loader
RC aagiza ukaguzi miradi Halmashauri 8

RC aagiza ukaguzi miradi Halmashauri 8

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amewapongeza madiwani, Mbunge na watalaamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa kupata hati safi ya hesabu kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya hesabu za mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,2019.

Mndeme alitoa pongezi hizo wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Tunduru katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu hoja na mapendekezo ya hesabu kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 mjini Tunduru.

“Kupata hati safi ni matokeo ya utendaji kazi mzuri wenye mshikamano na ushirikiano kati ya watalaam wa halmashauri na madiwani. Hii inatokana na halmashauri kuundwa na pande mbili, inapotekea mnafanya vizuri, hata viongozi katika ngazi ya mkoa tunafarijika, hongereni sana,” alisema Mndeme.

Hii ni mara ya tano mfululizo kwa halmashauri ya wilaya ya Tunduru kupata hati safi kuanzia mwaka wa fedha wa 2014/2015 hadi 2018/2019. Mndeme amesema kupata hati safi iwe chachu kufanya vizuri zaidi.

Mndeme amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Steven Ndaki kuhakikisha miradi yote ya maendeleo katika halmashauri nane za mkoa wa Ruvuma inakaguliwa na kufanyiwa tathimini.

“Iwapo kuna uzembe uliosababisha miradi kutotekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa nipate taarifa ya hatua stahiki zilizochukuliwa kwa watumishi wazembe kabla au ifikapo Septemba 30, 2020,” alisisitiza.

Mndeme pia alimwagiza kutafuta sababu za hoja za aina moja kujitokeza mara kwa mara na ambazo hazijafungwa na kupata majina ya waliohusika na hatua walizochukuliwa kabla ya Juni 30, mwaka huu.

foto
Mwandishi: Muhidin Amri, Tunduru

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi