loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

'Walidandia treni kwa mbele sasa hali ngumu'

MAAMUZI ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutofungia wananchi wake na kuwaacha waendelee kujishughulisha na mambo yao ya kiuchumi, yamesaidia serikali kuendelea kuwa na uwezo wa kulipia huduma zinazotolewa nchini.

Hali hiyo imewezesha serikali kulipa madeni ya wazabuni, wakandarasi na malimbikizo ya wafanyakazi, yanayofikia Sh trilioni moja na Sh bilioni 670 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu.

Malipo hayo yamefanyika baada ya kufanyika kwa uhakiki wa madeni halali yanayodaiwa na wafanyakazi na watoa huduma mbalimbali.

Hayo yamesemwa jana na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas wakati akizungumzia mafanikio yaliyotokana na maamuzi sahihi ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu, unaosababishwa na virusi vya corona.

Alisema pamoja na changamoto zinazoonekana sasa, lakini maamuzi sahihi ya kuwaacha watu waendelee na shughuli zao za kiuchumi huku wakichukua tahadhari kwa mujibu wa maagizo ya wataalamu wa afya, yameliokoa taifa kuingia katika mdororo wa kiuchumi na serikali kushindwa kujiendesha.

Alisema mataifa mengi duniani, yaliyochukua uamuzi wa kufungia watu wake, yamelazimika kukimbilia mikopo na mengine kupunguza hata mishahara ya watumishi wake, kutokana na changamoto za ugonjwa huo na hasa kuwafungia wananchi bila kufanya uzalishaji.

Dk Abbas alisema katika kipindi kilichoishia Aprili, serikali imeweza kulipa Sh bilioni 597 za malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa serikali na pensheni kwa waliostaafu.

“Kama tungefungia watu, hali hii isingeliwezekana” alisema Dk Abbas ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Pia, alisema seikali imelipa marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) Sh bilioni 173.7, ambapo awali serikali ilipanga kulipa Sh milioni 100. Pia wakandarasi na watoa huduma mbalimbali wamelipwa Sh bilioni 900.

Dk Abbas alisema serikali imeweza kulipa kiasi chote hicho cha fedha, licha ya nchi kukumbwa na changamoto ya mlipuko wa corona. Alisema nchi haikuwafungia wananchi, kama zilivyofanya nchi nyingine, zikiwemo nchi jirani za Afrika Mashariki.

“Serikali ipo imara, haijashindwa kulipa mishahara kwa watumishi wake, kuna nchi nyingine wamepunguzana kazini, wamekatana mishahara, hawajafanya kwa kupenda, sio kwamba wamepaniki, hali ni ngumu,” alisema Msemaji huyo wa Serikali.

Alisema hali tete katika nchi hizo, imetokana na kuwafungia wananchi wake kufanya shughuli za uzalishaji.

Lakini, alisema hatua ya Rais Dk John Magufuli kuamua kutofunga nchi na watu kuendelea na shughuli zao kama kawaida, imewezesha serikali kufanikiwa kulipa kiasi hicho kikubwa cha fedha huku ikiendelea kutekeleza miradi yake mbalimbali, ikiwemo ya maji, barabara na mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere.

“Huwezi kutekeleza miradi yote hii kama unafungia watu, unazuia biashara. Tutafakari manufaa ya nchi yetu kujiepusha na kudandia gari kwa mbele, kudandia treni kwa mbele kwa kuweka zuio,” alisema

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi