loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwanamke fanya haya mtoto ayazoee maisha na corona

DUNIA hivi sasa inakabiliwa na janga kubwa la mlipuko wa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.

Ugonjwa huo hatari unaendelea kuangamiza maelfu ya maisha ya watu kote duniani wakiwemo Watanzania.

Katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo ili usienee zaidi, njia mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na mataifa mengi kufunga mipaka yake, kufunga vyuo na shule na kuwaweka karantini wale wote wanaodhaniwa kukaa au kuwa karibu na waathirika wa ugonjwa huo.

Kutokana na hatua hiyo, wanafunzi wa vyuo na shule wako nyumbani na familia zao kwenye likizo ya lazima na wametakiwa kutozurura au kutembelea ndugu, bali kubaki nyumbani kama njia mojawapo ya kukijinga na kuenea kwa virusi hivyo hatari vya corona.

Katika kipindi hiki ni vyema basi wazazi, walezi na ndugu kwenye familia wakawasaidia watoto kwa kuwaelimisha jinsi ya kukabiliana na majanga ili kuwawezesha kuendelea na maisha bila kuona upweke wakiwa ndani ya nyumba. Mambo ya msingi ya kuwasaidia watoto ni pamoja na haya yafuatayo:

1.Kuwafariji na kuwathibitishia

Ni ngumu kuelewa kila linaloendelea kuhusu maambukizi ya ugonjwa huo kutokana na umri wao, lakini ni vema kuwapa faraja na kuwahakikishia kuwa suala hili litapita na maisha yataendelea kama kawaida kwa kuwaelezea masuala ambayo kwao itakuwa rahisi kuelewa.

2.Waeleze mikakati ya kuwa salama

Unapozungumza na watoto, waelezee njia za usalama wao kuwa wanatakiwa wawe salama kuepuka maambukizi kuliko kutumia njia za kuwaamrisha bali waeleze kwa nini wanatakiwa kunawa mikono yao mara kwa mara, kukaa ndani bila kucheza na rafiki zao na mengineyo.

Ni vema kuwa na muda wa kuhakikisha wanakuelewa katika kuhakikisha wanakuwa salama muda wote hivyo inakuwa rahisi kukuelewa unapowaeleza wasitoke ndani ya nyumba.

3. Jibu maswali yao Watoto wana maswali mengi siku zote, wapo wanaouliza mara kwa mara na ndiyo njia yao kufahamu masuala mbalimbali yanayoendelea baina yao hivyo ni lazima kuwa mvumilivu kwao. Wasikilize na kuwajibu hata kama ukifanya hivyo mara kumi zaidi.

4.Waendelee na kazi za shule Kuacha kwenda shule kwa sababu ya tatizo hilo si mwisho wa kujisomea na kuendelea na kazi za shule, ni vema kuendelea kuwapa kazi za shule ili wafanye kwa kutumia mitandao au vitabu vyao vya shule.

Kwa kufanya hivyo, pale shule zinazofunguliwa watakuwa hawajasahau kitu katika masomo yao hivyo inakuwa rahisi kuendelea mbele.

5. Wape muda wa kucheza

Ikiwa umebahatika kuwa na eneo nyumbani kwako, waache watoke nje ya nyumba ili kupata hewa safi, mwanga wa jua na kucheza.

Hata kama hawachezi na rafiki zao watafurahia kucheza wenyewe.

Kama huna nafasi nje ya kucheza, waache wacheze michezo mbalimbali ndani na kuwafundisha wanapomaliza kufanya usafi wenyewe.

6. Weka ratiba

Bila ratiba ya mambo ya kila siku, maisha yatakuwa ya vurugu hususan katika hali kama hii ambayo haifahamiki tatizo hili litadumu kwa muda gani, kuwa na ratiba ya kila siku na kuwafundisha watoto kufuata ratiba, ikiwemo muda wa masomo, kucheza na familia.

7.Waoneshe upendo

Ikiwa una jambo linakutatiza iwe kutokana na hali hii ya ugonjwa au suala lolote, ni vema kukaa chumbani kwako na kulitafakari ili watoto wasiingiwe na hofu.

Ni muhimu kuwaonesha upendo kwa kuwa nao muda mwingi, jambo litakalowafanya wao kuona kila kitu kiko sawa, licha ya kutakiwa kukaa ndani muda wote.

Ikiwa mwanamke utafuata njia hizi, mbali na kumsaidia mtoto kuepuka maambukizi lakini pia utawasaidia kutokuwa na hofu ya ugonjwa kwa nyakati hizi.

Lakini muhimu ni kuwa ikiwa wewe bado unatoka na kwenda kwenye shughuli zako au kufanya manunuzi ni vema kufuata kanuni za afya, ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na kutumia vitakasa mikono kuepuka kuwapelekea watoto ugonjwa huo.

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi