loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Corona yazidi kusambaa nchini

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema, sampuli zilizopimwa kati ya Aprili 18 na 20 mwaka huu, zimethibitisha kuwepo kwa wagonjwa wapya 84 wenye maambukizi ya virusi vya corona (Covid-19) nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kati ya hao, wagonjwa 16 ni waliotolewa taarifa na Waziri wa Afya wa Zanzibar jana. Kwa upande wa Tanzania Bara, idadi ya wagonjwa na mikoa wanayotoka kwenye mabano ni kama ifuatavyo: Dar es Salaam (33), Arusha (4), Mbeya (3), Kilimanjaro (3), Pwani (3), Tanga (3), Manyara (2), Tabora (1), Dodoma (3), Ruvuma (2), Morogoro (2), Lindi (1), Mara (1), Mwanza (3), Mtwara (1), Kagera (1) na Rukwa (2).

Wagonjwa wote walioripotiwa Tanzania Bara, wanaendelea vizuri, isipokuwa wagonjwa wanne wanaopatiwa huduma za wagonjwa wanaohitaji ungalizi maalumu. Taarifa hiyo ilibainisha kwamba Aprili 18, mwaka huu Waziri wa Afya Zanzibar, alitoa taarifa ya uwepo wa wagonjwa 23. Ongezeko la wagonjwa wapya, linafanya idadi ya watu waliopata maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 nchini kufikia 254, kutoka wagonjwa 147 waliotolewa taarifa Aprili 17, mwaka huu.

Pia Wizara ikatangaza vifo vitatu, vilivyotokea jijini Dar es Salaam vya watu waliothibitishwa kuwa na maambukizi ya Covid-19. Naye Mwandishi Wetu, Magnus Mahenge anaripoti kutoka Dodoma kuwa mmoja wa wabunge nchini, amethibishwa kuugua homa hiyo ya mapafu, inayoenezwa na virusi vya corona.

Akitoa taarifa ya Spika wa Bunge, Job Ndugai bungeni jijini hapa jana, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema wamepata taarifa kwamba mmoja wa wabunge amepata maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19. Dk Tulia alisema Spika Ndugai ametoa taarifa kwamba mbunge huyo, anaendelea vizuri na serikali inaendelea kumpatia matibabu kwa kadiri inavyowezekana.

Alisema taarifa zinaonesha mbunge huyo, alisafiri kwenda Dar es Salaam siku za hivi karibuni na aliporudi bungeni kuanzia Jumatano iliyopita, alianza kujisikia ana dalili za ugonjwa huo, kama wanazoeleza watalaamu wa wa afya. Dk Tulia alisema baada ya kupata vipimo, baadaye ilithibitika kwamba ana dalili hizo na hivyo ameambukizwa ugonjwa huo, unasambazwa na virusi vya corona.

“Spika ametangaza kwamba wabunge wanatakiwa kuzingatia na kufuata maelekezo bungeni wakati wowote wakiwa bungeni kama watalaamu wa afya wanavyoelekeza,” alisema Dk Tulia.

Dk Tulia alitoa onyo kila mbunge anapoingia bungeni, akae sehemu yake, asikea katika kiti cha mbunge mwingine, ili kufutilia mbunge na watu wanaomzunguka katika eneo hilo.

“Kila mbunge anatakiwa kukaa eneo linamhusu yeye kama sehemu ya jamii na kama kiongozi anayetaka kulinda afya za wengine,” alisema Naibu Spika, ikiwa ni ishara ya kuchukua tahadhari ya kudhibiti maambukizi.

Alisema, “tujitahidi kukaa maeneo yetu ili kulinda maeneo mengine ili kutohamisha virusi kutoka kiti kimoja hadi kingine, ili pia iwe rahisi kufuatilia na changamoto imetokea hapo.”

Dk Tulia alisema baada ya kikao hicho, kutokana na virusi kutinga bungeni, aliwataka wabunge wote baada ya kuahirisha Bunge kuondoka maeneo ya Bunge ili kutoa nafasi kwa ajili ya watalaamu wa afya, kunyunyiza dawa na wanapoondoka waende nyumbani.

SERIKALI imewataka waliohujumu mali za vyama vya ushirika kujisalimisha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi