loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kabudi- Jaji Ramadhani alisamehe wote

JAJI Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani, anatarajiwa kuzikwa keshokutwa Jumamosi katika makazi yake yaliyopo Kimara - King’ongo wilayani Ubungo mkoani Dar es Salaam sehemu ambayo alizikwa mama yake mzazi.

Aidha, watu waliowahi kufanya kazi na Jaji Ramadhani (75) wakiwemo mawaziri, wamemuelezea kuwa alikuwa Mtanzania kindakindaki, mnyenyekevu, mwadilifu na aliyekuwa na utumishi uliotukuka katika nafasi zote alizowahi kuwa nazo.

Wakati hayo yakijiri kuhusu Jaji Ramadhani, viongozi na watu wengine maarufu waliofariki hivi karibuni, baadhi maziko yao bado yanasubiri ripoti ya madaktari, ikiwa vifo vyao vinahusika na virusi vya corona ili kutoa utaratibu.

Aidha, aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Kamote, familia imeruhusiwa kumsafirisha hivyo atazikwa leo kijijini kwake Kilometa Saba wilayani Muheza mkoani Tanga.

Wakili Gaudious Ishengoma anatarajiwa kuzikwa leo wilayani Mkuranga mkoani Pwani kwa usimamizi wa serikali na wanafamilia watano, huku mdogo wa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, Ben Lowassa imeelezwa na familia kuwa alizikwa jana kwa usimamizi wa serikali na wanafamilia wachache katika makaburi ya Ununio jijini Dar es Salaam huku maombolezo mengine yakifanyika kijijini kwao, Monduli mkoani Arusha.

Maziko ya Jaji mstaafu Mussa Kwikima, yalikuwa yanasubiri taarifa za madaktari jana, ingawa familia ilisema kuwa walipanga kumzika kijijini kwake mkoani Tabora.

Mtoto wa Jaji Ramadhani, Bridget Ramadhani alisema jana kuwa familia imeridhia baba yao azikwe Kimara King’ongo keshokutwa baada ya Ibada ya Misa itakayofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Albano, Posta jijini Dar Salaam.

Hata hivyo, alisema wanasubiri ratiba ya serikali.

Kabudi: Mtanzania kindakindaki

Akizungumza kuhusu namna alivyomfahamu Jaji Ramadhani, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alisema alikuwa Mtanzania kindakindaki na mzalendo wa kweli, aliyeishi alichokisema kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.

“Nimempoteza kaka yangu, nilipomtembelea alipokuwa akiumwa alinitambulisha kwa ndugu zake kuwa mimi ni mdogo wake. Ni Mtanzania halisi, Mzanzibari kwa kuzaliwa, Mtanzania wa kukulia Bara, mzalendo, aliyekuwa na hekima, mshauri wa wengi na alitoa msamaha kwa wote waliomkosea,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema ni mtu mwenye historia ya kipekee kwa Taifa, kwani babu yake aliyerithi jina lake mwalimu “Augustino Ramadhani” ndiye mwasisi wa chama cha African Association of Zanzibar na Rais wa kwanza wa chama hicho, kilichozaa chama cha Afro Shiraz na kuwa sababu ya wazee hao kupambana na biashara za utumwa.

Profesa Kabudi alisema baba wa Jaji Ramadhani, Mwalimu Mathew Douglas Ramadhani alikuwa Mzanzibari wa kwanza kupata Shahada ya Sanaa nchini Uingereza na kufanya kazi kama Mkuu wa Shule ya Sekondari wa kwanza Mwafrika mwaka 1951 Mpwapwa mkoani Dodoma.

Alisema amefanya naye kazi akiwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na alikuwa msaada mkubwa kwa maboresho ya sheria na mfumo wa Mahakama uliopo sasa hata wakati akiwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Alifanya naye kazi pia katika Tume ya Marekebisho ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

“Watu wa kaliba yake si rahisi kuzungumza na kila mtu, lakini Jaji Augustino Ramadhani hakuwa na majivuno, alizungumza na mtoto asiye na chochote mpaka mtu mzima mwenye cheo kikubwa. Aliniachia kazi ya kuwa Msajili wa Kanisa la Anglikana Tanzania mwaka 2007 baada ya kutumika kuanzia mwaka 2000. Huwezi kujua alikuwa mwanajeshi kutokana na unyenyekevu aliyokuwa nao,” alisema na kuhamasisha Watanzania kumuenzi kwa mema yake.

Waziri Zungu

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Azzan Zungu alisema amempoteza ndugu, kwani wazazi wa Jaji Ramadhani na wazazi wake, walikuwa na undugu wa asili.

“Kifo chake ni pengo kubwa kwa taifa letu, mimi binasi tulikuwa pamoja kwenye kazi za serikali na tulichaguliwa kucheza timu ya ngome ya basketball na hatimae kucheza timu ya taifa, ni mtu mwadilifu na alipenda kijishusha chini. Mungu ampokee kwa kumpa makazi salama,” alisema Zungu.

Dk Abbasi Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi alisema, “Binafsi nilimfahamu kama mmoja wa wataalamu bingwa wa sheria katika nchi hii na alikuwa na mapenzi makubwa na mfumo wa utoaji haki kuboreshwa.”

Dk Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, alisema Jaji Ramadhani alikuwa pia karibu na wanahabari.

“Nakumbuka nilikuwa miongoni mwa wanahabari wa kwanza kumfanyia mahojiano wakati huo nikiwa mmoja wa wahariri katika Gazeti la Majira. Tutamkumbuka kwa utumishi kwa Watanzania na wana Afrika ambako pia alipata kuwa Jaji na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu,” alisema Dk Abbasi.

Jaji Ramadhani alifariki juzi asubuhi kutokana na shambulio la moyo. Hata hivyo, familia yake ilieleza kuwa aliugua kwa zaidi ya miaka 10 saratani ya tezi dume, na hali yake ilibadilika Februari mwaka huu na kutibiwa Nairobi na Aga Khan jijini Dar es Salaam.

Ameacha mke Saada Mbarouk na watoto wanne; Francis, Mathew, Marina na Bridget.

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi