loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

TV ‘zilishe’ watoto maadili mema

NAUNGANA na wadau wa elimu, afya na watoto kuunga mkono uamuzi wa serikali wa kuendelea kufungwa kwa shule na vyuo vyote nchini kama ilivyotangazwa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Ni uamuzi sahihi na wenye busara ikizingatiwa ongezeko la virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (covid- 19). Watoto ni kundi lililo hatarini hivyo wangeendelea kwenda shule kungeweza kuongeza maambukizi.

Kama ambavyo wadau wengi wamekuwa wakishauri, wazazi na walezi hawana budi kuunga mkono nia hii njema ya serikali kwa kuhakikisha watoto wanabaki nyumbani muda wote.

Ni hatari kuendelea kuona watoto wanaachwa kuzurura mitaani kama inavyoonekana huku wengine wakishuhudiwa kwenye vyombo vya usafiri wa umma jambo ni hatari kwa afya zao. Kama ni safari, basi ziwe ni zile za lazima mathalani, kwenda hospitali.

Naamini kadri siku zinavyokwenda, jamii itaendelea kuelewa kupitia elimu inayotolewa na serikali na wadau mbalimbali.

Sambamba na jamii kutakiwa kuzingatia usalama wa watoto wawapo nyumbani, ni vyema pia wasaidiwe wasisahau masomo badala yake wakapandikizwa mafunzo ya kuwaharibu kiakili na kimaadili.

Naungana na wadau mbalimbali ikiwamo Umoja wa Wamiliki na Mameneja wa Taasisi Binafsi za Elimu Tanzania (Tamongsco) iliyoiomba serikali ielekeze televisheni na redio zirushe vipindi vya mafunzo kuwezesha wanafunzi wote kujifunza wawapo nyumbani.

Akizungumza hivi karibuni, Mwenyekiti wa Tamongsco, Leonard Mao alisema itakuwa jambo jema kwa watoto wanapofungua televisheni wakutane na masomo.

Anasisitiza watoto wasikae kuangalia katuni pekee au sinema zisizo na maadili, bali vipindi vya televisheni na redio viwe vingi visaidie kuwafundisha kama inavyofanyika darasani.

Nakubaliana na ushauri wa mwenyekiti huyo wa Tamongsco kwa wazazi na walezi akiwataka wadhibiti watoto wao kuangalia picha zisizofundisha. Kipindi hiki kinahitaji ushirikiano na kujitoa kwa dhati kwa wadau mbalimbali.

Vituo vya televisheni na redio havina budi kila kimoja kwa wakati wake kukaa na kuangalia namna bora ya kuwezesha watoto kupata mafunzo.

Wanafunzi katika shule za serikali ni waathirika zaidi ikilinganishwa na wale wa shule binafsi ambao angalau shule nyingi zinajitahidi kuwasiliana na wazazi na kutuma kazi za nyumbani zisaidie kushughulisha watoto.

Lakini hata hao wanaotumiwa kazi za nyumbani, wanapokaa nyumbani na kulazimika kuangalia vipindi vya televisheni, wasaidiwe kukutana na vipindi vizuri v inavyoendelea kuwajenga kimaadili.

Endapo kila kituo cha televisheni kitatenga muda kwa ajili ya kipindi cha watoto kujifunza, itatoa mwamko wa kujifunza badala ya kushinda wakifuatilia muziki na sinema zisizoendana na umri wao.

Ombi hili la wadau kwa serikali na wamiliki wa televisheni kwamba utengwe muda unaoendana na watoto kusoma kuanzia saa mbili asubuhi hadi mchana, ni muafaka. Kama ilivyoshauriwa, wadau kwa kushirikiana na serikali wajadiliane namna ya kuwezesha walimu watakaohusika kufundisha kupitia vyombo hivyo vya habari angalau wanafunzi ambao hawajafikiwa na mfumo wa kujisomea nyumbani pia wanufaike.

Naamini hakuna linaloshindikana. Wakati serikali ikiendelea kupambana kuhakikisha maambukizi ya virusi vya corona yanapungua kama si kudhibitiwa, juhudi ziendelee kufanyika kutafuta utaratibu wa kusaidia wanafuzi hususani walio katika madarasa ya mtihani wapate elimu wakiwa nyumbani.

Lakini pia angalizo la Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) kuhusu kuwalinda watoto dhidi ya ukatili katika kipindi hiki ambacho wanakaa nyumbani muda mrefu, pia lizingatiwe.

Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla licha ya kuimarisha mifumo ya watoto kujifunza na kuwa na maadili, vile vile iimarishe ulinzi kwa watoto dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia unaoweza kufanyika nyumbani.

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi