loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kwanini Muungano?

Hapa nyumbani juma la jana tumeadhimisha miaka 56 ya Muungano.

Huko nyuma nimepata kuandika kuwa, kwetu sisi wa Tanganyika, jambo la Zanzibar ni letu, imani hiyo pia iko visiwani, kuwa jambo la Tanganyika ni lao.Tuko jirani mno na tuna historia ya pamoja.

Ni ndugu wa damu. Na tujifunze kupitia historia.

Nimeamini siku zote kuwa, historia ni mwalimu mzuri. Mwandishi, Ryszard Kapuchinski, alikuwepo Dar es Salaam na Zanzibar wakati wa Mapinduzi ya mwaka 1964.

Kapuchinski anaandika kuwa, Karume alikuwa Dar es Salaam wakati Mapinduzi yale yakiendelea kule visiwani.

Ameeleza pia kuwa, mtu aliyekuwa na udhibiti wa Mapinduzi kwenye ‘field’ wakati Karume akiwa nje ya Zanzibar, ni John Okello aliyekuwa na umri wa miaka 25 tu.

Kapuchinski anamzungumzia Karume kama mtu aliyekuwa akizungumza kwa sauti ya juu sana hata ukikaa nae karibu. Mara nyingi Karume alikuwapo pale New Africa Hotel, Dar es Salaam, mahali walipokutana wanamapinduzi wengi wa bara hili.

“Pale juu New Africa Hotel kulikuwa na baa watu wakinywa kahawa na vinywaji vingine. Hapo walikusanyika wanaharakati wa mapambano ya ukombozi wa Afrika kutoka kona mbalimbali za bara hili na nje.

Mahali hapa ilipangwa mikakati. Kwenye meza moja unaweza kumwona, Edward Mondlane wa Frelimo akiongea na Keneth Kaunda wa UNIP. Meza nyingine unamwona Karume akizungumza na Chisiza wa Malawi. Katika ukanda huu, Tanganyika ndio iliwatangulia wenzake kujikomboa.”- Ryszard Kapuscinski, Ebenholt ( Kwa Kiswidi) page 67- 88).

Kwanini Muungano? Ninapotafakari mitazamo tofauti juu ya dhana ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwa vile nimepata bahati ya kufika visiwani humo na kuzungumza na Wazanzibari wa Mji Mkongwe na wa mashambani, kuna uhalisia ninaouona kuwa, suala la Zanzibar na hususan Muungano si jepesi kama wengine wanavyofikiri au wanavyotutaka tufikiri.

Maana, Muungano ni zao la Mapinduzi ya 1964. Yale ya 1964 yalikuwa ni Mapinduzi ya umma. Ni Mapinduzi ya wajamaa wa Kiafrika.

Ni muhimu watu wakajua historia sahihi ya Mapinduzi, lakini, yumkini swali muhimu leo si nani aliyewaongoza wakulima, wavuvi na wakwezi wale kufanya mapinduzi, bali kuyafahamu malengo ya mapinduzi yale na kama yamefikiwa.

Naamini kuwa, kuuvunja Muungano leo ni kuvunja misingi ya uwapo wa Tanzania kama dola. Kuna hasara kidogo sana kubaki kwenye Muungano na hasara na madhara makubwa zaidi kuwa nje ya Muungano.

Zanzibar ya jana, leo na kesho, itabaki kuwa ni mkusanyiko wa wenyeji wa asili mbalimbali. Na wengi ni Waafrika wa kutokea Tanganyika.

Mathalan, Zanzibar ina Wazanzibari wenye asili ya unyamwezi, usukuma, umakonde, uluguru, uzaramo, undengereko, uarabu, ushirazi na kadhalika. Hivyo basi, swali gumu ni je, Mzanzibari ni nani nje ya Muungano?

Unafikiri haya unapokutana na Wazanzibari wenye kuzungumza kinyamwezi lakini hawajawahi kukanyaga Sikonge wala Urambo, Tabora. Mtafakari Mwalimu Nyerere aliposema, mwaka ule 1964 kuwa, kama ingewezekana Zanzibar isogezwe na upepo wa bahari na iwe mbali na Tanganyika huenda ingekuwa nafuu. Naye Nyerere alikuwa akisumbuliwa na ukweli huo.

Kuwa ni vigumu kwa Tanganyika kuondokana na Zanzibar katika uhalisia uliopo. Tulivyo sasa, suala la Zanzibar ni letu Tanganyika, na la Tanganyika ni la Zanzibar pia. Imekuwa hivyo jana, ndivyo ilivyo leo, daima itakuwa hivyo.

Yalikuwa malengo sahihi ya waasisi wa Muungano, kuwa uanze na serikali mbili kwa lengo la kwenda kwenye serikali moja. Na kuunganisha vyama; Afro Shiraz na TANU ulikuwa ni mwanzo wa safari ya kuelekea kwenye kuyafikia malengo hayo.

Maana, serikali kibaraka ya Sultan iliyopinduliwa mwaka 1964 ( Yale ni mapinduzi, si coup d’etat) kama wengine wanavyopotosha kuwa haikuwa na malengo ya kuukomboa umma wa Zanzibar ulio na mchanganyiko wa hata wenye asili ya Bara. Serikali iliyoundwa na ZNP na ZPPP ilikuwa ni mabaki ya usultani, ambao wanyonge walio wengi visiwani hawakuwa na faida nao. Huu ni wakati wa kujitafakari. Ni wakati wa kujisahihisha pia.

Kuyaacha malengo ya waasisi ya kuufikia Muungano kamili wa serikali moja kutoka kwenye serikali mbili na kubadili mwelekeo kwenda kwenye serikali tatu, kimsingi itakuwa ni kuianza safari ya kurudi Tanganyika na Zanzibar pasipo Muungano.

Historia inatufundisha nini? Itakumbukwa baada ya Vita Kuu ya Pili, dunia ilipitia kipindi cha vita baridi. Miaka ile ya 60 dunia iligawanyika katika kambi mbili kubwa kiitikadi; zilijulikana kama Warsaw Pact na Nato Pact.

Kambi ya Warsaw iliongozwa na Urusi ya zamani na ile ya NATO iliongozwa na Marekani. Kulikuwapo pia na kundi la nchi zisizofungamana na upande wowote.

Tanzania ilikuwa mwanachama wa kundi hili. Hata hivyo, nyingi ya nchi hizi kimsingi zilikuwa na upande zilizoegemea kati ya makundi mawili niliyoyataja. Tunasoma kuwa, Marekani na hususan kupitia shirika lake la ujasusi la CIA, ilijiingiza kwa mara ya kwanza katika siasa za Zanzibar mara baada ya Mapinduzi ya 1964.

Ni kwa lengo la kupunguza kasi ya kuenea kwa ukomunisti. Marekani iliingiwa na hofu ya Zanzibar kama kisiwa kutumiwa na wakomunisti. Katika Zanzibar bado kuna kumbukumbu ya historia hii kwa kuyaangalia majina kama Uwanja wa Mao Tse Tung, Hospitali ya V.I Lenin, shule za Fidel Castro, Patrice Lumumba na mengineyo. Yote haya yalikuwa na mwelekeo wa kambi ya Warsaw; Ukomunisti.

Mvutano wa kiitikadi kati ya Warsaw na NATO uliendelea kuwapo hadi pale ukuta wa Berlin uliopoangushwa Agosti 23, 1989.

Huo ndio ulikuwa mwisho wa vita baridi ya dunia. Marekani ikabaki bila mpinzani wa kiitikadi. Kuanzia hapo, upepo wa kisiasa uligeuka ghafla, wimbi la demokrasia ya vyama vingi likaanzia Ulaya Mashariki na kuikumba Afrika.

Kati ya mwaka 1990 hadi 1998, tulishuhudia kuwapo kwa ombwe la kiitikadi. Uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 1995 ulifanyika kukiwa na ombwe hilo la kiitikadi duniani.

Miaka mitatu baadae, Agosti 7, 1998, sura ya dunia ilianza kubadilika tena Ni mara ile balozi za Marekani Nairobi na Dar es Salaam zilipolipuliwa. Septemba 11, 2001 sura ya dunia ilibadilika ghafla, pale kikundi cha kigaidi cha Al qaeda kilipofanya maangamizi makubwa katika miji ya Washington na New York.

Hii ni tafakuri endelevu.

UJUMBE MUHIMU KWAKO MSOMAJI: Corona si mzaha.

Epuka mikusanyiko. Nawa mikono kwa maji yanayotiririka kwa sabuni.

Toka nyumbani kama una jambo la muhimu tu.

Fuata maelekezo ya wataalam. Jihadhari, Usitaharuki.

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Maggid Mjengwa

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi