loader
Ashauri serikali kutoa vibali sukari kuagizwa nje

Ashauri serikali kutoa vibali sukari kuagizwa nje

WAZIRI Kivuli wa Wizara ya Viwanda na Biashara, David Silinde ambaye pia ni Mbunge wa Momba mkoani Songwe, ameishauri serikali kutoa vibali vya kuagiza sukari nje kwa viwanda vya sukari nchini ili kutosheleza upungufu wa sukari ulioanza kujitokeza nchini.

Silinde alisema hayo jana katika mahojiano yake na Televisheni mtandao ya SAVP, akieleza kuwa upungufu wa sukari ulipo kwa sasa nchini unatokana na mvua zinazoendelea kunyesha ambazo zimeathiri kilimo cha miwa.

Alisema mashamba ya miwa nchini yamejaa maji kitendo kinachowakwamisha wakulima kuendelea na shughuli za kilimo cha miwa na hivyo kusababisha upungufu wa malighafi hiyo muhimu katika uzalishaji wa sukari.

Alisema kwa kuwa serikali ndio inayotoa vibali kwa wamiliki wa viwanda vya sukari kuagiza sukari kutoka nje ya nchi, huu ni muda mwafaka wa hilo kufanyika kwa kuwa hali ikiendelea kuwa kama ilivyo sasa bei ya sukari itazidi kupanda.

“Kwa sasa gunia moja la kilo 50 la sukari linauzwa hadi shilingi 70,000 wakati bei awali ilikuwa shilingi 58,000 pia kwa sasa sukari kilo moja inauzwa kwa shilingi 3,000 kutoka shilingi 2,400 hii inaashiria kuwa kama uagizwaji wa sukari kutoka nje usipofanyika bei inaweza hata kuzidi kupanda,” alieleza Silinde.

Aliongeza, “tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo wafanyabiashara walikuwa wakiagiza sukari nje ya nchi wenyewe kwa sasa inapaswa kuwepo kwa vibali maalumu vinavyotolewa na serikali ambapo waagizaji ni wenye viwanda vya sukari hivyo ninashauri itoe vibali kipindi hiki sukari kutoka nje iingie nchini kukidhi uhaba wa soko.”

Kuhusu ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya corona unaweza kuathiri uagizwaji huo wa sukari, alibainisha kuwa usafirishwaji wa mizigo haujakatazwa ni muda mwafaka kwa nchi kuagiza sukari “Najua kwa nchi kama Brazil ambako ndio tunaagiza sukari kama nako corona ikianza kuathiri uzalishaji ina maana hata bei itakuwa juu zaidi hivyo ni muda mzuri kuagiza sasa hivi,” alisema.

Pia ameishauri serikali kutoa ruzuku kwa viwanda vya sukari ili vizalishe na kuuza sukari kwa bei rahsi zaidi ambayo mwananchi wa kawaida anaweza kuinunua. Alisema ruzuku hizo zinaweza kutolewa hata kwenye bidhaa nyingine ili kuhamasisha uzalishaji na kunusuru ukosefu wa bidhaa nchini.

Kuhusu kupanda kwa bei za vitakasa mikono, barakoa pamoja na bidhaa nyingine muhimu katika kukabiliana na corona, alisema hiyo inatokana na kuongezeka kwa uhitaji wa soko huku uzalishaji ukisuasua, ambako aliwataka wazalishaji kuzalisha kwa wingi huku mamlaka husika kuendelea kukabiliana na ongezeko holela la bei.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/da887d72aed66ab85a56532f6f1a9217.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi