loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mfereji mkubwa kuchimbwa Skimu ya Titye

TUME ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kuchimba mfereji mkubwa wenye kilometa sita ili usaidie kutoa maji yaliyozidi mashambani katika Skimu ya Titye iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.

Haya yameleezwa na Wizara ya Kilimo wakati kujibu swali la msingi la Mbunge wa Kasulu Vijijini, Augustine Holle (CCM) aliyehoji ni lini serikali itakamilisha ujenzi wa mradi wa umwagiliaji wa Titye/Lalambe uliopo wilayani Kasulu.

Majibu ya wizara kwa swali hiyo yalieleza kuwa Skimu ya Titye iliyopo Kijiji cha Titye, inapata maji ya umwagiliaji kutoka Mto Ruchugi unaotiririsha maji yake kwa mwaka mzima na ina jumla ya hekta 700 zilizopimwa na kusanifiwa ,ambapo kati ya hizo, hekta 575 zimeendelezwa kwa kilimo cha zao la mpunga.

“Eneo liloendelezwa lina miundombinu yote ya msingi ya kupeleka maji mashambani kama vile banio la kuchepusha maji kutoka mtoni, mfereji mkuu, mifereji ya kati iliyojengwa kwa mawe, mifereji ya mashambani, vigawa maji na barabara za shambani kwa ajili ya kurahisisha uingizaji na utoaji wa zana za kilimo pamoja na kusafirisha mazao yaliyovunwa,” ilieleza wizara.

Iliongeza, “Tunawapongeza wakulima wa Skimu ya Titye ambao walishiriki katika kusawazisha hekta 475 ambazo zinamwagiliwa na zinalimwa zao la mpunga huku eneo lililobakia la hekta 100 ambazo usawazishaji wake haujakamilika kwa sasa wakulima wanalima zao la mahindi.”

Aidha, katika msimu wa 2020/21, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu pamoja na wakulima, watahakikisha kwamba eneo lililobaki linasawazishwa ili kuwezesha uzalishaji na umwagiliaji wa eneo lote lililoendelezwa.

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi