loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Baada ya miaka 10, wakazi wa Nyamongo wajazwa manoti

WAKAZI 1,639 wa vijiji vya Matongo na Nyabichune katika eneo la Nyamongo Wilayani Tarime Mkoa wa Mara wamelipwa fi dia ya jumla ya Sh bilioni 33 baada ya kusubiri kwa kipindi cha miaka 10.

Fidia hiyo imelipwa juzi na Mgodi wa Barrick North Mara ikiwa utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa wakati wa ziara yake mkoani hapa ambapo alitaka suala hilo ikiwemo la uchafuzi wa mazingira limalizwe haraka.

Akizungumza wakati wa utoaji fidia na ugawaji wa hundi kwa wakazi hao waliopisha maeneo yao kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za mgodi huo, Waziri wa Madini Doto Biteko amewahakikishia wote wenye haki ya kulipwa fidia hiyo kuwa watalipwa fedha zao.

Aidha, alitoa pongezi kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kueleza kuwa wizara hiyo ilifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha inamaliza mgogoro wa fidia uliokuwepo baina ya wananchi na mgodi huo.

Pia, alimpongeza Mthamini Mkuu wa Serikali kwa kazi ya uthamini iliyofanyika na kuwezesha wananchi wanaopaswa kulipwa fidia zao wanalipwa na kuongeza, “ maisha ya kutegesha yamekwisha, serikali haitakubali kushuhudia watengeneza migogoro wakitengeneza migogoro hapa”.

Katika hatua nyingine, ameiagiza Bodi ya Kampuni ya Twiga Corporation Limited kuhakikisha inaufungaminisha mgodi huo na shughuli za wananchi kiuchumi ili waweze kunufaika na uwepo wa mgodi wake.

Vilevile, aliutaka mgodi huo kuangalia na kuzifanyia kazi changamoto za kijamii zinazowakabili wananchi wanaozunguka mgodi huo zikiwemo za maji, barabara na ili kujenga mahusiano mazuri na jamii hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Azzan ‘Zungu’ alisema wizara yake imejiridhisha kuhusu usalama wa taka sumu na kuongeza kuwa mara kwa mara umekuwa ukifanyika ukaguzi kuhakikisha maji hayo hayaathiri wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Pia, amewahakikishia Wananchi kuhusu ufuatiliaji wa Sheria na taratibu za mazingira kuhusu suala hilo. Naye, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula alisema utoaji fidia umechukua muda mrefu kwa sababu wananchi hawakuwa wakitoa taarifa sahihi na baadhi kutegesha na akatumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kweli kwenye masuala yote yanayohusu ulipaji fidia.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Migodi ya Barrick, Hilaire Diarra alisema kampuni hiyo imeanza safari mpya ya amani, ufanisi wa pamoja kwa maendeleo ya Jamii. Alisema kwa miaka mingi mahusiano kati ya mgodi na jamii hiyo yamekuwa siyo mazuri lakini hivi sasa mgodi huo unaamini katika kuyajenga upya.

Ameongeza kuwa Kamati ya Maendeleo ya Jamii imeundwa ili kuangalia vipaumbele katika eneo hilo na yote yatafanyika kupitia kamati hiyo.

“Tumetembea miezi minne kufikia hapa, makinikia, ushuru, utafiti, vibali vya kazi, wafanyakazi wa nje, usajili wa Jina la Twiga. Nakumbuka mara mwisho Waziri(Biteko) ulikuwa bado ukisisitiza suala la fidia liwe historia,” alisema Diarra.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dk. Samwel Gwamaka alisema mamlaka hiyo inafanyia kazi malalamiko ya wananchi wanaozunguka migodi sambamba na kukagua iwapo taratibu za mazingira zinafuatwa.

Ameongeza kuwa Barrick North Mara ni miongoni mwa migodi inayofuatiliwa kuhakikisha uendeshaji wake hauleti madhara kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa wateja wa Benki ya CRDB Boma Raballa, iliahidi kutoa huduma bora za kibenki kwa wananchi waliolipwa fidia kwa kuhakikisha inatoa elimu kuhusu matumizi bora ya fedha walizozipata ikiwemo kuhakikisha wanapata fedha hizo haraka.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Tarime

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi