loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Muumbue anayekiuka bei elekezi sukari

TAKRIBANI wiki mbili zilizopita, wengi wetu tuliokwenda dukani kununua sukari tulipigwa na mshangao baada ya kukuta ongezeko kubwa la bei.

Katika maeneo tofauti nchini, wafanyabiashara wote ‘waliongea’ lugha moja ya kupandisha bei kana kwamba walifanya kikao cha kufikia uamuzi wa bei inayofanana.

Katika baadhi ya maduka, wauzaji waligoma kuuza wakidai sukari haipo jambo ambalo halikuwa kweli.

Walifanya hivyo ili kuaminisha jamii kuwa sukari imeadimika ili baada ya siku chache, wajifanye ndiyo wamenunua kisha waendelee kuuza kwa bei ya kuruka.

Wafanyabiashara wa reja reja waliwanyooshea vidole wale wa jumla wakidai ndiyo wamewapandishia bei jambo ambalo na wao hawawezi kuuza kwa bei ya hasara.

Lakini ukweli ni kwamba, hata wale waliokuwa na akiba ya sukari waliyoinunua kwa bei ya kawaida, waliamua kupandisha bei na kujipatia faida nono kwa kigezo kwamba wamepandishiwa bei na wauzaji wa jumla.

Mathalani, jijini Dar es Salaam ambako kwa mujibu wa bei elekezi wanapaswa kuuza sukari bila kuzidi Sh 2,600, ikaanza kuuzwa kati ya Sh 3,500 hadi 4,000 kwa kilogramu.

Ishukuriwe serikali kwa usikivu wake kwa sauti zilizojitokeza kulalamikia hali hiyo ambayo awali, wafanyabiashara walidai imetokana na sukari kuadimika.

Lakini kesho yake, serikali kupitia kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, iliweka bayana kuwa hakuna uhaba wa sukari nchini. Ilifafanua changamoto iliyokuwapo na ikasema imeshatatuliwa.

Ishukuriwe serikali kwa kuja na bei elekezi ya sukari ambayo ni kati ya Sh 2,600 na 3,200 kulingana na umbali wa mkoa.

Serikali imeonya wafanyabiashara watakaobainika kupandisha bei, watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wapo wafanyabiashara wanaoweza kuchukulia poa tamko hili la serikali lililotolewa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa. Naamini wapo wafanyabiashara ambao katika vipindi vilivyopita, walizoea kufanya jinsi watakavyo.

Wakishapandisha bei hata serikali ikisema, wanajua kwamba hakuna ufuatiliaji. Matokeo yake, bei inaendelea na kuhalalishwa na kutoa mwanya wa kupandisha holela bei ya sukari kadri watakavyo.

Kwa serikali ya awamu ya tano ni tofauti; Sheria lazima itachukua mkondo wake.

Wafanyabiashara watambue kwamba upangaji bei ya ukomo wa juu ni suala la kisheria. Sheria ya Sukari Namba 26 ya Mwaka 2001 (Kifungu cha 251) chini ya kifungu cha 11A inampa Mamlaka waziri mwenye dhamana ya kilimo kutangaza bei ya ukomo.

Waziri mwenye dhamana amesisitiza wafanyabiashara kuzingatia maelekezo.

Amewaambia kabisa kwamba atakayekiuka maelekezo atakuwa ametenda kosa na hivyo atafikishwa katika vyombo vya sheria.

Kwa mujibu wa Waziri Hasunga, adhabu itahusisha ama kunyang’anywa leseni ya biashara, kulipa faini au adhabu zote kwa pamoja.

Ni wakati wa wananchi (wateja) kushirikiana na serikali kuwaelekezea vidole wafanyabiashara watakaokaidi agizo hili halali la serikali.

Mathalani, kwa wakazi wa Dar es Salaam ambako jicho langu limeshuhudia baadhi ya maduka yakiendelea kuuza kwa bei yao waliyoipanga ya kati ya Sh 3,500 na 4,000, wasiogope kuwaumbua wanaouza sukari kwa zaidi ya bei elekezi ambayo ni Sh 2,600.

Hii ina maana, mkazi yeyote wa jijini humo hapaswi kukubali kuuziwa kilogramu ya sukari kwa zaidi ya bei hiyo ya ukomo.

Wale wa Iringa, Njombe, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Singida, Tabora na Dodoma wasikubali kuuziwa sukari kwa zaidi ya Sh 2,900.

Lindi na Mtwara bei ya ukomo ni Sh 2,800), Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Pwani, Tanga na Morogoro ni Sh 2,700. Songwe, Mbeya, Mara, Kagera ni Sh 3,000 na Rukwa, Katavi, Ruvuma na Kigoma Sh 3,200.

Kama ambavyo waziri amesema kwamba serikali haipo tayari kuona wananchi wake wanaumia kwa manufaa ya watu wachache, vivyo hivyo wananchi wasiogope kuenzi msimamo huu wa usikivu wa serikali kwa kutoa taarifa kuhusu wafanyabiashara wakaidi.

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi