loader
Picha

Hazina yawabana waliokopa dawa za viluwiluwi Kibaha

HALMASHAURI kadhaa zimeanza kukatwa fedha na Hazina, kulipa deni lililotokana na dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu, zilizochukua katika kiwanda cha Tanzania Biotech Product (TBP) Ltd na kushindwa kulipa.

Aidha, TBPL ambayo ni kampuni tanzu iliyo chini ya Shirika la Maendeleo Tanzania (NDC), imeendelea kulia na ukosefu wa masoko, unaochangiwa na kusuasua kwa halmashauri kununua bidhaa hiyo, hivyo kulazimika kutumia kampuni binafsi kuzunguka nchini kusaka masoko.

Rais Dk John Magufuli alipotembelea kiwanda hicho mwaka 2017 na pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika ziara yake kiwandani hapo mwaka juzi na kushuhudia uwapo wa dawa ambazo hazijapata soko, aliagiza halmashauri kununua dawa hizo na kuzitumia kutokomeza malaria.

Meneja Udhibiti Ubora wa kiwanda hicho, Samwel Mziray aliliambia gazeti hili jana kwamba kati Sh bilioni 1.4 ambazo TBP inazidai halmashauri tangu mwaka 2017, Hazina imesaidia kukata kwenye fungu la matumizi mengine (O C) na kuwawezesha kupata Sh milioni 900.

“Bado tunadai shilingi milioni 500,” alisema na kusema halmashauri zinazodaiwa zinatoka kwenye mikoa 12. Mziray ambaye amekiri kuwapo mwitikio mdogo wa halmashauri kununua bidhaa hiyo, alisema baada ya Rais Magufuli kutoa agizo mwaka 2017, halmashauri zilijitokeza lakini baadhi zilishindwa kulipa hadi hapo shirika lilipoomba O fisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) isaidie.

Kwa mujibu wa Mziray, awamu ya kwanza Rais Magufuli alilipia mwenyewe na kuagiza halmashauri zikachukue dawa hizo. Katika awamu ya pili, halmashauri zilichukua na kushindwa kulipa hadi hapo Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Hazina, ilipoombwa kusaidia kukata deni.

Alisema Tamisemi ilisaidia kuandika barua katika halmashauri zitenge bajeti, lakini nyingi zikawa zinalia kwamba vyanzo vya mapato yao ni vidogo, ndipo wakaishirikisha Wizara ya Fedha na Mipango kwa maana ya Hazina isaidie kupunguza kwenye O C zao ndipo wakafanikiwa.

“Kama isingepitia Hazina kwa kweli sidhani kama tungekuwa tumepata chochote mpaka sasa. Lakini hizo zote ni juhudi zetu, NDC, Tamisemi, Hazina na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,” alisema.

Mziray alisema zipo halmashauri chache zisizozidi 10 zilizoendelea kununua dawa tangu mwaka 2018 na zinachukua kwa kiwango kidogo cha wastani wa lita 200. Miongoni mwa halmashauri hizo ni Ilala na Kinondoni, zote za Dar es Salaam na Kibaha ya mkoani Pwani, ambazo kiasi kilichonunuliwa hakijafikia lita 100,000. Kwa mujibu wa Mziray, dawa zitaanza kupatikana nchi nzima kwenye maduka ya dawa za kilimo na mifugo.

Licha ya ujazo wa mililita 30 na lita 20 wa awali, kampuni imeongeza ufungashaji hivyo itapatikana pia kwenye nusu lita, lita moja, lita tano na lita 10. Mkakati mwingine uliofikiwa ni kuliwasilisha andiko kwa ofisi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhusu kampuni zinazofanya shughuli zinazosababisha kuwapo madimbwi zishiriki kuangamiza viluwiluwi wa mbu kwa kununua dawa hizo.

Kiwanda kina uwezo wa kuzalishaji lita milioni sita kwa mwaka, lakini kutokana na ukosefu wa masoko, kinazalisha pungufu kuepuka dawa kuharibika ghalani kwa kuwa muda wa matumizi yake ni miaka miwili baada ya kutengenezwa.

TBP ni kiwanda pekee katika Afrika kilichoanzishwa Julai 2015 na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kutafuta suluhisho la kupambana na malaria kwa kuua viluilui, badala ya kusubiri kuangamiza mbu waliokomaa.

Kilianza uzalishaji mwaka 2017 kwa thamani ya uwekezaji wa takribani Sh bilioni 50.6 kwa msaada wa teknolojia kutoka Cuba. Taarifa ya hivi karibuni ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu inasema Tanzania imepiga hatua katika mapambano dhidi ya malaria kutokana na kiwango cha maambukizi kupungua kwa asilimia 50 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017.

Katika taarifa hiyo ya maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani ambayo hufanyika kila Aprili 25, Waziri Ummy alisema maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 19 kutoka wagonjwa 150 kwa kila watu 1,000 mwaka 2015 hadi wagonjwa 122 mwaka 2019. Vifo vitokanavo na malaria vimepungua kwa asilimia 67 kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi vifo 2,079 mwaka 2019.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema tangu awe Waziri hajawahi ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi