loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mabibo kutengeneza vitakasa mkono

WAKATI serikali inapambana na janga la corona nchini, imebainika kwamba bibo la korosho likichakatwa kitaalamu lina ethanol ya kutosha kutumika kama malighafi ya kutengenezea vitakasa mikono (hand sanitizers).

Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa TARI Naliendele, Dk Fortunas Kapinga wakati akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, kuhusu hatua waliyofikia katika utekelezaji wa agizo la Rais Dk John Magufuli, alilolitoa mwaka jana akiwataka watafiti zaidi bibo la korosho.

Dk Kapinga alisema kazi waliyotumwa na Rais Magufuli imeshafikia ukingoni na kwamba katika utafiti walioufanya wamebaini bibo linatoa asilimia 74 ya ethanol ambayo inaweza kabisa kuwa malighafi ya kutengeneza vitakasa mikono.

Alisema katika upatikanaji wa asilimia 74 ya ethanol wametumia kilo moja ya mabibo ambayo ilitoa mills 210. Alisema kwa kiwango hicho, kama watanzania watazalisha tani 315,000 za mabibo ya korosho taifa linaweza kutengeneza lita milioni 400 hadi 500 ya ethanol ya asilimia 74 ikiwa ni malighafi ya kutengeneza vitakasa mikono.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Kilimo, korosho ghafi nchini zilizofika katika maghala zilipanda kutoka tani 155,245 kwa mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani 232,527.55 kwa msimu wa mwaka 2019/2020.

Aidha kuhusiana na vitakasa mikono katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe alisema kwa sasa uwezo uliopo wa kupatikana kwa kimiminika cha ‘ethanol’ kinachotumika kuzalisha vitakasa mikono vinavyotumiwa na wananchi ni asilimia 45 kiwango ambacho kinasaidia katika kuzalisha vitakasa mikono vilivyopo kwa sasa.

Kwa mujibu wa Dk Kapinga, pamoja na kuweza kutoa ethanol ambacho ni kiungo kikubwa cha kutengeneza vitakasa mikono, bibo hilo pia linaweza kutengeneza aina mbalimbali za pombe ikiwamo mvinyo na pia juisi.

“Kwa sasa sisi tumekamilisha utafiti wetu tumejua hesabu zinazotakiwa kufanywa. Hatujautoa rasmi utafiti huu kwa sababu tumepeleka maabara ya Mkemia Mkuu wa serikali kwa uthibitisho huru wa kazi tuliyofanya. Baada ya kukamilisha tunaweza kusema kwa yakini nini cha kufanywa,” alisema Dk Kapinga.

Akifafanua zaidi alisema kwamba kazi kubwa ya mkemia ni kuangalia uwiano ambao umefanyiwa kazi na taasisi yake ili kuuthibitisha . Alisema kinachostahili kufanywa kwa sasa ni kuongezwa kwa wigo wa kilimo cha korosho na pia wakulima kupewa maarifa ya kuhifadhi mabibo ili yaweze kuchakatwa na kupatikana kwa ethanol na bidhaa nyingine.

Aidha alishauri Shirika la Kuhudumia viwanda vidogo kuanza kuangalia namna bora ya kuwezesha mitambo wakulima ya kuzalisha ethanol ili waweze kuuza kwa viwanda vya kati na vikubwa vinavyobadili ethanol kuwa bidhaa mbalimbali. Nchini Tanzania kwa sasa kuna viwanda tisa vyenye leseni ya kutengeneza vitakasa mikono lakini hadi Machi,viwili ndivyo vinafanyakazi sasa .

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwanda wa Wizara hiyo, Leo Lyayuka, alisema Kiwanda cha Sukari cha Kilombero ambacho huzalisha ethanol wakati mwa utengenezaji wa sukari kimesitisha uzalishaji wa sukari kuanzia mwezi Februari hadi Juni hivyo hakitengenezi kimininika hicho kwa sasa. Lyayuka alisema katika kipindi hicho ambacho kiwanda hakifanyi uzalishaji wa sukari pia husababisha kukosekana kwa malighafi ya molasi ambayo ni mabaki ya sukari inayotumika kuzalisha kimiminika cha ‘ethanol’ kinachotumika katika kuzalisha vitakasa mikono.

Hata hivyo alisema kiwanda cha Kilimanjaro Biochem Ltd ambao hutumia molasi kwa ajili ya kuzalisha ‘ethanol’ kwa sasa wana akiba ya kutosha ya molasi.

“Asilimia 60 ya vitakakasa mikono ni ‘alcohol’, kwa hiyo tulikuwa tunaangalia kama tunaweza kuzalisha ‘alcohol’ hiyo kwa wingi hapa nchini,”alisema Lyayuka.

Kutokana na utafiti wa TARI ni dhahiri katika miaka michache ijayo, Tanzania inaweza kuwa na upande mwingine wa uzalishaji wa ethanol kwa kutumia mabibo na hivyo kuongeza malighafi ya vitakasa mkono na bidhaa nyingine za pombe.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi