loader
Wagonjwa watano wapona corona

Wagonjwa watano wapona corona

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (pichani) amesema wagonjwa wawili kati ya watu 24 walioathirika na virusi vya corona nchini, wamepona na kuruhusiwa jana, hivyo kufanya idadi ya waliopona ugonjwa huo hadi sasa kuwa watano.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam baada ya kupokea msaada wa vifaa vya kukabiliana na corona kutoka kwa wafanyabiashara Watanzania, Ummy alisema hadi sasa wagonjwa waliobainika kuwa na virusi hivyo nchini ni 24.

“Tunashukuru Mungu sampuli zilizochukuliwa jana kwa ajili ya vipimo kwenye Maabara Kuu majibu yametoka hayana maambukizi, hivyo walioambukizwa idadi yao hadi leo (jana) ni watu 24 na jambo la furaha ni kwamba watu wawili kati ya hao 24 wamepona na tumewaruhusu leo (jana),”alisema Ummy.

Akifafanua hali ilivyo kwa ugonjwa huo nchini, Ummy alisema kati ya wagonjwa wote 24, mmoja amefariki, waliopona hadi sasa ni watano, ambao kati ya hao watano, wawili ni hao walioruhusiwa jana mmoja akiwa wa Dar es Salaam na mwingine wa Arusha.

Aidha, wengine watatu waliopona awali mmoja pia ni wa Arusha, mwingine Kagera na mwingine wa Dar es Salaam na kwamba ambao hadi sasa wameathirika ni 18, na wametoka Dar es Salaam, Zanzibar na Mwanza.

Akizungumzia hali zao, Ummy alisema 17 wako kwenye hali nzuri na mmoja hali yake sio nzuri. Alitoa mwito kwa wale wote waliopona kuchukua tahadhari, kwani wanaweza kuambukizwa tena virusi hivyo, iwapo hawatazingatia kanuni na maelekezo ya kujikinga na ugonjwa huo.

“Nitoe tu angalizo kwa wote walipona corona kwamba wachukue tahadhari. Kuugua na kupona sio kwamba huwezi tena kuugua, usipochukua tahadhari utaambukizwa tena…China wanasema kati ya watu 100 waliopona corona na kuruhusiwa wanne huambukizwa tena iwapo hawachukui tahadhari,” alisema Ummy.

Aliwataka wanajamii kuwapokea watu hao, waliopona corona na kutowanyanyapaa, kwani hawana tena maambukizi, bali jamii yote iendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo. Pia aliwataka wanahabari nao, kuchukua tahadhari na kuvishauri vyombo vya habari nchini, kuangalia namna bora ya kutimiza majukumu yao ili kupunguza uwekezano wa kuambukizwa virusi hivyo.

Akizungumzia suala la kuwekwa karantini kwa watu wote wanaoingia nchini kwa gharama zao, Ummy alisema Aprili 4, mwaka huu serikali ilitoa Waraka wa Pili, ulioelekeza wasafiri wote wanaoingia nchini kutoka nje ya nchi, ni lazima wakae karantini kwa gharama zao.

“Hatuna utani na suala la karantini, wageni wote watakaa hosteli za Magufuli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa garama zao, changamoto zilizopo pale tunazifanyia kazi, ila ni lazima wote wakae pale, kipaumbele chetu ni kuhakikisha hakuna maambukizi mapya yanayoingia kutoka nje, ndio maana wote lazima wakae karantini.

“Kuna maswali yule muathirika aliyebainika alitokea Dubai ilikuaje…majibu ni kwamba aliingia nchini kabla ya Waraka wa Aprili 4, na hivyo yeye alifuata Waraka wa Kwanza tuliotoa Machi 23, wa kuwataka wale wote wanaoingia nchini wakitoka nchi zenye maambukizi ya corona kwa kiwango kikubwa, kukaa karantini na sio nchi zote,” alisema Ummy.

Akizungumzia vifaa vya kupambana na corona vilivyotolewa na mfanyabiashara maarufu nchini, Subash Patel, alisema wametimiza ahadi waliyotoa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kuchangia vifaa 1,000 vya kukabili corona.

Alisema vifaa hivyo ni madumu ya kunawia mikono 1,000 ambayo Mkoa wa Dar es Salaam umepewa 350. Mikoa iliyosalia nchini kila mmoja utapata madumu 26 kwa ajili ya kusambaza kwenye maeneo ya wazi ili wananchi watumie kunawia mikono. Alisema Mkoa wa Dar es Salaam umepewa idadi kubwa kwa sababu una watu wengi na pia maambukizi mengi yako kwenye mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwashukuru wafanyabiashara hao, waliotoa msaada huo. Alisema hayo ni mapambano ya wote na sio ya kuiachia serikali pekee.

“Tunashukuru wafanyabiashara wazalendo wa ngazi zote kwa kuona jambo hili sio tu la serikali, bali la wote na tunaishukuru serikali chini ya Waziri Mkuu aliyeteuliwa na Rais John Magufuli kushughulikia jambo hili, tushirikiane kupambana na corona,” alisema Makonda.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/8dcf2c71941eca1cefdabb44047da449.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi