loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwongozo wa kuzika waliokufa kwa corona waja

SERIKALI imesema iko mbioni kutoa mwongozowa mazishi na maziko ya marehemu wa virusi vya corona, ili ndugu na waombolezaji wengine, wasiwe kwenye hatari ya kupata maambukizi ya virusi hivyo.

Hato yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile. Alisema hayo juzi usiku kwenye kipindi cha MIALE, kinachorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1.

Dk Ndugulile alisema baada ya Rais Dk John Magufuli, kuruhusu ndugu kuzika marehemu wao, waliokufa kwa virusi vya corona na kuhakikisha wamehifadhiwa vizuri na vifaa vya PPE, ikiwemo mifuko maalum, wizara imeona ni vyema ikaandaa mwongozo wa jinsi gani marehemu hao watakuwa wanazikwa na ndugu zao.

“Tunataka tutoe mwongozo wa jinsi gani marehemu wa COVID-19 atazikwa, hii ni kuanzia jinsi gani atasafishwa na kufungwa kwenye mifuko maalum na hata idadi ya watu watakaoruhusiwa kuzika, kwa sababu tumeona hata baadhi ya viongozi wa dini wanashiriki wengi kwenye maziko, sasa hii ni hatari, lazima tuweke mwongozo kwenye hili kwa haraka,” alisema Dk Ndugulile.

Katika hatua nyingine, Dk Ndugulile alisema virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya mapafu, vimekuwa na tabia tofauti. Alisema sasa imebainika kuwa wengi wa wanaougua maradhi hayo, hawana dalili na asilimia 20 ya wanaougua, ndio hupata homa ya mapafu na kuhitaji vifaa maalumu vya kuwasaidia kupumua.

Alisema serikali hivi sasa imeona ipo haja ya kubadilisha mwongozo wa huduma kwa waathirika wote wa COVID-19, ambapo sasa wale watakaolazwa hospitalini, watakuwa ni wale tu wenye hali mbaya ya kuhitaji usaidizi wa vifaa vya kupumulia.

“Tumeona tubadilishe mwongozo, watakaolazwa ni wale tu wenye kuhitaji huduma ya matibabu zaidi kama wale wasioweza kupumua hivyo wanahitaji ventilators. Wale wote wenye hali nzuri watatakiwa wajitenge nyumbani na sio kwenda hospitalini,” alisema Dk Ndugulile.

Alisema kuwa virusi vya COVID-19, vimekuwa na tabia tofauti na athari zimekuwa tofauti, baina ya wagonjwa wa virusi hivyo wa Tanzania na wale mataifa ya Magharibi. Alisema tafiti lazima zifanywe ili kupata majibu ya epidemilogia, ya jinsi ya kutibu wagonjwa hao na aina gani ya dawa ni sahihi.

“Ndio maana Taasisi ya NIMR ilipewa maagizo na Rais Magufuli ya kukaa na wataalamu wengine wa ndani kutoka taasisi tofauti za utafiti waje na majibu ya jinsi ya kutibu watu wetu ,”alisisitiza Dk Ndugulile.

Kuhusu utafiti uliofanywa na moja ya nchi na kuonesha kuwa virusi vya COVID- 19, vipo pia kwenye mbegu za kiume za mgonjwa wa corona, Dk Ndugulile alisema utafiti mmoja, hauwezi kutosheleza kusema ugonjwa huo unaweza kusambazwa kwa njia ya kujamiiana.

“Ni lazima tafiti zaidi zifanywe kuthibitisha hilo, utafiti mmoja hauwezi kutosheleza kusema corona inaambukizwa pia kwa njia ya kujamiiana kutoka kwa mtu mwenye maambukizi kwenda kwa asiyenayo, ndio sayansi ilivyo,” alisisitiza Dk Ndugulile.

Mbali na hayo, aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo, kwa kuwasikiliza wataalamu wa afya na serikali. Aliwaonya wananchi kuacha kusikiliza habari za uzushi na za kutia hofu, kwani zinaweza kuwaharibu kisaikolojia.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi