loader
Dstv Habarileo  Mobile
Msomi anayetumia mavazi 'kupiga pesa'

Msomi anayetumia mavazi 'kupiga pesa'

TASNIA ya ubunifu wa mavazi inazidi kukua kwa kasi nchini huku wanamitindo vijana wakizidi kuchipukia na kuzitumia vema fursa zilizopo kwenye soko hilo.

Huku wakiwemo wabunifu mahiri ambao wamefanya vema ndani na nje ya nchi kama akina Mustafa Hassanali, Ally Remtullah, Ailinda Sawe na wengineo wengi katika tasnia hii, kwa sasa kundi la vijana linalokuja lina mengi ya kuiongezea tasnia.

Mwanadada Winnie Nzunda ni kati ya wabunifu wa mavazi vijana wanaokuja kwa kasi huku akiwa amejikita katika mavazi ya wanawake na wanaume kupitia lebo yake ya kazi ya WStyleloft.

Mhitimu huyo wa Chuo Kikuu cha Hertfordshire na Cardiff nchini Uingereza mwaka 2015, aliziona fursa nyingi katika tasnia ya ubunifu wa mavazi akiwa nchini humo ambapo alipania pindi tu akirejea nchini kuzifanyia kazi.

Amebainisha kuwa wapo wazungu wanaopenda zaidi kuvaa mavazi yaliyobuniwa na wabunifu wa mavazi wa nchini mwao hasa ikiwa ni ishara ya kuenzi na kuendeleza wabunifu wao wa mavazi.

Aliziona fursa hizo kuwa akirejea nchini atakuwa akiwabunia watu ambao ni maarufu na hata wasiokuwa na umaarufu kwa lengo kuendeleza utamaduni wa watu kuvalia mavazi ya wabunifu wa nyumbani yawe yenye nakshi za kiafrika hata yenye muonekano wa kimagharibi.

Amerejea nchini na kuanza kubuni mavazi. Aliporejea nchini alichagua kuwahusisha watu maarufu kwenye mavazi yake hayo, ikiwa ni mbinu mojawapo ya kuwachukulia kama mfano kwa wengine kuendelea kupenda kuvalia mavazi ya wabunifu wa ndani ya nchi.

Alianza kubuni mavazi ya mwanamuziki wa kizazi kipya, Mimi Mars na mtangazaji wa luninga katika kituo cha televisheni cha Clouds, Perfect Crispin ambao wote ni vijana.

”Najua kipindi ambacho ninamaliza chuo na kurejea nyumbani ni kipindi ambacho kulikuwa na dhana ya Tanzania ya Viwanda, hapo karibia kila mtu alikuwa na wajibu wa kubuni shughuli ambayo itazalishwa na malighafi za kitanzania na kuwaendeleza wazalishaji hao. Hapo niliona msukumo zaidi ndani yangu wa kuiendeleza tasnia ya mavazi hasa kwa kuangalia namna gani ninaweza kuingia na kuiendeleza huku nikiwa natambua uwepo wa magwiji kwenye tasnia hii”anasema.

Anasema kwa kuwatumia wawili hao haikuwa kazi ngumu kwa kuwa ni watu anaofahamiana nao na ni kundi la vijana lenye ushawishi mkubwa katika mitandao ya kijamii.

Anasema wakati huo alikuwa tayari ameshaanza maandalizi ya shughuli hizo za ubunifu hasa kwa kununua vifaa vya kushonea, kuandaa mahala pa kufanyia shughuli hizo na kutafuta wasaidizi.

Anasema alianza na gauni la Mimi Mars ambalo lilikuwa gauni refu jekundu lenye nakshi za kimagharibi kabla ya kuanza kumbunia mavazi mengine yenye nakshi za kiafrika.

Anasema baada ya kulibuni na kutengenezwa kwa gauni hilo, kisha kutangazwa katika mitandao ya kijamii liliwavutia watu wengi kwa ubunifu na hata mwonekano wa msanii huyo kupitia vazi lake hilo.

Anaongeza kuwa haraka alirejea tena kwenye ubunifu wa mavazi mengine ya Mimi Mars ambayo yalikuwa ya mitindo mbalimbali ambayo yote yalianza kumfungulia milango ya kazi.

Anasema kuwa hapo ndipo ndoto yake ya kushiriki katika kuongeza thamani ya mavazi ya wabunifu wa mavazi wa kitanzania ilizidi kupamba moto.

Anasema,”Najua nilipoona watu wengine wanampigia simu Mimi Mars wakitaka kufahamu zaidi mahala alipobuniwa mavazi yake, ndipo na mimi nikaona kuwa hakika soko lipo na kikubwa ni kuzingatia weledi wa kazi hii.”

Anasema alianza kubuni mavazi ya kiume huku akimtumia mtangazaji Perfect Crispin ambapo nako alibainisha mwamko mkubwa. Hapo mwanadada huyo alipoanza kujikita miguu miwili katika kazi hiyo huku akianza kuaminiwa na kupatiwa kazi nyingi za kibunifu.

Anasema aliamua bei ya mavazi yake iwe ya kawaida kabisa ambapo anaanzia 30,000/- hadi 100,000/- hasa kwa mavazi ya wanawake.

Anasema amekuwa akipata oda ya kubuni mavazi na amekuwa akitumia chini ya muda wa wiki moja kukamilisha kazi za wateja wake.

Aalikwa na Ally Remtullah

Akiwa anaendelea na kazi yake siku moja alipigiwa simu na mbunifu mkubwa wa mavazi nchini, Ally Remtullah ambaye alimwalika ashiriki katika uzinduzi wa duka lake la mavazi na kuuza bidhaa zake.

Duka hilo la Remtullah kwa hapa nchini ni kati ya maduka makubwa yanayouza bidhaa zilizobuniwa na wabunifu wa mavazi wa ndani ya nchi, ambapo hutoa miezi mitatu kwa wabunifu wa mavazi aliowachagua kuuza bidhaa zao dukani hapo.

Hivyo kwa Winnie kupata mwaliko huo aliona kwake ni kuthaminiwa, kwa kuwa kwake Ally Remtullah ni kati ya wabunifu wa mavazi anaowakubali na kuziheshimu kazi zao hivyo kuuza mavazi yake katika duka hilo ni nafasi ya kujipanga na kufanya kazi nzuri zaidi.

Anasema alianza kutengeneza nguo kali zaidi ambazo zitaoneshwa na kuuzwa katika duka hilo la Ally Remtullah, hivyo alitumia wiki nzima kuandaa mavazi mbalimbali.

“Siku ilipofika niliwasilisha mavazi yangu katika duka la Ally jijini Dar es Salaam na kuoneshwa mahala pa kuweka mavazi hayo, hakika kwangu ilikuwa ni furaha hasa kutokana na siku hiyo kukutana na wabunifu wakubwa kama akina Ailinda Sawe, Mgese Mimi na wengineo kadhaa.

Ilikuwa pia ni wakati wangu kuona wengine wanavyofanya kazi kwa kuwa hii fani huwa si suala la kubuni tu ila hata namna ya ufungaji wa mavazi yenyewe, kujinadi na mengineo mengi,” anasema Winnie.

Anasema kwake ilikuwa ni fursa kubwa zaidi ya kujitangaza hasa baada ya kutembelewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza aliyekuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa duka hilo.

Anasema waziri alipokuwa akitembea na kufika kwenye eneo alipokuwa ameweka mavazi yake, Waziri alisimama na kuanza kumpatia nasaha za kazi za kibunifu ambapo kwake anasema kuwa ushauri huo ulimfungua macho zaidi.

Anasema,“aliniambia kuwa ni lazima nijitangaze katika mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari kwa kuwa kazi ya ubunifu inahitaji zaidi kujitangaza”.

Anaongeza kwa kipindi akiwa anauza mavazi yake katika duka hilo aliimarisha zaidi mawasiliano katika mitandao yake ya kijamii ambayo ni Instagram na Facebook amejitangaza kwa kutumia jina la WStyleloft.

Anasema wapo wateja wengi ambao wamekuwa wakiwasiliana naye kupitia mitandao hiyo huku kwa sasa akipata oda kadhaa kupitia mitandao hiyo ya kijamii.

Mwito kwa vijana Winnie anawataka vijana kuwekeza zaidi katika ujasiriamali hasa kwa kuongeza thamani aina za biashara ambazo zimekuwa zikichukuliwa kuwa ni biashara za kawaida.

Anasema kuwa kuongeza thamani katika biashara ni kati ya mambo muhimu ambayo yanaweza kumtajirisha mjasiriamali na kuwa hapa nchini zipo shughuli nyingi ambazo zinaweza kumpatia kijana utajiri.

Anasema wapo vijana ambao wanajipatia kipato kizuri kutokana na kuwekeza kwenye shughuli za kiujasiriamali ambazo awali zilikuwa zikionekana ni za kawaida.

Anatolea mfano wa shughuli kama upigaji wa picha ambazo kwa miaka mingi iliyopita zimekuwa zikichukuliwa ni kama shughuli za kawaida tu, ila kwa sasa vijana wanajipatia mapato makubwa kupitia shughuli hizo.

Anavyoikabili corona Anasema kuwa kutokana na kufanya kazi za wateja wengi wakiwamo wasanii amejikuta akiwa karibu na watu wengi wenye majina makubwa hasa vijana katika tasnia ya sanaa.

Anasema aliamua kutumia nafasi hiyo kuandaa kampeni ya kukabiliana na corona kwa kutumia wasanii akiwemo Snura Mushi, Nurdin Bakari (Shetta), Doreen Noni na wengine kadhaa.

Katika kufanikisha hilo, anashirikiana na wasanii hao ambao hurekodi video fupifupi zenye ujumbe wa jinsi ya kukabiliana na corona na kisha kusisambaza kwenye mitandao ya kijamii kama njia ya kuwahamasisha jamii kuchukua tahadhari. Winnie ameolewa na Michael Mlingwa ambaye ni mtengeneza dokumentari mkubwa nchini wamejaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume.

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi