loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kupanga foleni mwendo kasi kuwe endelevu

ABIRIA wa mabasi ya ‘mwendo kasi’ wanapanga foleni kupanda mabasi hayo! Huu ni uamuzi uliofikiwa na mamlaka zinazohusika katika kukabili ugonjwa wa corona nchini.

Zimeamua abiria kupanga foleni ili waweze kupanda magari hayo katika njia isiyohatarisha afya ya watumiaji kama ilivyokuwa awali. Katika kituo cha Kimara Mwisho, jicho limeshuhudia abiria wakiwa kwenye mstari.

Anayefika wa kwanza ndiye anaondoka wa kwanza kupanda mabasi hayo yanayokwenda Gerezani, Morocco na Kivukoni. Basi likifika, abiria wanaongozwa kuingia na ikifika idadi inayostahili, mstari unakatwa.

Kabla ya kuingia kwenye mabasi, abiria lazima wanawe na kupaka vitakasa mikono.

Tangu awali, watumiaji wa usafiri wa mwendo kasi walitamani utaratibu huu mpya wa kistaarabu utumike katika vituo vyote vya mwendo kasi.

Lakini haikuwa hivyo. Ingawa utaratibu umeanzishwa ikiwa ni hatua ya kukabili maambukizi ya ugonjwa wa corona, watu wengi wamepongeza kwa uamuzi huo.

Binafsi, nimekuwa miongoni waliostaajabu, kufurahi na kupongeza utaratibu huu baada ya kuona abiria wa mabasi ya mwendo kasi wakipanga foleni kupanda.

Kawaida, utaratibu wa kupanga foleni umezoeleka kwa mabasi ya mwendo kasi yanayofanya safari yakiunganisha abiria kutoka na kwenda Mbezi na kituo kikubwa cha mabasi hayo cha Kimara Mwisho.

Lakini kwa mabasi ya kutoka kwenye vituo vikubwa kama vile Kimara Mwisho kwenda Kivukoni, Gerezani na Morocco, hapakuwa na utaratibu wowote wa kuingia ndani ya mabasi zaidi ya abiria kupigania.

Imezoeleka kuona abiria wakivamia mabasi kwa kusukumana huku wasio na nguvu wakibaki bila kufahamu hatma ya safari.

Kwa ufupi ni kwamba, mwenye nguvu ndiye aliyekuwa na uhakika wa kusafiri bila kujali amefika muda gani.

Kama nilivyowahi kuandika kuhusu usafiri huu kupitia safu hii, ni ukweli usiopingika kwamba kupanda mabasi haya kulihitaji kifua na kuweka kando ustaarabu.

Asiyemudu mabavu angeweza kujikuta kituoni muda mrefu huku wenye nguvu wakipambana na kumuacha.

Wakati wa purukushani, wapo waliojeruhiwa na wengine kuibiwa vitu kama simu na fedha. Kero hizi ikiwamo msongamano kupita kiasi ndani ya mabasi, ziligeuka wimbo usioisha midomoni mwa abiria, vyombo vya habari na wadau wengine zikiwamo taasisi zinazotetea abiria bila hatua kuchukuliwa.

Nilitamani kuona kero hizi zikifanyiwa kazi na kubaki kuwa historia ili mantiki ya kuanzishwa kwa mabasi haya ibaki kuwa ni ukombozi kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Ilisikitisha ziliposikika sauti za baadhi ya abiria waliotamani daladala za kawaida zirejeshwe na kusahau kero zaidi hususani foleni barabarani zilizotokana na mabasi hayo katika barabara ya Morogoro.

Kero za mwendo kasi zikawafanya abiria wasahau kuwa daladala za kawaida zilitumia takribani kati ya saa mbili na tatu kwa safari ya kutoka Kimara kwenda Kivukoni wakati mwendo kasi ya kawaida yanatumia dakika 45 na ya express ni dakika 45 .

Wakazi wa Kimara, Mbezi na Kibamba na maeneo mengine yanakopita mabasi ya mwendo kasi, wanakumbuka walivyotumia fedha nyingi kwa usafiri wa kuunga unga daladala wakati wa kwenda na kurudi kwenye shughuli zao.

Hata hivyo hao waliotamani daladala za kawaida zirejeshwe si wa kubeza wala kuwashangaa kwa kuwa kero za mwendo kasi ikiwamo kugombania mabasi ndizo zilisababisha hayo yote.

Abiria wengi waliweka bayana kwamba mwendo kasi ni hatarishi kwa afya na maisha yao. Kilio hiki kiligeuka wimbo usio na mwisho.

Ndiyo maana baada ya kushuhudia ustaarabu huu mpya, nimebaki kustaajabu. Nikabaki pia kujisemea kwamba ‘kumbe mambo haya yanawezekana’.

Kumbe mamlaka zikatoa amri na zikasimamia utaratibu wa foleni ukafanyika kwenye vituo vyote! Wakati jicho langu likiendelea kupongeza mamlaka kwa mkakati huu wa kudhibiti maambukizi ya corona, nashauri ustaarabu huu wa kupanga foleni kwenye mabasi ya mwendo kasi uwe endelevu hata baada ya nchi kufanikiwa kudhibiti ugonjwa huu.

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi