loader
Makonda atoa siku 10 kwa ma-DC

Makonda atoa siku 10 kwa ma-DC

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa siku 10 kwa wakuu wa wilaya zote tano za mkoa huo, kupitia upya sheria za mazingira na kutoa mapendekezo nini kifanyike kudhibiti mito inayofuata makazi ya watu na shughuli za kibinadamu zinazoharibu mazingira na kuhatarisha maisha.

Aidha, ametoa mabati 1,000 kwa wajane wa mkoa huo ambao nyumba zao zimeezuliwa paa kutokana na mvua na amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa, wapeleke majina yao kwake ili wakifikia kuezeka, wapewe mabati.

Makonda aliyasema hayo jana, alipotembelea wakazi wa Mtaa wa Mzimuni wilayani Kinondoni walioathika kwa mafuriko yaliotokana na mto Mbezi kuacha mkondo wake. Nyumba 150 zimebomoka tangu mvua zianze kunyesha huku mvua ya juzi pekee, ikisababisha nyumba 25 kati ya hizo kubomoka.

Nyumba nyingine 150 zimeathiriwa pia. Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo baada ya kuzunguka katika maeneo walioathirika, Makonda aliwasilisha kwa wananchi mambo makuu matatu.

“Kwanza niwape pole wananchi kwa mvua, niwakumbushe tu kwamba serikali ilishatoa maelekezo ya kuchukua tahadhari kwa wanaoishi maeneo hatarishi. Lakini pili athari za mvua ni kubwa, nawaagiza wakuu wa wilaya tano za mkoa kupitia upya sheria za mazingira na mito yake,” alisema Makonda.

Aliwaagiza kukaa na viongozi wa Serikali za Mitaa katika maeneo yao na ndani ya siku 10, wamfikishie ripoti ya mito mikubwa na midogo na mapendekezo ya nini kifanyike kwa kuwa ipo inayofuata makazi ya watu lakini ipo inayoharibiwa kwa shughuli hatarishi zinazofanyika mitoni ikiwamo kuzoa mchanga.

Alisema serikali ilifanikiwa kujenga Daraja la Malecela lililopo katika mtaa huo na kupunguza kero ya mafuriko, lakini mto huo Mbezi umetanuka na kusababisha mafuriko mvua zinaponyesha, hivyo lazima kupata suluhisho la kudumu kama lililopatikana mto Ng’ombe.

“Ma-DC wapite waangalie mabadiliko ya tabia nchi wakae na viongozi wa Serikali za Mitaa, watendaji wa Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Ardhi na mkoa tuangalie nini kifanyike kujenga mito, madaraja na barabara za kudumu. Tumechoka kusikia kila mvua inaponyesha maafa makubwa kwa wananchi,” alisisitiza.

Kuhusu jambo la tatu, Makonda alisema anatambua zipo familia zina changamoto kubwa ya makazi kutokana na nyumba zao kuezuliwa paa.

“Ni ubinadamu tu kiongozi unatakiwa ufanye kwa ajili ya wengine. Nina mabati ya nyumba 1,000 za wajane ambazo zimeezuliwa paa mkoa wa Dar es Salaam, nimuombe kiongozi wenu hapa kama anao wajane ambao nyumba zao zimebomoka aniletee majina yao ili wakifikia kupaua, tuwape mabati,” alisema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f8abdb6b3a97e0e042997a3eff77f516.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi