loader
Tanzania yamaliza uhaba vitunguu Kenya

Tanzania yamaliza uhaba vitunguu Kenya

WAFANYABIASHARA wa vitunguu nchini Kenya, wamefurahishwa na kumalizwa kwa matatizo ya madereva mpakani, yaliyosababisha kuadimika kwa vitunguu kutoka Tanzania.

Tangu serikali ya Kenya ifunge mpaka wake na Tanzania, wafanyabiashara wa vitunguu katika masoko mbalimbali nchini Kenya, wamekuwa wakilalamika kuwa kumekuwa na uhaba mkubwa wa vitunguu na vichache vilivyopo, vimepanda bei maradufu.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, bei ya vitunguu imepanda kwa asilimia 86 tangu kufungwa kwa mpaka wa Tanzania, ambako asilimia kubwa ya vitunguu vinavyotumika Kenya vinatoka.

Wakizungumza na vyombo vya habari vya Kenya, vilivyokuwa vikifuatilia hali ya bidhaa hiyo nchini humo, wafanyabiashara katika masoko mbalimbali walisema vitunguu vimepanda bei kutoka shilingi za Kenya 55 hadi Shilingi 156 kwa debe moja.

“Kuna uhaba wa vitunguu uliosababishwa na kufungwa kwa mpaka wa Tanzania na Kenya, hali ambayo imesababisha bei ya vitunguu vichache vilivyopo kupanda bei kwa kiwango kikubwa,” alisema mfanyabishara wa vitunguu katika Soko la Nairobi, Teddy Ngoba.

Waziri wa Kilimo wa Kenya, Peter Munya alikiri uwepo wa uhaba wa vitunguu kutokana na kutokuwepo kwa vitunguu vya Tanzania.

Aliwataka wakulima wa Kenya, kuziba pengo hilo ili kukabiliana na uhaba huo.

“Hii ni nafasi muhimu kwa wakulima wa humu nchini kuzidisha bidii ili kuziba pengo lililoachwa wazi na vitunguu vya nje, ambavyo vilikuwa vikiuzwa bei rahisi,” alisema Munya.

Hata hivyo, kutokana na mapatano yaliyofikiwa kati ya mawaziri wa Tanzania na Kenya kuhusu masuala ya mpaka wa nchi hizo mbili, huenda hali itaanza kurejea kama kawaida katika siku za karibuni.

Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano wa Tanzania , Isack Kamwelwe alisema anaamini tatizo la vitunguu lililojitokeza nchini Kenya, litamalizika kwa kuwa tatizo lililojitokeza mpakani, limepatiwa ufumbuzi kwa maelekezo ya marais wa nchi hizi mbili, Rais Dk John Magufuli na Rais wa Kenya, Uhuru Kwenyatta .

Kamwelwe ndiye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo hayo ya mpakani. Habari zaidi kutoka nchini Kenya zinasema kwamba vitunguu vilivyoko sokoni kwa sasa, ambavyo vinatoka kwa wakulima wa Kenya, ubora wake ni wa viwango vya chini halafu bei yake ni kubwa.

“Kusema ukweli vitunguu vya Kenya ni vidogo na vinalazimishwa viuzwe bei moja na vya Tanzania hali inayowasukuma wafanyabishara kukimbilia vya Tanzania ambavyo ni vikubwa na vina ubora kuliko vya Kenya,” alidai mfanyabiashara wa bidhaa za jumla, Ngoba.

Mfanyabiashara huyo aliomba serikali ya Kenya, kuwaokoa wakulima kwa kuwapa unafuu katika upatikanaji wa pembejeo, ili waweze kushindana na wenzao wa Tanzania katika kulitawala soko la vitunguu.

Alisema msaada wanaoupata wakulima wa Tanzania kutoka katika serikali yao, unawawezesha kuleta ushindani mkubwa katika soko la vitunguu katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, kama vile Rwanda, Uganda na Burundi, kwani wote hao wanategemea vitunguu kutoka Tanzania.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/38a64b9acfb3e2c82921a30dc10e171a.jpg

WADAU wa Sekta ya Kilimo nchini wameshauriwa ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi