu la kuratibu, na kuhamasisha vijana.

 “Halikadhalika tumefanikiwa kujenga uhusiano mzuri na shule mbalimbali. Kwa mfano, Kimara Temboni ya Dar es Salaam, na kutoa fursa ya ufikiwaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa wanafunzi na walimu. Hii inawawezesha kutoa mwongozo mzuri wa masomo ya Tehama,” anasema Msuva.

Kwa mtazamo wake, Msuva anasema mbali na harakati za kuwajengea vijana uwezo wa kujitambua kwa nafasi na wakati, pia ameongeza uwezo binafsi kama kiongozi mwenye lengo la kukuza vijana.

“Kwa kufanya programu za vijana, tumepata washirika wenye dhamira kwa ajili ya kukuza fikra za vijana kwa undani kwa kuzingatia maslahi ya pande zote,” Msuva anasisitiza.

 

WAKULIMA wa Kijiji cha Manda Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi