loader
Corona isikuzuie kuhakiki taarifa Daftari la Wapigakura

Corona isikuzuie kuhakiki taarifa Daftari la Wapigakura

TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazoendelea kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (COVID- 19), huku majukumu yakiendelea nchini kama kawaida.

Kwa mantiki hiyo, ikumbukwe kuwa mwaka huu 2020 ni wa Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kuwachagua viongozi mbalimbali akiwemo Rais, Wabunge na hata madiwani.

Ili kufikia mchakato huo wa uchaguzi, zipo taratibu mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika kabla, ikiwa ni pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuratibu shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura.

Katika utaratibu huo, wananchi ambao hawakuweza kuhakiki na kuboresha taarifa zao katika daftari hilo katika kazi iliyofanyika mapema Februari kwa Awamu ya Kwanza wanahimizwa kujitokeza kuanzia Mei 2,2020 hadi Mei 4 ili kuhakikisha kuwa hawatokosa haki yao ya kupiga kura kutokana na majina yao kutokuwepo katika daftari hilo.

Aidha wananchi wanatakiwa kutumia muda huo uliopangwa na NEC, licha ya kuwepo kwa kwa maambukizi ya Corona kwa kuwa tayari Tume imenunua vifaa kinga vinavyotakiwa kwa ajili ya kuchukua tahadhari za maambukizi ya ugonjwa wa COVID – 19 na tayari imetoa maelekezo kwa watendaji wa uboreshaji kuzingatia miongozo ya afya.

Uboreshaji wa daftari hilo ni pamoja na kuwaingiza wale waliofikisha miaka 18 au watakaofikisha umri huo ifikapo Octoba mwaka huu, jambo ambalo litawasaidia kushuriki katika hatua ya kupiga kura kuchagua viongozi wao.

Ni muhimu pia kwa kila atakayekwenda kuhakiki au kuboresha taarifa zake, kuhakikisha anachukua tahadhari mwenyewe kwa kuepuka misongamano, kuvaa barakoa na hata kuendelea kunawa mikono kwa maji na sabuni kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya.

Kwa muktadha huo, haitarajiwi ifikapo uchaguzi, wakawepo wananchi ambao watajitokeza kulalamika kuwa hawakuweza kujitokeza kuhakiki majina yao kutokana na hofu ya maambukizi ya corona, la hasha kwa kuwa hatua za udhibiti wa afya zinachukuliwa na mamlaka husika ni vyema kuzingatia muda uliopangwa ili kutekeleza suala hilo.

Ni muhimu kukumbuka kuwa muda uliotolewa kwa ajili ya uboreshaji wa daftari hilo ni siku tatu, ambazo kila mmoja anatakiwa kuhakikisha anazitumia ipasavyo ili kujiweka sawa ili uchaguzi ufikapo asikose haki y apiga kura kwa mujibu wa taratibu.

Ikumbukwe kuwa kila mamlaka ina kanuni za taratibu zake za utendaji, hivyo ni vyema kwa wananchi pamoja na kuwepo kwa maambukizi hayo, kuhakikisha hawatokosa haki yao kikatiba ya kupiga kura muda utakapofika, badala yake kujitokeza kuhakiki majina wakatio huo wa uboreshaji wa daftari.

Kwa mujibu wa NEC raundi ya pili katika awamu hiyo ya pili ya uboreshaji wa daftari hilo katika mikoa 14 kwa Tanzania Bara ambayo ni pamoja na Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma, Iringa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Wakati wa uboreshaji maeneo yanayohusika ni Tanzania Visiwani na mikoa 14 ya Tanzania Bara ambapo vituo vya kuandikisha wapiga kura vipatavyo 2001 vitahusika

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/154a5671a0cb8990d05c981f53ce00fd.jpeg

SERIKALI kupitia Shirika ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi