loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanawake unene uliopitiliza si sifa

FEBRUARI 4 kila mwaka dunia huadhimisha siku ya saratani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) katika ujumbe wa mwaka huu limesema Afrika imeathirika zaidi na saratani ya mlango wa kizazi kuliko mabara mengine.

Mkurugenzi wa kanda ya Afrika wa WHO, Dk Matshidiso Moeti alisema kukithiri kwa ugonjwa kunatarajiwa kuongezeka kutoka wagonjwa milioni moja mwaka 2018 hadi zaidi ya wagonjwa milioni mbili ifikapo mwaka 2040.

Saratani iliyokithiri ni ya mlango wa kizazi, matiti, ini na ya tezi dume ambazo kwa pamoja zimesababisha moja ya tatu ya vifo vyote vya saratani Afrika mwaka 2018.

Takwimu za kiulimwengu zinaonesha katika kila watu watano mmoja atapatikana na saratani kabla ya kufikia umri wa miaka 75.

Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza (TANCDA) kupitia kitabu chake cha ‘Mtindo wa Maisha na Magonjwa Yasiyoambukiza’ linaelezea saratani kwa ujumla kwa kuainisha vitu vinavyochangia, dalili na namna ya kupunguza uwezekano wa kupata saratani.

Linaelezea saratani kwamba hutokea wakati sehemu ya mwili inapokua na kuongezeka bila utaratibu na kusababisha uvimbe na kwamba magonjwa mengi ya saratani hutibika yakigundulika mapema.

Kwa kawaida saratani huanza taratibu na huchukua muda kuonesha dalili zozote. Pia dalili za awali haziambatani na maumivu hivyo kusababisha wagonjwa wengi kuchelewa kutafuta matibabu.

Asilimia 60 ya magonjwa yote ya saratani yanahusishwa na mtindo wa maisha ambao vipengele vyake ni ulaji, ushughulishaji wa mwili na matumizi ya pombe na tumbaku. Virusi vya bakteria, madini mazito, mionzi na sumu kadhaa pia huchangia.

Vyakula huchangia kwa kiasi kikubwa saratani ya kinywa na koo, matiti, tezi ya kiume, utumbo mpana, mapafu, tumbo, ini, kongosho na kizazi.

Ulaji unaoweza kuchangia ni pamoja na ulaji wa nyama nyekundu kupita kiasi, nyama zilizosindikwa, vyakula vilivyokuzwa kwa kemikali nyingi na vyakula vyenye mafuta mengi vinavyosababisha uzito mwingi.

Uzito uliozidi ni jambo lingine linalochangia saratani. Humweka mtu kwenye hatari ya kupata magonjwa mengi sugu kama vile kisukari, msukumo mkubwa wa damu, magonjwa ya moyo, figo na saratani za matiti, kongosho na kizazi.

Utaratibu mzuri wa kula husaidia kupunguza uzito au kuzuia ongezeko kubwa la mwili. Nyama nyekundu ni muhimu kwa binadamu lakini ulaji wa kiasi kikubwa huongeza uwezekano wa kupata saratani ya utumbo mkubwa.

Kula hadi nusu kilo kwa wiki haiongezi uwezekano wa kupata saratani lakini kila gramu 50 zinazoongezeka huongeza uwezekano wa kupata saratani kwa asilimia 15.

Nyama zilizosindikwa pamoja na zilizohifadhiwa kwa kuongezwa chumvi, mafuta, kemikali au kukaushwa kwa moshi (mfano nyama za kopo, soseji na becon) zinaongeza sana uwezekano wa kupata saratani.

Hakuna kiasi chochote cha nyama iliyosindikwa kinachoweza kutumika bila kuongeza uwezekano wa kupata saratani. Matumizi ya pombe na tumbaku huchangia sana ongezeko la saratani za koo na mapafu.

Pombe inaongeza sana uwezekano wa kupata saratani hasa zile za koo, kinywa, ini na matiti. Wataalamu wa magonjwa yasiyoambukiza wanaainisha wanasema magonjwa mengi ya saratani hutibika yakigundulika mapema.

Hivyo wanashauri mtu anapoona dalili zifuatazo, wamuone mapema mhudumu wa afya. Dalili za awali Dalili hizo ni pamoja na kukosa hamu ya kula, kupungua uzito bila sababu, uchovu bila ya kufanya kazi, uvimbe wa zaidi ya wiki tatu shingoni, kwapani, tumboni, kwenye ngozi au matiti.

Nyingine ni kubadilika kwa kawaida ya kupata choo kwa maana ya kufunga choo, kutokwa na ute, maji maji au usaha ukeni, kutokwa na damu kwenye choo, mkojo, makohozi au pua.

Kwa wanawake, kutokwa na damu ukeni baada ya tendo la ndoa, baada ya kukoma mzunguko wa hedhi au nje ya mzunguko.

Dalili nyingine ni shida au maumivu wakati wa kumeza chakula au vinywaji, kukohoa au sauti ya kukwaruza kwa zaidi ya wiki tatu, matiti kubadilika maumbile, uvimbe, ngozi au kutoa maji maji. Pia kwenda haja ndogo nyingi zaidi ya kawaida au kutoka kwa shida ni dalili nyingine ya magonjwa ya saratani.

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi