loader
Picha

Wizara yafafanua riba, penati mikopo elimu ya juu

MIKOPO ya Elimu ya Juu inayotolewa na serikali haitozwi riba wakati wa urejeshaji wake, kama ilivyo kwa mikopo inayotolewa na taasisi za fedha za kibiashara, ambazo hutoza riba kati ya asilimia 14 hadi 22.

Haya yalileezwa bungeni jana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa kujibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Rehema Migilla (CUF).

Migilla alisema,”Kumekuwepo na ongezeko la riba na penati nyingi kwa wanufaika wa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ambao wamemaliza vyuo na wanadaiwa.”

Hivyo, Migilla alitaka kujua mpango wa serikali wa kupunguza riba na penati hizo ili kuwanusuru waathirika. Wizara hiyo ilisema urejeshaji na utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo Sura 178.

Kufuatia marekebisho ya sheria ya mwaka 2016, kwa sasa sheria hii inaelekeza wanufaika wote kuanza kurejesha mikopo yao baada ya miezi 24 tangu walipohitimu masomo yao, badala ya miezi 12.

Aidha, wanufaika ambao watapata ajira ndani ya miezi 24 baada ya kuhitimu, hivi sasa wanawajibika kuanza kurejesha mara baada ya kuajiriwa.

“Kwa wanufaika waliojiajiri au waliopo katika sekta isiyo rasmi, sheria inaelekeza kurejesha Sh 100,000 au asilimia 10 ya kipato cha mwezi wanacholipia kodi,” ilisema wizara.

Aidha kwa mujibu wa sheria hiyo, mnufaika ambaye hataanza kurejesha mkopo miezi 24 baada ya kuhitimu, adhabu yake ni malipo ya asilimia 10 juu ya deni la msingi.

“Mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na serikali haitozwi riba wakati wa urejeshaji wake kama ilivyo kwa mikopo inayotolewa na taasisi za fedha za kibiashara ambazo hutoza riba kati ya asilimia 14 hadi 22.

“Mikopo ya elimu ya juu ya serikali hutozwa asimilia 6 kama Tozo ya Kutunza Thamani ili kutunza thamani ya fedha za mkopo. Tozo hii hukatwa kwenye deni la msingi kadri linavyopungua na husaidia marejesho kuwa na thamani ya kuweza kutumika kuwakopesha watanzania wengine wahitaji,” ilisema wizara.

Wizara ilitoa wito kwa wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu, kujitokeza kwa wakati na kuanza kurejesha mikopo. Pia iliwakumbusha waajiri kuhakikisha makato yote kutoka kwa wanufaika, yanawasilishwa kwa Bodi ya Mikopo ndani ya siku 15, baada ya kila mwisho wa mwezi, kama inavyoelekezwa na sheria.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema tangu awe Waziri hajawahi ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi