loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kunjal: Mwanamke mpambanaji asiyependa mzaha kazini

Kunjal: Mwanamke mpambanaji asiyependa mzaha kazini

“Dhamira yangu siku zote ni kufanya kazi kwa bidii na kujituma wakati wote ili niweze kutimiza ndoto zangu, lakini pia kutekeleza kwa vitendo mwito wa Rais wetu John Magufuli anayemtaka kila mtu kuchapa kazi ili kujiinua kimaisha na kuipeleka mbele nchi yetu kiuchumi”.

Ni kauli ya Gina Kunjal, maarufu kwa jina la Kunjal mfanyakazi katika kiwanda kinachozalisha vifaa vya umeme cha AFRICAB, Dar es Salaam, Meneja anayehusika na masuala ya Utawala. Akizungumzia majukumu yake kiwandani hapo, anasema katika utekelezaji wa majukumu yake anaamini hakuna kinachoshindikana kama mtu akiweka dhamira ya dhati katika jambo husika.

Kunjal anasema msimamo wake huo ndio uliomfikisha hapo kwa sasa akiwa kiunganishi kikuu kati ya uongozi, wafanyakazi na wadau wao wa kibiashara. Miongoni mwa shughuli zake, ni kuiunganisha kampuni yake na wadau mbalimbali ambao ni wateja wa bidhaa za umeme zinazozalishwa kiwandani hapo zikiwemo nyaya, transfoma, vikombe vya umeme.

Anataja wadau wakuu ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Wakala wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA) pamoja na wadau wengine wa masuala ya umeme. Kunjal ameolewa, ana watoto kadhaa na kuwa familia yake imekuwa sehemu kubwa ya msaada kwenye utekelezaji wa majukumu yake ya kazi.

Anasema chini ya serikali ya awamu ya tano yanafanyika mambo NYOTA HABARILEO JUMAPILI APRILI 5, 2020 NYOTA Gina Kunjal akitekeleza majukumu yake ofisini kwake. Akitoa maelezo ya uzalishaji kiwandani mbele ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Nishati.

Kunjal: mengi na mazuri ya maendeleo, hatua inayotokana na fursa nyingi ikiwemo ya uwekezaji iliyotolewa na Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani, jambo analosisitiza kuwa ndilo linalochangia maendeleo ya kasi ya kiuchumi na kuipeleka mbele Tanzania.

Anasema chini ya utawala wa Rais Magufuli, Tanzania imeshuhudiwa ikipiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda na kuongezeka tija kwa viwanda vilivyokuwepo huku ajira nazo zikiongezeka kwa kasi tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Kunjal anasema anaiona Tanzania kuwa nafasi ya juu kwa kuwa na viwanda bora vinavyozalisha bidhaa zenye ubora zinazovutia mataifa mengine kuhitaji bidhaa hizo.

Anasema pamoja na mafanikio hayo yanayotokana na kuongezeka kwa viwanda bado kuna changamoto ya baadhi ya bidhaa hapa nchini kuzalishwa na ubora hafifu. Anasema kuzalisha bidhaa zisizo na ubora unaotakiwa ni jambo linalohatarisha au kuondoa sifa nzuri kwa bidhaa zinazotengenezwa nchini ambazo zimepata soko nje ya nchi.

“Mfano bidhaa tunazozalisha katika kiwanda chetu kwa sasa zimepata soko kubwa katika mataifa ya Congo, Zimbabwe pamoja na Zambia ambapo kwa namna ya kipekee tunaishukuru Serikali yetu ya Tanzania kutusaidia hadi tumefanikiwa kuwekeza nchini Zambia baada ya bidhaa zetu kukubalika nchini humo,” anasema Kunjal.

Anasema hakuna ubishi kuwa kwa sasa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini zina ubora wa juu kuliko hata zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi huku akiipongeza serikali kwa hatua wanazoendelea kuzichukua kwa siku za hivi karibuni.

Anataja hatua hizo kuwa ni pamoja na kusitisha uingizwaji wa vifaa vya umeme kutoka nje, lengo likiwa ni kuvilinda viwanda vya ndani ambavyo vimeonesha uwezo wa kuzalisha bidhaa bora.

“Kipekee naomba sana kuwashukuru mawaziri wetu wanaohusika na sekta ya nishati, Dk Medard Kalemani pamoja na Subira Mgalu kwa juhudi zao wanazozichukua kulinda soko la ndani, ukweli wametusaidia sisi wazalishaji wa ndani kulinda soko letu ingawa bado kuna watu wachache wanaoingiza bidhaa hizo kwa njia ya magendo,”anasema Kunjal.

Anasisitiza kuwa hakuna sababu wala ulazima wowote wa kuingizwa kwa vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi kwa kuwa tayari viwanda vya hapa nchini vimeonesha uwezo mkubwa katika uzalishaji wa bidhaa hizo huku akitolea mfano kwa kiwanda cha AFRICAB ambacho kina uwezo wa kuzalisha kwa mwaka nyaya za umeme kilomita 75,000 transfoma 6,500 na vikombe vya umeme 660,000.

“Tunaishukuru Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati kwa moyo mzuri iliyotupa ilipofanya ziara yake hivi karibuni, kimsingi ilituhakikishia kuwa itaiagiza Serikali kuhakikisha inatulinda sisi kama wazalishaji wa ndani, hatua ambayo pamoja na mambo mengine itasaidia kukuza uchumi wetu”, aliongeza Kunjal.

Pamoja na hayo alisema bado kuna kila sababu kwa mamlaka zinazohusika na masuala mbalimbali ikiwemo TBS kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda vya hapa nchini pamoja na madukani ili kudhibiti kuzalishwa au kuzagaa kwa bidhaa zisizo na ubora ambazo matokeo yake ni vilio kwa wananchi pindi bidhaa hizo zinaposababisha janga la moto.

Anasema hakuna shaka kuwa pamoja na uwepo wa viwanda vinavyozalisha bidhaa zenye ubora wa juu, bado vipo baadhi ya viwanda na wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiwauzia wananchi bidhaa hizo kwa bei za chini na baadae kuwaletea madhara hayo ambaye mwisho wake hugeuka kuwa hasara kubwa kwa wananchi hao.

“Tunapaswa kuijenga nchi yetu na kila mmoja ajivunie kuwa katika nchi yenye mafanikio, kwetu hatushindani na yeyote bali tunawaona kama wenzetu ambao tupo kwa lengo moja la kuipeleka mbele nchi yetu kiuchumi na kimaendeleo ili mwisho tujisifu kama watanzania huku tukizidi kuijenga vyema nchi yetu”, anasisitiza Kunjal Matarajio yake

Anasema kutokana na utendaji wake matarajio yake ni kuona siku moja anaiwezesha kampuni yake kufika mbali kiutendaji na uzalishaji wa bidhaa zitazoweza kuliteka soko la nchi mbalimbali zikiwemo zilizopo katika ukanda wa SADC ili kuitikia mwito wa Rais Magufuli aliyewataka watanzania wote kulichangamkia soko hilo.

“Siku zote huwa naamini hakuna kinachoshindikana katika maisha kama umekiwekea nia, kwangu mimi nitajiona nimetimiza ndoto zangu pale bidhaa zetu zitakavyoweza kwenda mbali zaidi ya haya mataifa michache tunayoyahudumia kwa sasa, Rais wetu katufungulia njia jukumu lililobaki ni letu kuhakikisha tuna tunasonga mbele,” anasisitiza Kunjal.

Anachopendelea Kunjal anasema mara nyingi baada ya kazi hupendelea kuwa karibu na familia yake na wakati mwingine hufanya mazoezi madogo madogo kwa ajili ya kuuweka sawa mwili wake, lakini pia kujisomea vitabu mbalimbali hususani vinavyohusu masuala ya biashara na uongozi.

Asichokipenda Anasema kitu asichokipenda kwenye maisha yake ni kuona watu wakikaa vijiweni na mitaani bila ya kufanya kazi na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya taifa lenye fursa mbalimbali zikiwemo za kilimo, viwandani pamoja na sekta nyingine ambazo kimsingi zinaweza kuwaingizia kitu chochote kuliko kukaa bila kufanya kazi.

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi