loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ligi Kuu Bara ichezwe viwanja vya Dar es Salaam

LIGI Kuu Tanzania Bara huenda ikaendelea tena mwezi ujao baada ya kusimama kwa takribani miezi miwili kutokana na mlipuko wa janga la virusi vya corona.

Dalili za kutaka kurejea kwa ligi hiyo ni jambo zuri sana pamoja na kwamba itachezwa bila ya kuwa na mashabiki uwanjani, hilo sio muhimu, kikubwa ni kurejea tena kwa ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 20.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Joseph Pombe Magufuli alisema wiki iliyopita kuwa atawasiliana na washauri wake ili kuona nini kinafanyika Ligi Kuu Tanzania Bara inarudi.

Kauli hiyo ilikuwa faraja kubwa kwa wadau wa michezo na hasa soka, ambao wameumisi mchezo wao kwa muda na zaidi baada ya hata ligi zile kubwa na hata ndogo za nje nazo kusimamishwa.

Hakuna ubishi kuwa kurejea kwa Ligi Kuu ni faraja kubwa, kwani katika kipindi kigumu kama hiki cha corona ni muhimu sana kuwepo na kitu cha kufariji watu wanapokuwa wamejifungia ndani, ambako hakuna shughuli nyingi za kufanya. Jamani `Lockdown’ ina mambo yake na ndio watu wakati mwingine wanachanganyikiwa na kusababisha hata kuwepo matukio mengi ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji.

Ingawa Tanzania hakuna lockdown ya ujumla, lakini baadhi ya watu wako nyumbani na wanafanyia kazi huko, hivyo hali ya kujifungia nao inawahusu kwani wako ndani kama watu wa nchi zingine. Ligi Kuu itarejesha faraja majumbani, kwani watu watakuwa wakiangalia mechi hizo pamoja na zile za nje, kitu ambacho kitasaidia sana kuleta faraja katika kipindi hiki cha janga la corona au ugonjwa wa COVID-19.

Sasa ni jukumu la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi kukaa chini na kuangalia jinsi au mfumo gani utatumika kwanza kucheza ligi hiyo na pili utaratubu mzima licha ya kutokuwa na mashabiki.

Kwa England, wenyewe tayari wamesema kuwa watatumia viwanja takribani 10 kumalizia mechi zilizobaki za Ligi Kuu ya England na hakuna timu itakayokuwa mwenyeji, kwani kila timu inatakiwa kuwa mgeni.

Kwa ufafanuzi, hata kama timu imetoa kiwanja ijue kuwa kiwanja hicho kitatumiwa na timu zingine, ambazo utakuwa uwanja wao wa ugenini na mwenyeji wa hapo atakwenda kucheza kwenye viwanja vingine.

Kwa hiyo katika Ligi Kuu ya England, kila timu itakuwa inacheza kwenye viwanja huru (neutral venues), ili kutoa haki sawa kwa timu zote. Tukirudi kwetu, timu nyingi ziko tayari kucheza katika mfumo wowote na hasa ule wa nyumbani na ugenini, ambao zimeuzoea na zilikuwa zikiucheza huko nyuma kabla ya ligi kusimama. Hatahivyo, safu hii inapenda kutoa ushauri pamoja na Bodi ya Ligi kutaka mechi hizo zichezwe nyumbani na ugenini, lakini tunaona ni bora wakateua viwanja kadhaa jijini Dar es Salaam na timu zote kucheza kwenye viwanja hivyo.

Kwanza mfumo wa kuchagua viwanja utazisaidia sana timu kubana matumizi hasa ukizingatia kuwa mechi hizo hazitaudhuriwa na watu, hivyo hakutakuwa na viingilio na timu hazitapata fedha yoyote. Tayari timu zimeanza kulia kuwa hazina fedha, kwani katika kipindi chote cha ligi kusimama, wameshindwa kuingiza hata senti chache ili angalau wangepata fedha kidogo kwa ajili ya kitu fulani, lakini sasa hakuna kitu wanachoingiza.

Kama timu zimeanza kulia, basi ijulikane wazi kuwa timu hizo zitakuwa na hali mbaya zaidi pale zitakapoanza kusafiri na kwenda kucheza mechi kwenye viwanja vya ugenini na huko pia watakuwa hawapati pesa wakati watakuwa wakiingia gharama ya chakula, usafiri, malazi na mahitaji mengine. Timu ikisafiri itatakiwa kujigharamia usafiri, chakula, malazi na huduma nyingi kama matibabu na meingine, kwani huko wanakokwenda timu zitakuwa hazizalishi chochote, lakini zinahitaji fedha za kutumia.

Ushauri ni kwamba, TFF ichague viwanja kadhaa jijini Dar es Salaam kama vile Taifa, Uhuru, Karume, Azam Complex hata Bandari Tandika na vingine ili timu zitumie na kukaa mahali fulani, ambako wanaweza kupangishiwa na TFF ili kubana matumizi. Timu nyingi zilikuwa zinaishi kwa kutegemea mapato ya milangoni kabla ligi haijasimama, hivyo wakati huu zitakuwa na hali ngumu zaidi, hivyo TFF iangalie utaratibu wa kusisaidia.

Endapo mechi za ligi zitachezwa jijini Dar es Salaam hiyo itazisaidia sana klabu kuanzia kiuchumi na suala la kiafya, kwani itakuwa rahisi kuwadhibiti wachezaji na maambukizi ya virusi vya corona. Kitendo cha timu, waamuzi, waandishi na viongozi kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine, bila shaka kutaongeza hatari ya wao kuambukizwa virusi vya corona, hivyo ni bora wakachezea katika mkoa mmoja tu.

Huo ni ushauri tu na kikubwa ligi inatakiwa imalizike na bingwa ajulikana, hivyo TFF na Bodi ya Ligi pamoja na klabu shiriki ndizo zitaamua mfumo gani utumike na sisi tutakuwa tayari kuzifungulia TV zetu na kuangali mechi hizo nyumbani. Kwa upande wa wachezaji, wenyewe wanatakiwa kuwa makini katika kipindi hiki cha kukaa ndani, kwani wanatakiwa kujifanyisha mazoezi kabla ya kuanza mazoezi ya pamoja.

Muda utakuwa mdogo sana wa maandalizi, hivyo endapo mchezaji atakuwa hafanyi mazoezi katika kipindi hiki cha ligi kusimama, basi ajue atakuwa na kazi mara dufu kujiweka fiti. Ligi itakapoanza kuna wachezaji watakuwa fiti, kwale ambao sasa wanajifanyisha mazoezi na wengine watakuwa nyoronyoro, ambao kipindi hiki wamebweteka na kukaa tu nyumbani wakisubiri muda wa msosi ufike, hao watakuwa na hali ngumu sana ya kuondoa vitambi.

Yote na yote tunaisubiri Ligi Kuu Tanzania Bara kwa hamu na ije kwa mfumo wowote ule, mradi mechi zichezwe na bingwa apatikane uwanjani. Ingawa Simba ana pointi nyingi, lakini hadi sasa timu kama tatu au nne kila moja ina nafasi ya kuweza kulitwaa taji hilo, endapo Simba atateleza na hilo katika soka linawezekana.

KWA sasa nchi nzima ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi