loader
JPM akaribisha maombi ya kitaifa kutokomeza corona

JPM akaribisha maombi ya kitaifa kutokomeza corona

Rais John Magufuli amewaomba Watanzania kutumia siku tatu kuanzia Aprili 17-19 mwaka huu, kumuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na corona. Alisema hayo jana katika ujumbe wake kwa Watanzania, alioutoa kupitia mtandao wa Twitter.

“Ndugu zangu Watanzania, kutokana na ugonjwa wa corona, nawaomba tutumie siku tatu za kuanzia tarehe 17-19 Aprili 2020 (Ijumaa, Jumamosi na Jumapili) kumuomba Mwenyezi Mungu aliye muweza wa yote atuepushe na janga na ugonjwa huu. Tusali kwa kila mmoja kwa imani yake, atatusikia” alisema Rais Magufuli.

Ushauri wa Makonda Vicky Kimaro anaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameshauri watu wa mikoa mingine, kutofanya safari za kuja mkoani Dar es Salaam, kwa sababu mkoa huo hali yake ni tete, kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosabbishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa juzi na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, idadi ya wagonjwa ilikuwa 88, na 11 wamepona, huku Dar es Salkaam ikiwa na wagonjwa wengi, wagonjwa 20. Jana kulikuwa na ongezeko la wagonjwa sita wote kutoka Zanzibar.

Makonda amepiga marufuku kwa watu wa mikoani, kuja jijini Dar es Salaam kipindi hiki kwa lengo la kutembea, kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha yao.

“Marufuku wa mikoani kuja Dar es Salaam kutembea sijui mjomba au shangazi…baki huko huko hali ya Dar es Salaam ni tete imebadilika. Acheni wakazi wa Dar wapambane na janga hili la corona wenyewe; na wa Dar sio mtoke kwenda mkoani, bakini hapa hapa tupambane…msipeleke huko kwa wengine,” alisema Makonda.

Alisema ni vema kuchukua tahadhari na kinga kuliko mauti, kwani kwa hali ilivyo sasa, mambukizi ya Dar es Salaam hayaridhishi, hali ni mbaya, ni vema kujilinda na kuwalinda uwapendao ili kulishinda janga hilo. Makonda alitoa kauli hiyo jana kwenye Viwanja vya Karimjee wakati akipokea mashine 25 za kutakasa mwili na barakoa 75,000 kutoka kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Makonda alisema alisema hali ilivyo kwa sasa kwa Jiji la Dar es Salaam, inatia hofu kutokana na maambukizi kuongezeka. Aidha, Makonda alibainisha kuwa kuna vituo 60 vya watoto yatima, ambavyo vinahitaji msaada wa chakula katika kipindi hiki cha janga la corona. Aliwataka wadau kujitolea kupeleka misaada katika vituo hivyo.

Pia alipiga marufuku kwa wananchi, kuendelea kuwapa fedha ombaomba wa barabarani, huku akiwataka kwa sasa kuondoka maeneo hayo ya barabarani, kutokana na hali ni mbaya iliyopo sasa ili wasije kuupata ugonjwa. Awali, Rostam alitekeleza ahadi yake ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 baada ya jana kukabidhi kwa Makonda mashine 25 za vitakasa mwili pamoja na barakoa 75,000.

Vifaa hivyo zitasambazwa katika maeneo yote ya msongamano ikiwemo stendi za mabasi na hospitali. Mashine hizo zinazotoa mvuke ni maalumu kwa ajili ya kuulia virusi, ikiwa ni kupambana na janga la corona.

Kila abiria atakayepanda, atalazimika kutumia kitakasa mkono kabla ya kuingia kwenye daladala. Mfanyabiashara huyo hivi karibuni jijini Dodoma aliahidi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa vifaa vyenye thamani ya Sh bilioni moja kwa Jiji la Dar es Salaam ili kukabiliana na corona, ambao uliingia nchini Machi 16, mwaka huu. Tayari ugonjwa huo umeua watu wanne.

Rostam anayemiliki Kampuni ya Taifa Gas ambayo ilitoa Sh milioni 100 kwa Waziri Mkuu, na nyingine kadhaa, alikabidhi vifaa hivyo jana kwenye Viwanja wa Karimjee jijini Dar es Salaam huku akiwataka wafanyabiashara wengine, kujitokeza ili kusaidia serikali katika mapambano hayo ya corona. Aidha, Rostam alimpongeza Rais John Magufuli kwa kuwaongoza Watanzania kwa hekima na busara na kuwaepusha na taharuki, kama ilivyotokea katika mataifa mengine.

Pia, alimpongeza Waziri Mkuu, Majaliwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa namna ambavyo wanavyoshiriki katika kukabiliana na virusi vya corona. Makonda alisema kutokana na hali hiyo, kila abiria atakayeingia kwenye dalaldala na kwenye masoko, ni lazima kutumia vitakasa mkono ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo. Alivitaka vyombo vyote vya usafiri, kuzingatia taratibu na kanuni zinazotolewa na Wizara ya Afya.

Aliwataka madereva na makondakta, kuwaripoti abiria wakorofi ambao watakaidi kutumia vitakasa mkono kabla ya kupanda gari. Aliwataka kutumia vifaa hivyo, kwa manufaa ya umma na sio kupeleka kwenye matumizi binafsi. Alisema Dar es Salaam ina vituo 25 vikiwemo hospitali, kwa lengo la kupunguza mizunguko ya watu wanaohisi kuumwa corona kwenda maduka ya dawa au vituo vya afya.

Alitaka wanaohisi kuumwa corona, wapige simu na timu ya waratibu wa afya, watawafuata walipo, kwani tayari Rais ametoa magari 25, yakiwamo maalumu ya wagonjwa. Mganga Mkuu wa Mkoa, Rashid Mfaume alisema vita dhidi ya corona ni kama vita nyingine na askari waliopo mstari wa mbele ni madaktari ambao wapo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi. Aliwataka wadau zaidi, kujitokeza kusaidia vifaa na pia kuwasisitiza wananchi kufuata maelekezo.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Elisha Osati alitaka serikali kupiga marufuku kwenye hospitali zote hakuna mtu yeyote kuingia bila ya kuvaa barakoa na kunawa mikono mlangoni, kwani hospitali ni sehemu ambayo ina maambukizi mengi. Mwongozo mpya kwa wabunge kujikinga corona Anna Anyimike, anaripoti kutoka Dodoma kuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ametoa Mwongozo mpya kwa wabunge, kujikinga ugonjwa wa corona.

Akisoma Waraka wa Mwongozo huo jana, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema wabunge wanatakiwa kuchukua tahadhari zaidi, ikiwa ni pamoja na kupunguza safari za kwenda kwenye miji iliyoathirika zaidi ya Dar es Salaam na Zanzibar na pia kupunguza mizunguko ndani ya jiji la Dodoma Dk Tulia alisema mtindo ambao wabunge wanatakiwa kwenda nao ni kutoka nyumbani kwenda Bungeni na kurudi nyumbani.

“Lakini hata mnapokuwa hapa Dodoma, ni vema mkajilinda na safari za hapa na pale ndani ya jiji. Na hata katika ukumbi wa Bunge msitembee tembee. Hata mahitaji ya nyumbani, mnatakiwa kununua walau kwa wiki mara moja, siyo kila siku”ulisema waraka huo.

Pia, wametakiwa kujiepusha na kupunguza kufuatilia taarifa za kuogofya kuhusu ugonjwa huo, kwani kwa kufanya hivyo, hofu inaongeza msongo wa mawazo na kupunguza kinga za mwili.

Wabunge pia wametakiwa kuzingatia mlo kamili kwa kila siku na kunywa maji kwa wingi, huku wakifanya mazoezi mepesi. Lakini, wataalamu wanasema kuwa wenye umri mkubwa na wenye magonjwa mengine, ndiyo wako kwenye hatari zaidi.

Hata hivyo, haina maana kuwa wanaotajwa katika makundi hayo, ndiyo wahusika au waathirika, bali mtu yeyote anaweza kupata ugonjwa huo bila kujali yupo katika kundi gani, hivyo wanatakiwa kuchukua tahadhari zaidi ili Bunge limalizike salama na waweza kutimiza wajibu wao.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/43a606f41f7285c217068a5bcab2ab3b.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi